Apr 17, 2017 07:01 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Apr 17

Karibu tukupashe kwa kina bingwa wa Ligi Kuu ya Soka Iran, matokeo ya Kombe la CAF na msimamo wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza........

Persepolis yatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Iran

Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini baada ya kuichachafya klabu ya Machine Sazi ya Tabriz Jumamosi. Katika kipute hicho cha kukata na shoka, vijana wa Persepolis au ukipenda waite Wekundu wa Tehran waliwabamiza Watengeneza Magari wa Iran mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Yadegare-Imam mkoani Tabriz, kaskazini mashariki mwa nchi, na hiyo kutia kikomo ukame wa miaka tisa wa kutoshinda taji hilo. The Reds walianza kwa kasi nzuri na kutawala mchezo huo, huku kiungo Ali Alipour akifunga moja ya mabao ya mapema zaidi msimu huu, kunako sekundu ya 29.

Wachezaji na wasimamizi wa Persepolis wakisherehekea ushindi

Wekundu wa Iran walipoteza fursa nyingi za wazi kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza huku shuti za kiungo nyota wa klabu hiyo Mehdi Taremi zikikosa kutikisa nyavu. Hata hivyo alifanikiwa kucheka na nyavu kunako dakika ya 69 kupitia mkwaju wa penati, baada ya Alipour kuchezewa visivyo katika sanduku la hatari.

Persepolis ilishinda taji hili kwa mara ya kwanza katika msimu wa ligi ya mwaka 2001-2002 huku wakitwaa ubingwa huo mara ya pili katika msimu wa mwaka 2007 na 2008. Klabu ya Sepahan ndiyo imetwaa Ligi Kuu ya Soka ya Iran inayofahamika pia kama Persian Gulf Pro League mara nyingi zaidi, ikizingatiwa kuwa imetwaa taji hilo mara tano; katika misimu ya mwaka 2002-03, 2009-10, 2010-11, 2011-12 and 2014-15.  Kutokana na kichapo hicho cha Jumamosi, klabu ya Machine Sazi imeshushwa daraja.

Mieleka: Vijana wa Kiirani waibuka wa pili Azerbaijan

Timu ya mieleka ya mabarobaro wa Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyofanyika huko Azerbaijan. Vijana hao wa Iran wameibuka wa pili baada ya kuzoa jumla ya medali 4 katika mashindano hayo ya kuwania Kombe la Shirikisho la Mieleka la Azerbaijan katika safu za Freestyle na Greco-Roman yaliyofanyika katika Ukumbi wa Michezo wa Baku, mji mkuu wa nchi mwenyeji.

Muirani akipambana na hasimu katika mieleka ya Greco-Roman

Mwanamiekea wa Kiirani Abbas Foroutan aliipa Jamhuri ya Kiislamu medali ya dhahabu katika kitengo cha wanamieleka wenye kilo 85 baada ya kuwalemea mahasimu kutoka Kyrgyzstan, Azerbaijan na Uzbekistan. Alireza Abdollahi aliipa Iran dhahabu ya pili katika kategoria wanamieleka wenye kilo 100 baada ya kumpelea mchakamchaka raia wa Georgia. Ashkan Koushki alishinda medali ya shaba baada ya kumdondosha Muirani mwenziwe Amir Hossen Maqsoudi katika safu ya kilo 63 huku Mehdi Khodabakhshi akiipa Iran medali ya mwisho ya shaba baada ya kumlemea mwenyeji Muazeri katika kategoria ya kilo 50. Mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama “Azerbaijan Wrestling Federation Cup” International Freestyle and Greco-Roman Wrestling Tournament  yalianza Aprili 13 na kufunga pazia lake Aprili 16, katika mji mkuu, Baku.

Soka Afrika: Michuano ya CAF

Baada ya klabu ya Yanga ya Tanzania kucheza mchezo wa kwanza wa kuwania kutinga hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho barani Afrika mnamo April 8 uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kufanikiwa kupata ushindi wa goli 1-0, April 15 ilikuwa ni zamu ya kusafiri Algeria katika mchezo wa marudiano. Ni hapa ndipo vijana wa Young Africans walifahamu kilichomtoa kanga manyoa kwa kuwa walipokea kichapo cha mbwa cha mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa katika uwanja wa July 5 1962 mjini Al-Jaza’irYanga ambao waliingia wakiwa wanahitaji sare ya aina yoyote ili waweze kupata nafasi ya kuingia katika hatua ya makundi ya Kombe la CAF, walikubali kipigo hicho na safari yao kuishia papo hapo. Magoli ya MC Alger ambao waliingia uwanjani kwa mchecheto mkubwa yalifungwa na Aouadj dakika ya 14 na 91, Derrardja dakika ya 39 na Zerdab dakika ya 66, na hivyo kuifanya Yanga iondolewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa jumla ya magoli 4-1. Hata hivyo wachezaji wa Yanga akiwemo kipa wa klabu hiyo wamelala kuhusu uendeshaji mbaya wa mechi hiyo. Masaibu ya Yanga hayakuishia hapo kwenye kuchezea mkong'oto, klabu hiyo ilipata pigo jingine nchini Algeria baada ya wachezaji wake kuachwa na ndege baada ya kuchelewa kufika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumediene, jijini Algeirs. Wachezaji hao walikuwa wasafiri na ndege ya Uturuki kupitia Istanbul wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwassa walichelewa kufika uwanjani hapo na hivyo wakalazimika kusubiri keshoye.

Klabu ya Yanga uwanjani

Huku hayo yakirifiwa, klabu ya soka ya CS Sfaxien kutoka Tunisia, imekuwa klabu ya kwanza kufuzu katika hatua ya makundi kuwania taji la CAF. CS Sfaxien ilifika katika hatua hiyo baada ya kuishinda Rail club du Kadiogo ya Burkina Faso kwa mabao 4-1 baada ya mchuano wa mzunguko wa pili siku ya Ijumaa. Mchuano wa kwanza CS Sfaxien ilishinda mabao 2-1 na kupata ushindi mwingine wa mabao 2-0 walipocheza nyumbani. Katika michuano nyingine iliyoshuhudiwa mwishoni mwa wiki, miamba ya soka Afrika, klabu ya Mamelodi Sundown waliizaba Free States Stars bao moja la uchungu na hivyo kuzidi kutuama katika katika nafasi ya pili wakiwa na alama 41, alama nne nyuma ya Cape Town Stars ambayo kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa mashindano hayo. Rivers United ya Nigeria nayo ilifanikiwa kuisasambua Rayon Sport ya Rwanda mabao 2-0 na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Ligi ya EPL

Tunahitimisha kipindi kwa kutupia jicho baadhi ya matokeo ya michuano ya Ligi Kuu ya Soka Uingereza, na namna msimamo wa ligi ulivyo. Mchuano wa hivi karibuni kabisa ambao umezusha mijadala na minong'ono miongoni mwa mashabiki wa spoti ni ule kati ya Manchester United na Chelsea siku ya Jumapili. Man U waliupa maana msemo usemao mcheza kwao hutuzwa, kwani walifanikiwa kuigaragaza The Blues wa Uingereza mabao 2-0 ugani Old Trafford. Magoli ya Mashetani Wekundu yalifungwa na Marcus Rashford kunako dakika ya 7 huku Ander Herrera akipiga msumari wa mwisho kupitia goli lake la dakika ya 49.

Ligi Kuu ya Soka Uingereza EPL

Ushindi huo wa Man United dhidi ya Chelsea ni wa kwanza toka waifunge The Blues mara ya mwisho Oktoba 28 mwaka 2012. Kwengineko, Tottenham iliigeuza Bournemouth kichwa cha mwenda wazimu na kuidhalilisha kwa kuifunga mabao 4-0. Moussa Dembele aliifungia klabu hiyo bao la kwanza, Son Heung-min akapata la pili huku Harry Kane akifunga bao la tatu. Vincent Janssen alipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la mahasimu wao dakika moja moja tu baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba.

Wakati huohuo, kiungo Roberto Firmino alifunga bao la ushindi na kuiwezesha Liverpool kupanda hadi nafasi ya tatu katika jedwali la Ligi. Mshambualia huyo raia wa Brazil aliifungia Liverpool bao hilo katika dakika za lala salama kwenye kipindi cha kwanza walipovaana na West Brom. Everton nayo iliichachawiza Burnley mabao 3-1 wakati ambapo mabingwa watetezi Leicester City walikuwa wanalazimishwa sare ya mabao 2-2 na Crystal Palace.

Licha ya kichapo cha mbwa, Chelsea wanasalia kileleni mwa jedwali la ligi wakiwa na alama 75, pointi nne mbele ya Tottenham. Liverpool kwa sasa hawana budi kutosheka na nafasi ya tatu wakiwa na pointi 66 wakifuatwa unyo kwa unyo na Manchester City yenye alama 64. Man U wanafunga orodha ya tano bora kwa sasa wakiwa na alama 60.

………………………………TAMATI……………………….

 

 

 

 

 

Tags