Jumapili, 26 Februari, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 28 Jamadal-Awwal 1438 Hijria mwafaka na Februari 26, mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 215 iliyopita, yaani mwaka 1802 alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa Victor Hugo. Alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25. Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki dunia mwaka 1885.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alifariki dunia marjaa na mwanamapambano mkubwa wa Kishia Ayatullah Mirza Mohammed Hassan Husseini Shirazi. Ayatullah Shirazi alizaliwa tarehe 15 Jamadul-Awwal mwaka 1230 Hijiria huko mjini Shirazi Iran. Akiwa na miaka minne alianza kujifunza kusoma, huku akihitimu masomo ya msingi akiwa na umri wa miaka minane. Akiwa na umri wa miaka 15 alianza kufundisha elimu ya fiqhi kupitia kitabu mashuhuri katika uwanja huo cha 'Limuat Dimashqiyyah' na baada ya hapo alifanya safari mjini Isfahan. Aidha akiwa na umri wa mika 29 Ayatullah, Mirza Mohammed Hassan Husseini Shirazi alifika mjini Karbala, Iraq na baadaye mjini Najaf na kusoma kwa maulama wakubwa wa miji hiyo kama vile Sheikh Murtadha Answari. Baada ya kufariki dunia mwalimu wake huyo hapo mwaka 1281 Hijiria, Ayatullah Husseini Shirazi alichukua uongozi wa Waislamu wa Shia kwa kipindi cha miaka 30 ambapo alitatua matatizo ya watu na kuongoza Hawza ya kielimu mjini hapo Najaf. Moja ya matukio yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha uongozi wake ni harakati ya kupiga marufuku tumbaku iliyomlazimu mfalme wa wakati huo wa Iran kuvunja mkataba wa tumbaku na wakoloni.
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, alifariki dunia, mvumbuzi wa Marekani kwa jina la Richard Jordan Gatling. Getling alizaliwa mwaka 1818 na katika umri wake alifanya vumbuzi kadhaa moja wapo ikiwa ni bunduki iliyopewa jina lake ya Getling. Bunduki ya Getling ina mabomba kadhaa ambayo baada ya ufyatuaji kila moja huzunguka na kuachia risasi kwa hatua na kwa utaratibu huo kuipa uwezo wa kufyatua risasi nyingi kwa wakati mmoja. Mzunguko wa mabomba hayo ulitengenezwa na Richard Jordan Gatling mwenyewe.
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, yaani mwaka 1921 kulisainiwa mkataba wa kirafiki baina ya Iran na Urusi ya zamani. Katika mkataba huo ambao ulisainiwa baada ya miaka minne ya mapinduzi ya Muungano wa Sovieti ya zamani, Moscow ilitangaza kwamba, haingeendelea na siasa za kikoloni dhidi ya Iran zilizokuwa zikifuatwa na utawala wa Tzar nchini humo. Kwa mujibu wa kifungu hicho muungano huo wa zamani uliacha kutekeleza mikataba ya awali iliyokuwa inaidhuru Iran. Katika mkataba huo wa urafiki Moscow ilitangaza kwamba haingetambua tena mikataba yote iliyotiwa saini na utawala wa tatu wa Tzar dhidi ya Iran. Hata hivyo Urusi ya zamani haikuipatia Iran ardhi za Caucasia na Turkmenistan zilizopo kaskazini magharibi na mashariki mwa Iran. Aidha katika mkataba huo Iran iliahidi kutoruhusu nchi nyingine kutumia ardhi yake dhidi ya Urusi. Itakumbukwa kuwa, Urusi kipindi hicho ilikuwa inakabiliwa na vitisho vya nchi za Magharibi.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, aliuawa shahidi Hossein Kharrazi, mmoja wa makamanda muhimu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran. Mwaka mmoja baada ya kujiri mapinduzi ya Kiislamu, shahidi Kharrazi aliteuliwa katika nafasi hiyo na miezi michache baadaye akatumwa katika eneo la Kordistan katika harakati ya kulinda Mapinduzi ya Jamhuri ya Kiislamu. Baada ya kuanza vita vya kulazimiwa na kutekwa mji wa Khorramshahr na askari wa Iraq, shahidi Kharrazi alitumwa kwenda mjini Khuzestan na kuandaa kikosi cha wanamapambano kwa ajili ya kuwazuia askari hao vamizi. Operesheni za Thaminul-Aimmah, Fat'hul-Mubin, Baytul-Muqaddas, Khaibar, Badr, al-Fajru 8 na Karbalaa 4 na 5 zilifanyika kwa uongozi wa kamanda huyo shupavu. Shahidi Hossein Kharrazi alifariki dunia katika operesheni za Karbala 5 wakati akiongoza kikosi cha 14 cha Imamu Hussein (as), katika siku kama ya leo.
Na mwaka mmoja uliopita katika siku kama ya leo alifariki dunia, mwongozaji filamu mashuhuri wa filamu za kidini, Farajullah Salahshoor. Farajullah Salahshoor, alizaliwa mwaka 1953 katika mji wa Qazvin hapa nchini Iran. Alianza kujishughulisha na sanaa ya filamu kwa kuanzia katika uigizaji wa filamu za sinema katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yaani baada ya mwaka 1979. Baadaye alianza kutengeza filamu za kidini kama vile kisa cha Nabii Ayyub (as), As'habul-Kahf na Nabii Yusuf (as). Wakati akiwa anaumwa Farajullah Salahshoor alikuwa anaandaa kisa cha Nabi Mussa (as). Salahshoor alifariki dunia kutokana na maradhi ya saratani.