May 08, 2017 10:18 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Mei 8

Huu ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Iran yaibuka ya 3 Kombe la Dunia, Soka ya Ufukweni

Timu ya taifa ya soka ya ufukweni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya tatu katika mashindano ya Kombe la Dunia ya mchezo huo mwaka huu 2017. Hii ni baada ya kuisasambua Italia mabao 5-3 katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu Jumapili jioni huko Bahamas. Timu mbili hizi awali zilikutana katika hatua ya makundi ambapo Italia iliitandika Iran mabao 5-4. Katika mchezo wa Jumapili, mvua ya mabao ya Iran ilifunguliwa na kiungo Mohammad Ahmadzadeh, hili likiwa bao lake la saba tangu mashindano hayo yaanze. Mchezaji huyo bingwa wa Iran aliongeza la pili katika duru ya pili ya mchezo na hivyo kufikisha idadi ya mabao 8. Bao la tatu la Iran lilipachikwa kimyani na Mohammad Mokhtari. Kufikia hapa Italia walikuwa wamepoteza matumaini kabisa ya kupata bao. Hata hivyo vijana wa Kitaliano walijipapatua na kujikusanya, na kufanikiwa kucheka na nyavu kupitia wachezaji Gabriele Gori, Dejan Stankovic na Dario Ramacciotti. Bao la kiungo wa Iran Moslem Mesigar halikutosha kuipa Jamhuri ya Kiislamu ushindi. Ahmadzadeh alipata mwanya wa kutikisa nyavu ambapo bao lake hilo halikuwa la ushindi tu, bali pia lilimfanya awe amefunga mabao matatu ya hat-trick katika mchuano mmoja na hivyo kutunzwa medali ya shaba.

Bendera ya Brazil

Vijana hao wa Iran walishindwa kutinga fainali ya Kombe la Dunia la Soka ya Ufukweni linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA, baada ya kukung'utwa mabao 3-2 na mahasimu wao wa Tahiti katika ufukwe wa taifa wa Malcolm Park mjini Nassau. Brazil imeibuka wa mashindano hayo ya dunia, baada ya kuidhalilisha Tahiti mabao 6-0.

FIBA yaruhusu mabinti wa Kiirani kushiriki katika mashindano ya kimataifa wakiwa na Hijabu

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani (FIBA) limetangaza kuafiki pendekezo la Iran la kutaka wanawake wa Kiislamu na mabinti wenye Hijabu wa Kiirani kushiriki katika michezo ya kimataifa ya mpira wa kikapu (basketiboli). Mahmoud Mashhoon, Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa, hatimaye Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani (FIBA) limekubaliana na matakwa ya Iran ya wachezaji wake wa kike kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya mpira wa kikapu wakiwa wamejistiri kwa vazi tukufu la Hijabu. 

Mabinti wa Kiirani wamekuwa wakishiri michezo mingine kama taekwondo na mieleka kwa kuruhusiwa Hijabu

Ameongeza kuwa, uamuzi huo wa FIBA umetangazwa katika kikao cha shirikisho hilo kilichofanyika huko Hong Kong. Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kufuatia uamuzi huo, kuanzia Oktoba mwaka huu mabinti wa Kiirani sasa wataweza kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo wakiwa wamejistiri kwa vazi la Hijabu. Ikumbukwe kuwa, Timu ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Kikapu ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran kwa muda sasa haikuwa ikishiriiki katika mashindano ya kimataifa ya mpira wa kikapu kutokana na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Duniani (FIBA) kupiga marufuku wanawake wanaovaa Hijabu kushiriki katika mashindano yanayoandaliwa na shirikisho hilo. 

Mkenya avunja rekodi ya dunia Italia

Mwanariadha mahiri wa Kenya Eliud Kipchoge ameweka muda mpya wa mbio za masafa marefu za marathon baada ya kushinda mbio hizi za kilomita 42 kwa kutumia saa 2:00:26 katika mashindano ya Nike Breaking 2 nchini Italia mapema Jumamosi. Bingwa huyo wa Olimpiki alikaribia kuwa binadamu wa kwanza kutimka umbali huo chini ya saa 2:00:00, lakini akakosa kwa sekunde 26. Kipchoge aliimarisha muda wake bora wa 2:03:05 aliotimka katika London Marathon mwaka 2016. Muda wake pia ni bora kuliko rekodi ya dunia ya saa 2:02:57 ambayo Mkenya mwenzake Dennis Kimetto aliweka katika Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2014. Kipchoge alikuwa hapa aka hapa na bingwa mara mbili wa Boston Marathon, Lelisa Desisa, kutoka Ethiopia, na mshikilizi wa rekodi ya nusu-marathon duniani Zersenay Tadese kutoka Eritrea. Tadese alimaliza katika nafasi ya pili kwa saa 2:06:51 naye Desisa akamaliza mizunguko hii 17 kwa saa 2:14:00. Huku hayo yakirifiwa, nyota mwengine wa riadha raia wa Kenya Hyvin Kiyeng alitimka muda wa kasi wa sita katika historia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji na kunyakua taji la Doha Diamond League nchini Qatar, Ijumaa. Mkenya huyu, ambaye aliibuka bingwa wa dunia mwaka 2015, alishinda wapinzani wake 17 kwa kukamilisha kitengo chake kwa dakika 9:00.12. Alichomoka kabla tu ya kiunzi cha mwisho na kuwabwaga wapinzani wake wa karibu Mkenya Beatrice Chepkoech na mshikilizi wa rekodi ya dunia Ruth Jebet kutoka Bahrain. Wakati huo huo bingwa wa Olimpiki, Caster Semenya wa Afrika Kusini aliendelea kutawala mbio za mita 800 za wanawake akifuatwa unyounyo na Wakenya Margaret Nyairera na bingwa wa zamani wa dunia Eunice Sum katika mashindano hayo ya Diamond League. Muethiopia Genzebe Dibaba alimaliza katika nafasi ya tano katika jaribio lake la kwanza kabisa katika mbio za mita 800. Mwanariadha nyota wa kimataifa Elaine Thompson naye aliibuka kidedea katika safu ya mita 200 upande wa wanawake.

Ligi Kuu ya EPL

Tunafunga kipindi kwa kutupia jicho Ligi Kuu ya Soka Uingereza. Msururu wa klabu ya Manchester United kutofungwa mechi 25 katika Ligi ya Primier ulikatizwa siku ya Jumapili baada ya Mashetani Wekundu kukubali kichapo cha mbwa cha mabao 2-0 kutoka Arsenal katika mchuano wa aina yake. Arsenali ambao walikuwa wanaupiga nyumbani uwanja wa Imarati wasingethubutu kuwabwaga mashabiki, haswa kipindi hiki ambapo klabu imekuwa ikifanya vibaya kiasi cha mashabiki kushinikiza kutimuliwa mkufunzu Arsene Wenger. Kipindi cha kwanza cha mchuano huu kilishuhudia ukame wa mabao licha ya majaribio tasa ya hapa na pale. Hata hivyo vijana wa Jose Mourinho walilegeza kamba baada ya mapumziko na kuruhusu Wabeba Bunduki kufyatua risasi mbili za hasira. Bao la kwanza la Gunners lilifungwa na Granit Xhaka kunako dakika ya 54. Kufumba na kufumbua mchezaji nyota wa Arsenali Danny Welbeck alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Man U kwa bao lake la kichwa katika dakika ya 57. Huu ulikuwa mchuano wa 225 toka timu hizo mbili hasimu zikutane kwa mara ya kwanza Oktoba 13 1894. Gunners imeifunga Red Devils mara 81 na kupoteza mara 96 huku mahasimu hao wakitoka sare mara 47.  

Miamba ya EPL

Licha ya kichapo hicho Man U anasalia katika nafasi ya 5 kwenye msimamo wa Ligi ya EPL ikiwa na alama 65, alama mbili mbele ya Arsenali. Chelsea inasalia kileleni mwa jedwali la ligi ikiwa na pointi 81 ingawaje inatazamiwa kuvuna alama 3 zaidi baada ya kukipiga na Middlesbrough Jumatatu, ikifutwa na Tottenham yenye alama 77. Liverpool na Manchester City wanapelekana unyo kwa unyo katika nafasi ya 4 na tano kwa usanjari huo, zikiwa na alama 70 na 69 mtawalia.

………………………….TAMATI………..………..