Feb 21, 2017 08:41 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (152)

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kujinga nasi katika sehemu hii ya 152 katika mfululizo wa vipindi hivi vya itikadi ya Kiislamu.

Kipindi cha juma hili kitaendelea kujadili suala ambalo tumekuwa tukilizungumzia katika vipindi vinane vilivyopita ambapo tunajaribu kujibu swali ambalo tuliuliza mwanzoni mwa vipindi hivyo kuhusiana na majukumu ulionayo Umma wa Kiislamu kuwahusu Maimamu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) au kwa ibara nyingine haki zao kwa Umma huu. Tulifahamu kupitia aya za Quráni pamoja na hadithi tukufu, manane kati ya majukumu au haki hizo ambazo ni: Haki ya utiifu mutlaki kwao na haki ya kuwarejea ili wapate kutatua tofauti na kila aina ya ugomvi unaozuka miongoni mwetu kwa sababu wao ni sawa na Quráni Tukufu na ndio wanaofahamu vyema ufafanuzi na sheria zake kuliko Waislamu wengine wote. Haki ya kuwaswalia pamona na bwana wao, al-Mustafa (saw), haki ya kuwapenda kama inavyotuamrisha Quráni Tukufu na haki ya kuwatukuza na kuwaenzi kwa sababu wana nafasi adhimu na maalumu mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Haki ya sita ni kuwabai na kujadidisha beia hiyo kwa Imam aliyehai kati yao, haki ya saba ni kuwazuru kwa karibu au mbali wakati wa uhai wao wa dhahiri na wanapoaga dunia na haki ya nane ni haki ya kuwapa khumsi ya kisheria kwa ajili ya kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala. Hivyo basi baada ya kuzijua haki hizi nane, haki ya tisa ni ipi? Endeleeni kuwa pamoja nasi ili tupate kuijua haki hii, karibuni.

 

Wapenzi wasikilizaji, katika maandiko matakatifu kuna sehemu nyingi ambapo Imam Maasumu na asiyetenda dhambi katika kizazi cha Mtume Mtukufu (saw) anatajwa kuwa ni baba wa kimaanawi na kiroho wa Waislamu, na hii ni katika nafasi na vyeo maalumu vya Mtume wetu (saw), cheo ambacho Maimamu (as) wamekirithi kutoka kwake.

Hivyo, kutokana na maandiko haya tunajifunza kwamba kati ya haki za Imam maasumu ni zile haki ambazo Mwenyezi Mungu amezijaalia kwa baba mzazi kutoka kwa watoto wake, kama vile haki za kumfanyia wema, kumtii, kumuheshimu na haki nyingine nyingi ambazo zimetajwa na aya za Quráni na hadithi tukufu kuhusu haki za wazazi. Bali la muhimu tunalojifunza kutokana na maandiko hayo matukufu ni watoto kutekeleza haki za baba mzazi zinazohusiana na Ahlul Beit (as), kwa sababu ubaba wa kimaanawi na kiroho unafungamana na ukombozi na wokovu wa mwanadamu katika maisha yake ya humu duniani na huko Akhera na kwa hivyo ni muhimu zaidi kuliko ubaba unaotokana na kizazi. Imam Maasumu kama alivyo Mtume wa Rehema (saw) hutekeleza majukumu kama yale ambayo yanatekelezwa na baba mzazi katika kuwaongoza watoto wake kuelekea haki na kuwalea kwenye njia nyoofu na kuwaepusha na madhara. Huyatekeleza majukumu hayo yote kwa moyo mkunjufu na kwa njia kamilifu zaidi na kwa msingi huo katika kujibu wema huo, watoto nao, ambao kwa hakika ni Waislamu wote, wanapasa kumtendea wema, kumtii na kumuheshimu kwa njia kamilifu zaidi.

Kwa msingi huo inabainika wazi kuwa matokeo ya kumuasi na kutomtii  Imam maasumu, ambaye ni baba wa kiroho na kimaanawi, ni mabaya zaidi kuliko kumuasi baba mzazi, na hili ni jambo ambalo limebainishwa na kusisitizwa wazi na maandiko matakatifu ambayo tutakusomeeni baadhi hivi punde, hivyo endeleeni kuwa nasi.

 

Wapenzi wasikilizaji, Allama Bahrani amenukuu katika kitabu chake cha ‘Ghayat al-Maraam’ hadithi ya Mtume Mtukufu (saw) ambayo imepokelewa kwa njia za Ahlu Sunna kwamba alimwambia wasii wake Imam Ali (as): ‘Ewe Ali! Mimi na wewe ni baba wa Umma huu, hivyo laana ya Mwenyezi Mungu imshukie anayewaasi wazazi wake.’ Na Faqihi bin al-Maghazili as-Shafi’I katika kitabu cha al-Manaqib na Ibn Asakir ad-Dimashki katika kitabu chake cha Tarikh ad-Dimashk na wengineo katika wanazuoni wa Kisunni wananukuu hadithi kutoka kwa Mtume (saw) kwamba alisema: ‘Haki ya Ali kwa Waislamu ni kama haki ya mzazi kwa mwanawe.’ Naye Shaadhan bin Jabrail ananukuu hadithi ndefu katika kitabu cha ar-Raudhwa kutoka kwa Asbagh bin Nabata anayezungumzia kifo cha Imam Ali (as) kwamba baada ya kupigwa upanga akiwa anaswali katika Msikiti wa al-Kufa nchini Iraq ya leo, Imam (as) alimuhadithia hadithi ndefu kutoka kwa Mtume (saw). Sehemu ya hadithi hiyo ya Mtume (saw) inasema: ‘Ewe Aba al-Hassan! Hakika mimi na wewe ni baba wa Umma huu, hivyo mtu anayetuasi basi na laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, hakika mimi na wewe ni Maula –yaani Mabwana – wa Umma huu, basi anayejitenga nasi laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake. Hakika mimi na wewe ni waajiriwa - yaani wahudumu – wa Umma huu hivyo anayetudhulumu ujira (malipo) wetu - yaani mahaba – laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake.’

Naye Hafidh as-Sarawi al-Halabi ananukuu katika kitabu cha al-Manaqib riwaya kadhaa kutoka kwa wanazuoni wa Kisunni ambazo zina madhumuni hayohayo tuliyotangulia kuyaashiria, na miongoni mwa riwaya hizo ni hii ambayo imenukuliwa kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kwamba alisema: ‘Ewe Ali! Mimi na wewe ni baba wa Umma huu na hakika haki yetu kwao ni kubwa zaidi kuliko yaki ya wazazi kwa wana wao. Hii ni kwa sababu tutawaepusha na moto iwapo watatutii na kuwapeleka kwenye makao ya kudumu na kuwakutanisha huko katika ibada na wabora wa watu walio huru.’ Kisha al-Hafidh al-Halabi ananukuu maelezo yaliyobainishwa na mmoja wa maulamaa wa Kisuni kuhusiana na hadithi hii, ambaye ni al-Qadhi Abu Bakr Ahmad bin Kamil akisema: ‘Yaani Mtume (saw) anakusudia kwamba haki ya Ali kwa kila Mwislamu ni kutomuasi kamwe.’

 

Marehemu Ayatullah as-Sayyid Shihab ad-Deen al-Mar’ashi an-Najafi (MA) amekusanya katika juzuu ya sita na nyinginezo katika kitabu cha Mulhaqaat Sharh Ih’qaqul Haq, vyanzo vingi vya Ahlu Sunna ambavyo vimenukuu hadithi hii ya ‘Ewe Ali! Mimi na wewe ni baba wa Umma huu.’

Na hadithi hii tukufu imenukuliwa pia na vitabu vingi vya madhehebu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) yaani Shia. Jambo hili linatosha kuthibitisha kwamba hadithi hii imepokelewa kwa wingi katika madhehebu zote mbili za Kiislamu na linatuongoza katika kuamini kuwa haki hii ni miongoni mwa haki muhimu za Maimamu wa Ahlul Beit wa Mtume Muhammad (as). Hili ni suala ambalo tutalijadili kwa kina katika kipindi chetu kijacho cha Maaswali Yetu na Majibu ya Thaqalain Inshallah. Basi hadi wakati huo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka hapa mjini Tehran kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.