Jumanne, Aprili 11, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 13 Rajab 1438 Hijria sawa na Aprili 11, 2017 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1461 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa katika nyumba tukufu ya al Kaaba, Ali bin Abi Twalib AS, ambaye ni binamu, mkwe na Khalifa wa Mtume Muhammad (saw). Mama wa mtukufu huyo ni Bibi Fatima bint Assad na baba yake ni Abu Talib. Katika kipindi chake cha utotoni, Ali bin Abi Talib alilelewa na kupata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanaume wa kwanza kuukubali Uislamu. Mwishoni mwa mwaka wa Pili Hijria, Imam Ali AS alimuoa Bibi Fatimatu Zahra binti ya Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alishiriki kwenye vita vyote bega kwa bega na Mtume Mtukufu SAW isipokuwa vita vya Tabuk, na alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume katika hali zote za shida na matatizo. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji asiye na mithili, lakini pia Imam Ali bin Abi Talib alikuwa mpole, mwingi wa huruma na mtetezi wa wanyonge.
Miaka 1159 iliyopita katika siku kama ya leo mwaka 279 Hijria, alifariki dunia Abu Isa Tirmidhi hafidh wa Qur'ani tukufu na mpokeaji hadithi mashuhuri wa Kiislamu. Tirmidhi alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa miaka mingi kwa ajili ya kujipatia elimu ya dini na hadithi. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi hodari wa Imam Bukhari na kitabu chake maarufu zaidi ni Jamiu Tirmidhi. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa miongoni mwa marejeo muhimu ya hadithi katika madhehebu ya Suni.
Miaka 157 iliyopita katika siku kama ya leo, chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre. Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi dawa na vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Katika siku kama ya leo miaka 32 alifariki dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania. Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia. Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti.
Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran. Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekuwa akiishi Ujerumani. Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Takribani miezi kumi baadaye mabalozi wa Umoja wa Ulaya walianza kurejea hapa Tehran mmoja baada ya mwingine.