Maswali yetu na Majibu ya Thaqalain (153)
Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kama tulivyokuahidini katika kipindi kilichopita, kipindi che leo kitakamilisha jibu kuhusu wajibu au haki ya tisa waliyonayo Maimamu wa Ahlul Beit (as) kwa Umma wa Kiislamu. Hiyo ni haki ya ubaba wa kimaanawi kwa Umma.
Aya za Quráni na hadithi tukufu kutoka madhehebu zote mbili za Kiislamu zinafafanua na kusisitiza wazi kwamba kila Imam maasumu katika Maimamu waliomrithi Mtume Mtukufu (saw) ana haki ya ubaba wa kimaanawi na kiroho kwa Waislamu kama aliyvokuwa nayo Mtume (saw) katika Umma wa Kiislamu. Suala hili linaashiriwa wazi na hadithi mashuhuri ambayo imepokelewa na madhehebu zote mbili ambapo Mtume Mtukufu (saw) amepokelewa akisema: ‘Ewe Ali! Mimi na wewe ni baba (wawili) wa Umma huu.’ Na kadhalika kauli yake (saw): ‘Haki ya Ali kwa Waislamu ni kama haki aliyonayo mzazi kwa mwanawe.’ Kuna hadithi nyingine nyingi kama hizi katika vyonzo na vitabu vya kuaminika katika pande zote mbili za Shia na Sunni. Katika kipindi kilichopita tuliashiria na kunukuu hadithi kadhaa kutoka madhehebu ya Sunni kuhusu suala hili na leo tutataja baadhi ya hadithi za madhehebu ya Shia zinazobainisha madhumuni hayahaya, karibuni.
**********
Sheikh Swaduq (MA) amenukuu katika kitabu cha al-Aamali hadithi ya Mtume (saw) alipomuhutubu Imam Ali (as) kwa kusema: “Ewe Ali! Wewe ni ndugu yangu na mimi ni ndugu yako. Mimi ni al-Mustafa kwa ajili ya Utume na wewe ni al-Murtadha kwa ajili ya Uimamu. Mimi ni mwenye ufunuo (uteremsho) – yaani Quráni iliyoteremshwa – na wewe ni mwenye kuifafanua – yaani uliye na ujuzi na maarifa ya makusudio ya Quráni. Na mimi ni wewe ni baba (wawili) wa Umma huu.” Mtume (saw) amenukuliwa pia katika kitabu cha Kamal ad-Deen akisema katika hadithi: ‘’Mimi na Ali ni baba wa Umma huu. Mtu anayetujua huwa amemjua Mwenyezi Mungu Mtukufu na anayetukana huwa amemkana Mwenyezi Mungu Mtukufu. Watatokana na kizazi cha Ali, mabarobaro na mabwana wawili wa vijana wa Peponi ambao ni Hassan na Hussein. Na katika kizazi cha Hussein watatokea Maimamu tisa ambao utiifu kwao ni sawa na utiifu kwangu na kuasiwa kwao ni sawa na kuasiwa mimi. Wa tisa wao ndiye atakayekuwa Imam wa zama na Mahdi wao.” Kuna hadithi nyingi mno kuhusiana na suala hili ambapo baadhi ya maana ya hadithi hizo zinafungamanishwa na maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu yenye thamani kubwa kama vile ya ‘kuwatendea wema wazazi wawili.’
Imepokelewa katika vitabu vya Tafsir al-Ayashi, Ali bin Ibrahim, Faraat al-Kufi, al-Kafi, Maani al-Akhbar na vitabu vingine muhimu vya kuaminika kwamba maana halisi ya maneno, ‘wazazi wawili’ ambao Mwenyezi Mungu anatuamuru kuwatendea wema ni Mtume Muhammad (saw) na Imam Ali (as) kama anavyothibitisha jambo hilo Mtume mwenyewe (saw). Jambo hili bila shaka linathibitisha kwamba kutekeleza majukumu na haki za ubaba huu wa kimaanawi na kiroho ni muhimu zaidi kuliko utekelezaji wa haki za ubaba wa kizazi. Hili ndilo suala linalosisitizwa na hadithi nyinginezo ambazo zimenukuliwa na al-Allama al-Majlisi na wengineo kuhusiana na tafsiri ya Imam al-Askari (as), ambapo tutakutajieni baadhi ya hadithi hizo hivi punde, hivyo basi endeleeni kuwa pamoja nasi.
Imam al-Askari (as) anasema katika tafsiri yake kutoka kwa Bwana Mtume (saw) katika kubainisha makusudio aali ya maneneo ya Mwenyezi Mungu anapotutaka tuwatendee wema wazazi wawili kwa kusema: ‘Mbora wa wazazi wenu wawili na wanaostahiki zaidi shukrani zenu ni Muhammad na Ali.’
Na Imam Ali (as) amepokelewa katika kitabu cha al-Kafi akisema: ‘Wazazi wawili ambao Mwenyezi Mungu amewajibisha shukrani kwao ni wale waliozalisha elimu, kurithi hukumu na watu kuamrishwa kuwatii.’
Na katika hadithi moja iliyopokelewa kutoka kwa Bibi Fatuma az-Zahra (as) kuna ishara ya kuvutia kwamba kuzingatiwa kwa haki za ubaba wa kimaanawi wa Mtume na Imam maasumu kunatokana na ukamilifu wa malezi yao kwa umma wa Kiislamu, kama anavyowalea watoto wake baba mzazi, na kutokana na kuuonyesha umma huo njia ya wokovu na ufanisi. Bibi Fatuma (as) anasema katika hadithi hiyo: ‘Muhammad na Ali ni baba (wawili) wa Umma huu. Iwapo utawafuata wawili hao, wataukomboa na kuuepusha na upotovu wa humu duniani na adhabu ya kudumu milele ya Alhera; na kuwanufaisha na neema nyingi tofauti na za kudumu milele huko Peponi.’
Naye Imam Hassan al-Mujtaba (as) amesema: ‘Muhammad na Ali ni baba wa Umma huu. Heri kwa yule anayetambua haki yao na kuwatii katika kila hali! Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu atamjalia kuwa miongoni mwa waja bora zaidi wanaoishi kwenye Pepo zake na kumpa saada ya ukarimu na radhi zake.’
Imam Baqir (as) amesema: ‘Mtu anayetaka kujua thamani yake – yaani nafasi yake – mbele ya Mwenyezi Mungu basi na anatazame thamani ya baba wake wawili walio bora kwake, Muhammad na Ali (as) ni ya kiwango gani.’
Na Imam Sajjad (as) amesema: ‘Kama ukubwa wa haki ya wazazi inatokana na ihsani yao kwa watoto wao basi ihsani ya Muhammad na Ali kwa umma huu ni adhimu na kubwa zaidi na kwa hivyo wao wanastahiki zaidi kuwa wazazi.
Ndugu wasikilizaji, muhtasari wa mambo tuliyoyasoma kutokana na hadithi tulizosoma katika kipindi cha leo na nyinginezo nyingi ni kuwa Imam (as) akiwa ndiye mrithi halisi wa hukumu za Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mtume wake (saw), ndiye anayesimama sehemu stahiki ya kuwa baba wa kimaanawi wa watu na ndiye anayewasaidia katika kuwaonyesha na kuwaongoza kwenye njia salama na nyoofu kuelekea saada ya milele, kama anavyotaka Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa msingi huo Waislamu wote wanatakiwa kuheshimu na kutekeleza haki zote za baba huyo wa kimaanawi (as) kwa njia bora na kamilifu zaidi kuliko wanavyofanya kuhusiana na baba zao wazazi.
Na kwa muhatasari huo wasikilizaji wapenzi ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kulichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakutakieni nyote usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia, kwaherini.