Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (155)
Assalaam Aleikum Wapensi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kama mnavyokumbuka ni kuwa bado tunaendelea kujibu swali tulilouliza katika vipindi 11 vilivyopita ambalo linahusiana na majukumu pamoja na nyadhifa walizonazo Waislamu kwa Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (saw).
Swali hilo linasema je, ni wajibu gani ulionao Umma wa Kiislamu kwa Ahlul Beit wa Mtume (as) au ni haki gani walizonazo (as) kwa Umma wa Kiislamu? Tulizungumzia kwa kina sehemu ya jibu la swali hili katika vipindi vilivyopita kwa kutegemea aya za Quráni pamoja na hadithi tukufu ambapo tulichunguza na kufafanua kumi kati ya haki hizo za lazima.
Kutokana na umuhimu wa kivitendo wa suala hili, tutatenga kipindi cha juma hili kuzungumzia kwa muhtasari haki hizo kumi ambazo tulizijadili katika vipindi vilivyopita kwa msingi wa aya za Quráni na hadithi tukufu, huku tukitilia mkazo umuhimu mkubwa wa kutekelezwa na kuheshimiwa haki hizo, karibuni.
Wapenzi wasikilizaji, tunaashiria mwanzoni mwa kipindi hiki suala muhimu sana ambalo linafungamana na haki zote za Maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume (as) nalo ni kwamba haki zao hizo zinatokana na haki za bwana wao na mbora wa viumbe vyote al-Habib al-Mustafa (saw). Suala hili linatokana moja kwa moja na aya za kitabu kitukufu cha Quráni ambacho kwa mfano kinafungamanisha moja kwa moja utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale waliopewa haki ya uongozi na utiifu miongoni mwa kizazi cha Mtume, na kufungamanisha mapenzi kwa Mtume (saw) na mapenzi kwa Maimamu watoharifu wa kizazi hicho, Maimamu ambao yeye mwenyewe Mtume alisisitiza na kutilia mkazo kwamba walitokana na kizazi chake. Watukufu hawa ni wale ambao Mwenyezi Mungu amesisitiza katika aya za kitabu hicho kitakatifu kwamba wametoharishwa na kuwekwa mbali na kila aina ya dhambi. Katika hilo wapenzi wasikilizaji kuna sisitizo hili linaloashiria kwamba majukumu ya Maimamu wa Ahlul Beit (as) ni mwendelezo wa majukumu ya Mtume (saw). Kwa ibara nyingine ni kwamba Maimamu (as) ni mawasii na makhalifa wa Mtume Mtukufu (saw) katika umma wake ambao hulinda sunna zake na kuwaongoza waja kwenye njia nyoofu inayofuatilia kufikiwa malengo matukufu ya Mtume katika kusimamisha uadilifu wa Mwenyezi Mungu kwa njia bora zaidi, katika mtazamo wa mtu binafsi na vilevile mtazamo wa kijamii. Kwa msingi huo tunafahamu kwamba utekelezaji wa Waislamu majukumu yanayotokana na haki hizo za Maimamu kwa hakika ndio msingi wa kutekeleza ibada ya Mwenyezi Mungu na kufuata kikamilifu dini yake tuliyoletewa na Mtume Muhammad (saw). Katika kufanya hivyo waja huwa wamefikia daraja ya juu ya kumwabudu Mwenyezi Mungu jambo ambalo huwaletea ufanisi na saada maishani kama ambavyo kuheshimu na kutekeleza haki hizo ni mshikamano wa wazi wa wilaya ya watu wanaolinda dini ya haki na ni alama ya msaada wao kwa Maimamu wa kizazi cha Mtume ambao ndio wanaomtetea na kufuatilia kwa juhudi zao zote malengo ya ujumbe wake wa mbinguni.
Ndugu wasikilizaji, haki ya kwanza ya Ahlul Beit wa Mtume (as) kati ya zile haki kumi tulizozitaja katika vipindi kumi na moja vilivyopita ni haki ya utiifu mutlaki kwao (as) kwa sababu katika utiifu huo kuna dhihirisho halisi, kamilifu na la moja kwa moja la utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) kama inavyobanisha wazi suala hilo aya ya 59 ya Surat an-Nisaa.
Ama haki ya pili ni haki ya kuwapelekea mashtaka tunapogombana na kuzozana katika jamii ili wapate kutusuluhisha na kutufafanulia hukumu ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na suala ambalo tunazozania. Hili linatokana na ukweli kwamba wao ndio wajuzi zaidi wa hukumu ya Mwenyezi Mungu katika kila jambo linalotokea. Kwa msingi huo wana uwezo wa kufahamu vyema hukumu ya Mwenyezi Mungu kwenye Quráni Tukufu kama inavyobainisha hilo aya ya 83 ya Surat an-Nisaa, na hili ni suala ambalo pia linaashiriwa na hadithi ya Thaqalain ambayo imepokelewa kwa wingi na inayoaminika kuwa ni ya kweli na madhehebu zote mbili za Kiislamu za Shia na Suni.
Haki ya tatu ni haki ya mawadda yaani haki ya kuwapenda Watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw). Wajibu na ulazima wa kutekelezwa haki hii unasisitizwa na aya ya 23 ya Surat as-Shura na hadithi nyinginezo za kuaminika ambazo zinaashiria ulazima wa kupendwa na kuonyeshwa mahaba watoto wanaotokana na kizazi cha Bibi Fatuma na Ali (as). Ni wazi kuwa utekelezwaji wa haki hii, yaani kuonyesha mapenzi kwa Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (as) ndilo dhihirisho la wazi zaidi linalothibitisha na kuimarisha ufuasi kwao kwa ajili ya kufikia malengo ya ujumbe wa mbinguni na ni kutokana na ukweli huo ndipo Mwenyezi Mungu akajalia jambo hilo kuwa na thawabu sawa na zile za kuhubiri ujumbe wa Mtume (saw).
Ama haki ya nne wapenzi wasikilizaji ni haki ya kuwajumuisha watukufu hao katika kumswalia Mtume (saw) na kujiepusha kumswali swala ya mkato, yaani isiyowajumuisha watukufu hao wa kizazi chake kitoharifu, jambo ambalo amelikemea na kulikataza Mtume mwenyewe (saw). Katika suala hili kuna uimarishaji wa mawasiliano ya kiitikadi na kimatendo kati ya imani ya Utume na Uimamu na ukamilifu wa imani na neema kama inavyosisitiza suala hilo aya ya kutangazwa uongozi na wilaya ya Imam Ali (as) katika tukio la al-Ghadir.
Wasikilizaji wapenzi, ama haki ya tano kati ya haki za Maimamu wa Ahlu Beit wa Mtume Muhammad (saw) ni haki ya kukirimu, kutukuza na kuwatangaliza kama walivyowatanguliza Mwenyezi Mungu mwenyewe na Mtume wake Mtukufu (saw). Haki ya sita ni kuwatengea baia (as) na kuitangaza upya kwa kila Imam aliye hai. Maana ya jambo hili ni kuwasaidia na kuwafauata kwa sababu kufanya hivyo ni kumsaidia Mwenyezi Mungu mwenyewe na uongozi wake ardhini. Haki ya saba ni kuwazuru katika zama za uhai wao na wanapokuwa wameaga na kuondoka humu duaniani. Kuwazuru baada ya kuaga kwao dunia hutimia kwa kwa kuyatembelea makaburi yao au kuwazuru kutokea mbali kwa kuwaombea dua na kuwatumia salamu. Kwa kufanya hivyo huwa tumehuisha na kuimarisha maadili na sifa njema za Mwenyezi Mungu ambazo watukufu hao walipigania na kufanya juhudi kubwa za kuzieneza katika zama za uhai wao humu duniani. Ya Nane katika haki hizo ni haki ya kuwatolea khumsi ambayo Mwenyezi Mungu aliwajaalia kama utukufu na msaada wa kufikia maslahi ya dini yake ya haki na pia kuwasaidia waja wake wanaonyenyekea na wasioomba watu. Kutekeleza haki zao za ubaba wa kimaanawi na kiroho ni haki ya tisa, wapenzi wasikilizaji, tunayopasa kuitekeleza sisi Waislamu kuhusiana na kizazi kitoharifu cha Mtume (saw) kama inavyoashiria hilo hadithi ya Mtume ambayo imepokelewa na madhehebu zote mbili za Kiislamu. Hadithi hiyo inasema: ‘Haki aliyonayo Ali kwa Waislamu ni kama haki aliyonayo baba kwa mwanawe. Haki hii inajumuisha mambo yote yanayohusiana na haki ya ubaba, kukiwemo kuwatendea wema, kuwaheshimu na kuwatii, na kwa kawaida ubaba wa kimaanawi na kiroho huwa ni muhimu zaidi kuliko ubaba wa kizazi na wa damu.
Na haki ya kumi ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) ni haki ya kuwaridhisha na kuepuka kuwaidhi na kuwaghadhibisha. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuwaridhisha humridhisha Mwenyezi Mungu na kuwaudhi humuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Hili ni jambo ambalo limesisitizwa sana na hadithi nyingi za Kiislamu.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Mswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.