Jumapili, Februari 19, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 21 Jamadal-Awwal 1438 Hijria, sawa na Februari 19 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1118 iliyopita, alizaliwa Abu Jaafar Bin Ibrahim Qirwan, maarufu kwa jina la 'Ibn Jazzar' tabibu, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa jografia wa nchini Morocco. Alisoma masomo ya awali kwa baba na ami yake na kadhalika kwa msomi mashuhuri wa zama hizo kwa jina la Is'haq Bin Sulaiman. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye kujitolea sana huku akiandika kitabu alichokipa jina la 'Twibul-Fuqaraa' kilichozungumzia masuala ya tiba. Aidha msomi huyo ameandika vitabu zaidi ya 20 maarufu Zaidi kikiwa ni kile alichokipa jina la 'Risaalat fil-Ibdaalil-Adwiyat' na 'Zaadul-Musaafir.' Abu Jaafar Bin Ibrahim Qirwan alifariki dunia mwaka 400 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 828 iliyopita, alifariki dunia huko Khwarezm, Burhanud-Din Abul-Fath Ali Matrazi, faqihi, mtaalamu wa fasihi na mtaalamu wa lugha maarufu wa karne ya 17 Hijiria. Alizaliwa mwaka 536 Hijiria katika mji huo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Matrazi alikuwa mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Allamah Al-Zamakhshari, mfasiri wa Qur'ani, mtaalamu wa hadithi na lugha katika zama hizo. Alikuwa na ujuzi katika elimu ya Nahau, mashairi, lugha na elimu nyingine za fasihi na dini huku akiwa na wanafunzi wengi katika uga huo. Aliandika kitabu katika fani ya lugha alichokipa jina la 'Al-Maghrib fi Lughatil-Fiqhi.' Mbali na kitabu hicho aliandika pia kitabu cha 'Sharhu Maqaamaat Hariri' na vitabu vingi katika masuala ya lugha.
Siku kama ya leo miaka 544 iliyopita, alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland Nicolaus Copernicus. Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na pia dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake.
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita alifariki dunia Andre Gide, mwandishi na mkosoaji mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 81. Andre Gide alizaliwa mwaka 1869 mjini Paris. Hata hivyo aliishi kwa muda mrefu huko kaskazini mwa Afrika hususan nchini Algeria. Maudhui ya visa vingi mashuhuri vya mwandishi huyo ilitokana na ilhamu ya maisha ya wananchi wa maeneo hayo. Moja ya vitabu vyake maarufu ni kile cha "Nyimbo za Vijijini". Mwaka 1947 alitunukia tuzo ya fasihi ya Nobel.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Norwey Knut Hamsun. Alizaliwa mwaka 1859 katika familia masikini kaskazini mwa nchi hiyo, na alipotimiza miaka 24 aliingia katika uwanja wa uandishi.
Hamsun alisafiri mara mbili kwenda Marekani na akaandika makosa aliyoyaona nchini humo ndani ya kitabu alichokipa anwani ya "Maisha ya Kimaanawi katika Zama Mpya Nchini Marekani." Pia aliandika kitabu kilichopewa jina la "Njaa" ambacho kilibeba tamaduni mbali mbali za dunia. Uandishi wake wa kitabu cha "Matunda ya Ardhini" ulikuwa na nafasi muhimu katika kutunukiwa zawazi ya Nobel mwaka 1920.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita alifariki dunia Deng Xiaoping, kiongozi wa zamani wa China na mhandisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wa Xiaoping China ilifanya mageuzi makubwa katika nyanja za kiuchumi na kisiasa ambapo alifanya marekebisho makubwa katika uchumi wa kisoshalisti wa wakati huo wa China na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko. Wakati huo China ilifanikiwa kuingia katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kutatua migogoro iliyokuwepo katika uhusiano wake na nchi kadhaa za dunia. Deng Xiaoping alijiuzulu mwaka 1990 kutokana na maradhi na umri wake mkubwa na hadi anafariki dunia alikuwa akihesabiwa kuwa shakhsia mkubwa na mashuhuri zaidi wa China.
Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe Mosi Esfand 1366 Hijria Shamsia kwa mujibu wa kalenda ya Iran, ndege moja ya abiria ya nchi hii ilishambuliwa na kutunguliwa kwa kombora la majeshi ya utawala wa kidikteta wa Saddam Hussein wa Iraq na kuangushwa, wakati wa vita vya kichokozi vya nchi hiyo dhidi ya Iran. Katika tukio hilo, Hujjatulislam Fadhlullah Mahallati, mwakilishi wa Imam Khomeini kwenye Kikosi cha Kulinda Mapinduzi ya Kiislamu Sepah aliuawa shahidi akiwa pamoja na viongozi na wabunge 39 wa Iran.