Jul 09, 2017 14:05 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya tisa ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia manyanyaso na mateso yanayowakumba watu wa jamii ya Rohingya wakati wanapokuwa katika juhudi za kunusuru nafsi zao kutokana na jinai za serikali ya Myanmar. Tukasema kuwa, aghlabu ya wahanga wa jinai hizo huishia mikononi mwa magenge hatari ya wafanyamagendo ya binaadamu ambapo huwa wanaadhibiwa na kuteswa kama wafungwa na watumwa. Leo tutaendelea kuelezea suala hilo, hivyo endeleeni kuungana nami hadi mwisho wa kipindi.

Ndugu wasikilizaji matamshi ya hivi karibuni ya kamanda wa jeshi la Myanmar kwa mara nyingine yalibainisha kwamba madai ya hapo kabla ya serikali ya nchi hiyo juu ya kuhitimisha mashambulizi katika eneo la Rakhine, yalikuwa mbinu tu za kuzipotosha fikra za walio wengi na asasi za kimataifa kuhusiana na hali mbaya ya Waislamu wa jimbo hilo. Katika matamshi hayo, Min Aung Hlaing  kamanda wa jeshi la Burma akihutubia mkutano huko Naypyidaw, mji mkuu wa Myanmar alitetea mauaji na ukandamizaji wa kijinsia wa askari wa serikali dhidi ya Waislamu wa Rakhine na kusema kuwa, wakazi wa eneo hilo ni Wabangladesh ambao walihajiri nchini Myanmar na hivyo hawahesabiwi kuwa raia wa Burma. Utetezi wa kamanda huyo wa jeshi la Myanmar kuhusu mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya, ulijiri ikiwa ni baada ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa kupitisha uamuzi wa kuanzisha uchunguzi kuhusiana na tuhuma za mauaji ya kimbari, jinai na utesaji unaofanywa na askari wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu.

Utetezi wa afisa huyo wa jeshi la serikali juu ya mashambulizi hayo ni ishara ya wazi ya kuendelea hujuma hizo dhidi ya Waislamu hao. Serikali ya Myanmar inawalazimisha Waislamu wa Rohingya ambao wana asili ya muda mrefu nchini humo, ima kukiri kuwa ni raia wa Bangladesh au wakamatwe na kutiwa mbaroni na kisha kuzuiliwa katika kambi za wakimbizi zenye mazingira mabaya sana. Akthari ya Waislamu wa Rohingya wanafadhilisha kukimbia nchi kutokana na kuuawa kikatili na kwenda nchi za jirani. Hata hivyo kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita, kukimbia kwao huko huwa kunakabiliwa na matatizo mengi sana ikiwa ni pamoja na kuangukia mikononi mwa makundi ya wafanya magendo ya binaadamu, sambamba na kukumbwa na hali mbaya ya kimaisha hata katika nchi wanazozikimbilia.

************************

Kwa muda mrefu sasa jamii ya wachache ya Rohingya imekuwa ikikumbwa na ubaguzi wa hali ya juu. Watu wa jamii hiyo ni jamii ya watu wanyonge zaidi katika jamii ya Burma ambapo hawana haki ya uraia na Hulazimishwa kuwa wakimbizi nchini Bangladesh na kwengineko.

Baadhi ya jinai kubwa zinazofanywa na Mabudha kwa kushirikiana na askari wa serikali

Mwezi Novemba mwaka 2016 akthari ya Waislamu wa kabila la Rogingya walilazimika kuyahama makazi yao na kwenda nchi jirani baada ya watu wasiojulikana kuvamia vituo kadhaa vya polisi na kutekeleza mauaji ambapo baadaye serikali ya Myanmar na bila ya kufanya uchunguzi wowote iliwahusisha Waislamu hao na hujuma hizo. Hadi sasa zaidi ya Waislamu elfu 17 wa Rohingya baada ya kuhama makazi yao huko Myanmar, wanaishi katika kambi za wakimbizi katika mji wa mpakani wa Bangladesh. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Myanmar haiwaruhusu Waislamu hao kurudi nchini kwao wala serikali ya Bangladesh kuwaruhusu kuishi kwa uhuru nchini humo. Hii ni katika hali ambayo akthari ya Waislamu wengine wa kabila hilo la Rohingya wanaishi bila kutambuliwa rasmi kuwa ni wakimbizi huko katika miji ya Jammu na Kashmir maeneo ambayo yako mpakani baina ya Myanmar na India. Takwimu zilizotolewa na serikali za jimbo la Jammu na Kashmir, zilisema kuwa karibu Waislamu wa Rohingya elfu 10, wanaishi katika majimbo hayo.

Aung San Suu Kyi, mshindi wa zawadi ya Nobel ambaye anachuki kubwa dhidi ya Waislamu

Aidha serikali ya India inakadiria kuwa karibu wahajiri elfu 40 wa Rohingya wanaishi nchini India baada ya kukimbia makazi yao nchini Myanmar. Hata kama Waislamu hao wanasimamiwa na Umoja wa Mataifa, lakini bado serikali ya India imekataa kuwatambua rasmi kuwa ni wakimbizi wanaohitajia haki maalumu za ukimbizi. Idara za usalama za nchi hiyo zimekuwa zikiwatisha wahajiri hao wa Rohingya na kuwaambia kuwa eti uepo wao ni tishio kwa usalama wa majimbo ya Jammu na Kashmir, suala ambalo halina ukweli wowote. Kwa hakika jamii ya wachache ya Rohingya inaishi maisha magumu katika mataifa jirani. Katika hatua mpya iliyotokana na kubatilishwa vitambulisho vya akthari ya Waislamu wengi wa kabila hilo eneo la Jammu na Kashmir, Waziri wa Makazi wa jimbo la Jammu aliitisha kikao na viongozi wa ngazi za juu wa idara ya usalama wa mpakani na jaji wa mahakama kuu ya nchini Myanmar kwa ajili ya kujadili njia za utatuzi wa mgogoro wa Waislamu hao.

Mwanamke wa Rohingya akilia kwa uchungu baada ya familia yake yote kuteketezwa na Mabudha

Katika kikao hicho alisema kuwa, India haiwatambui Waislamu wa Rohingya kama wahajiri rasmi na kwa mujibu wa sharia zinazowahusu raia wa kigeni nchini India, kubakia kwa watu hao ndani ya ardhi ya nchi hiyo ni kinyume cha sharia. Kufuatia matamshi hayo, kiongozi huyo wa serikali ya India aliwaamuru Waislamu hao kuondoka nchini humo, amri ambayo bado inaendelea kusisitizwa na serikali ya jimbo la Kashmir hadi sasa. Katika hali hiyo hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya India iliitaka serikali ya Myanmar kutatua matatizo ya jimbo la Rakhine na kuacha kuwakandamiza Waislamu wa eneo hilo ili kuzuia mwenendo wa wakazi wake kuendelea kukimbilia katika mataifa ya jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New Delhi, mji mkuu wa India, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo alisema kuwa, serikali ya taifa hilo imekusudia sambamba na kuwabaini zaidi ya wahajiri elfu 10 wa Rohingya, iweze kuuwaondoa wahajiri hao kutoka katika majimbo ya Jammu na Kashmir. Kufuatia hali hiyo Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) lilikitaja kitendo cha kuwarejesha Waislamu hao kutoka India kwa nguvu kuwa kilicho na hatari kubwa.

 
*******************************
Kuwafanya wakimbizi na kadhalika mauaji ya kimbari ni mambo ambayo wanayokumbana nayo watu wa jamii ya wachache wa Rohingya katika maisha yao ya kila siku nchini Burma. Pamoja na hayo na katika hali ambayo hatua ya kutumwa timu ya kuchunguza iwapo jeshi la Myanmar limetenda jinai za kivita, maangamizi ya kizazi na ubakaji wa kutisha dhidi ya wanawake na mabiti wa Kiislamu wa jamii hiyo, umeongeza mashinikizo ya kimataifa dhidi ya serikali ya Naypyidaw. Hivi sasa viongozi wa serikali ya Burma na kupitia mbinu mpya wanajaribu kupotosha fikra za walio wengi duniani kuhusiana na jinai zao hizo.

Kofi Atta Annan, Katibu Makuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa

Pendekezo la kutaka kurejea nyumbani wakimbizi wa Rohingya wanaoishi nchini Bangladesh, lililotolewa na Kofi Atta Annan, Katibu Makuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa tume ya watu wanane ya kuchunguza tofauti zilizopo baina ya serikali ya Myanmar na wakazi wa jimbo la Rakhine, lilitumiwa vibaya na viongozi wa serikali kwa ajili ya kupotosha fikra za walio wengi duniani juu ya jinai kubwa zibazotekelezwa nchini Burma. Hii ni kwa kuwa viongozi wa Myanmar wanafahamu kwamba, Waislamu hao hawawezi kurejea tena katika hatari ya kuuawa kutokana na khofu waliyo nayo juu ya jinai za kutisha walizozishuhudia kutoka kwa askari na Mabudha wa Myanmar. Aidha viongozi wa serikali ya nchi hiyo walikubaliana na pendekezo hilo kwa kuwa walijua kuwa halina ulazima wowote  wa kutekelezwa.  Hii ni kwa kuwa ukweli wa serikali ya Myanmar kuhusu kurejea wakimbizi hao, ungethibiti kwa pendekezo hilo la Annan kusimamiwa kikamilifu na asasi za kimataifa sambamba na kuwekwa waangalizi wa Umoja wa Mataifa katika jimbo la Rakhine angalau kwa kipindi cha miaka miwili ya mwanzo, suala ambalo hadi sasa bado halijatekelezwa.

Machungu na taabu za Waislamu hao wanaoongoza kwa kudhulumiwa duniani yanaakisiwa mara chache sana na vyombo vya habari vya dunia. Kisa kichungu kinachotokana na machungu kuwahusu Waislamu hao wasio na hatia kinawahusu pia watoto na wanawake, wanaochomewa nyumba zao na kisha kulazimika kuwa wakimbizi kupitia mitumbwi na maboti yasiyo na usalama na hivyo kuishia kuzama maji baharini. Safari za wakimbizi wa Rohingya wanaojaribu kuokoa maisha yao huwa zinakabiliwa na hatari, ambapo wanaofanikiwa kufika nchi kavu wakiwa salama pia huwa wanakabiliwa na matatizo chungu nzima huku wakikosa wa kuwaonea huruma hata katika nchi walizokimbilia.

Mwanamke aliyenusurika kuteketezwa kwa moto na Mabudha makatili

Wakati mwingine Waislamu hao huwa wanafariki dunia kutokana na njaa kali huku watoto na wanawake wao wakiuzwa kama bidhaa ili kuokoa maisha yao. Hali ikiwa ni hiyo, wanaume wa jamii hiyo nao husalia mikononi mwa magenge ya wafanya magendo ya binaadamu na kutumikishwa kama watumwa huku wakiwa hawajui mustakbali wao.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya tisa ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum Warahmatullahi wa Barakaatu…………./


 


 

 

Tags