Jumamosi, Aprili 15, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 17 Rajab 1438 Hijria sawa na Aprili 15, 2017 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 565 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mashuhuri wa kutengeneza vinyago wa Italia Leonardo da Vinci. Mwaka 1461 alianzisha kituo cha uchoraji katika mji wa Florence nchini Italia na hatua kwa hatua akaanza kupata umashuhuri katika uchoraji. Alionesha kipaji kikubwa cha kuchora akiwa bado mtoto mdogo na alikweya daraja za juu katika fani hiyo haraka mno. Mwaka 1506 Miladia da Vinci alichaguliwa kuwa mchoraji wa Mfalme Luis wa 12 kisha akawa mchoraji wa Mfalme Francis wa Kwanza.
Mbali na uhodari wake katika kuchora na kutengeneza vinyago, Leonardo da Vinci pia alisomea fizikia na hisabati. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni michoro ya kanisa kuu la mji wa Milan, mchoro wa picha ya "Tabasamu la Jugund," picha ya Mona Lisa na ya Karamu ya Mwisho ya Issa Masih (as). Leonardo da Vinci alifariki dunia mwaka 1519 akiwa na umri wa miaka 67.
Na miaka 167 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 17 Rajab mwaka 1271 Hijria Qamaria alizaliwa Ayatullahil Udhmaa Sayyid Abuturab Khansari katika mji wa Khansar moja ya miji ya eneo la kati mwa Iran. Alikuwa mwanazuoni mtajika wa Kiislamu. Baada ya kumaliza masomo ya awali alijiunga na vyuo vya kidini mjini Isfahan na Najaf na kunufaika na elimu ya walimu wakubwa wa vituo viwili hivyo. Alikuwa mtaalamu mkubwa katika elimu za fiqhi, usul falsafa na tafsiri na hivyo kufundisha masomo hayo kwa ustadi mkubwa. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha "Misbahus- Swalihin" na "Qasdus-Sabil." Ayatullah Khansari aliaga dunia mwaka 1346 Hijria Qamaria.
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita meli kubwa ya abiria ya Titanic ambayo ilitambuliwa kuwa nembo ya mafanikio makubwa ya viwanda vya meli vya wakati huo iligonga mwamba wa theluji na kugharibi katika Bahari ya Atlantic, katika safari yake ya kwanza kutoka bandari ya Southampon nchini Uingereza ikielekea New York, Marekani. Zama hizo Titanic ilitambuliwa kuwa meli kubwa zaidi na ya kifahari kuliko zote duniani. Watengenezaji wa meli hiyo walikuwa wakisema kuwa haiyumkini kughariki na kuzama. Wasafiri 705 tu kati ya abiria wake wote 2207 ndio waliookoka katika ajali hiyo. Ajali hiyo inatambuliwa kuwa mbaya zaidi ya baharini na iliyosababisha idadi kubwa ya vifo duniani.
Tarehe 15 Aprili 1988, shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel MOSSAD lilimuua shahidi Khalil al Wazir maarufu kwa jina la Abu Jihad mwasisi na shakhsia nambari mbili wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO huko Tunis, Tunisia. Abu Jihad aliongozana na wenzake nchini Misri, na huko wakaamua kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, na kuipatia jina la Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO.
Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuanzisha Shirika la Biashara Duniani (WTO) nchini Morocco. Utangulizi wa kuasisiwa shirika hilo ulifanywa na Marekani na Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kwa msingi huo, mwaka 1947 nchi 23 zilizoendelea zilitia saini makubaliano ya kuanzisha GATT. Makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kufanyika mazungumzo ya kupunguza ushuru wa forodha, vipingamizi vya biashara na kuondoa vizuizi vya biashara huru. Baadaye jumuiya ya GATT ilibadilishwa jina na kuwa WTO na hati yake ilianza kutekelezwa Januari mwaka 1995. Hata hivyo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeliteka nyara shirika hilo la kibiashara duniani na kulitumia kwa faida na maslahi yao wenyewe.
