Ijumaa, Mei 26, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 29 Shaaban 1438 Hijria Qamaria sawa 26 Mei 2017 Miladia.
Leo ni Ijumaa tarehe tano Khordad mwaka 1396 Hijria Shamsia sawa na 29 Shaaban mwaka 1438 Hijria Qamaria inayosadiiana na 26 Mei 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1219 iliyopita , yaani 29 Shaaban mwaka 219 Hijria Qamaria alifariki dunia Fadhlu Bin Dukin maarufu kwa jina la Ibn Naim, mtaalamu wa hadithi, fiq'hi na mwanahistoria. Ibn Naim aliyezaliwa mwaka 130 Hijiria nchini Iraq, alikuwa mmoja wa wapokezi wa hadithi huku akipewa heshima na maulama wakubwa wa Kiislamu wa enzi hizo. Kitabu cha 'as-Swalat' ni miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1129 iliyopita sawa na 29 Shaaban mwaka 318 Hijria Qamaria alifariki dunia Ibn Mundhir, mtaalamu wa sheria za Kiislamu, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Mundhir alijifunza elimu ya fiq'hi na hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa zama zake huku akifanya safari pia kuelekea mjini Makkah, ambapo alisikiliza na kujifunza elimu ya hadithi hadi mwisho wa uhai wake. Aidha akiwa mjini Makkah alijishughulisha na uandishi wa vitabu tofauti. Katika kitabu cha 'Al-Ijmaa' alibainisha na kufafanua nadharia tofauti za wasomi katika uwanja wa sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei mwaka 1981, kulitangazwa rasmi kuundwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Baraza hilo linazijumuisha nchi 6 za kusini mwa Ghuba ya Uajemi ambazo ni Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Qatar na Oman. Malengo ya kuundwa baraza hilo ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kushirikiana nchi wanachama katika kukabiliana na vitisho vya kigeni.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei mwaka 1881, Ufaransa ilianza rasmi kuikoloni Tunisia. Kabla ya hapo Ufaransa ilianza kupenya Tunisia kupitia harakati za kiuchumi na kibiashara. Aidha kwa miaka kadhaa Tunisia ilikuwa ikidhibitiwa na Ufaransa. Hata hivyo katika muongo wa 1930 Miladia zilianza harakati za kupigania uhuru kwa uongozi wa Habib Bourguiba, na ilipofika mwaka 1957 nchi hiyo ikajipatia uhuru wake huku Bourguiba akiwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Hata hivyo hadi kufikia mwaka 1987 Bourguiba alianza kuiongoza nchi hiyo kwa mabavu na hivyo kupelekea kupinduliwa na Zine El Abidine Ben Ali. Ben Ali ambaye naye pia aliendeleza sera za udikteta na ukandamizaji aling'olewa madarakni kupitia mapinduzi ya wananchi ya mwezi Januari 2011, na kukimbilia Saudi Arabia. Tunisia yenye ukubwa wa kilometa mraba 163,610 iko kaskazini mwa Afrika na inapakana na nchi za Libya, Algeria na Bahari ya Mediterania.
Siku kama ya leo, miaka 218 iliyopita yaani 26 Mei mwaka 1799, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru.
Na siku kama ya leo miaka 137 iliyopita yaani tarehe 26 Mei mwaka 1880 Charles Louis Alphonse Laveran, daktari wa Kifaransa aligundua chanzo cha ugonjwa wa malaria duniani.
Baada ya kupata shahada yake ya uzamifu, Daktari Alphonse Laveran alisafiri Algeria kwa lengo la kuhudumia watu wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya afya na tiba. Akiwa huko alipata fursa ya kuchunguza na kufanya utafiti wa kina kuhusiana na malaria, ugonjwa ambao ulikuwa ukiwaangamiza watu wengi katika pembe tofauti za dunia, ambapo mwaka 1880 alifanikiwa kupata chanzo cha ugonjwa huo. Aligundua kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na mbu waanaoitwa Anopheles ambao huishi katika sehemu za unyevunyevu na zilizo na maji yaliyotuama. Mwaka 1907 Alphonse Laveran alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika uwanja wa tiba na ugunduzi wake wa chanzo cha ugonjwa wa malaria.