Jul 23, 2017 14:05 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 10 ya makala yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar.

 

Ndugu wasikilizaji, hata kama masaibu na machungu ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar yamekuwa yakikabiliwa na kimya cha muda mrefu cha jamii ya kimataifa,  hatimaye yameweza kuzivutia hisia za walio wengi duniani kiasi cha kuvifanya hata vyombo vya habari hivi karibuni kuanza kusambaza picha na video za madhila na ukatili wa Mabudha dhidi ya watu wasio na hatia wa kabila la Rohingya. Kama tulivyosema kuwa, mwaka 2012 ndipo kulianza wimbi la mashambulizi yasiyo na huruma dhidi ya watu wa jamii hiyo ambapo kufuatia wimbi hilo, maelfu ya Waislamu wa Rohingya walilazimika kuihama nchi yao na kuelekea nchi za jirani hususan Bangladesh.

Askari wa Myanmar wakiwa wamewazunguka Waislamu kabla ya kuwaua kwa halaiki

Aidha miezi  minane iliyopita wimbi hilo la mauaji ya kutisha liliibuka tena baada ya askari wa serikali ya Burma kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali ya kigaidi kuvamia miji na vijiji vya Waislamu na kuua idadi kubwa ya Waislamu hao sambamba na kufanya jinai nyingine nyingi kukiwemo kuteketeza moto maelfu ya nyumba na makazi yao, kubomoa misikiti na kuwabaka wanawake na mabinti wa jamii hiyo inayodhulumiwa ndani ya taifa hilo. Uchunguzi uliofanywa na tume ya Umoja wa Mataifa umethibitisha wazi kwamba, mashambulizi hayo yalisukumwa na chuki za kidini na ukabila kuwalenga Waislamu hao na ni kwa ajili hiyo ndio maana hata Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch likatangaza wazi kwamba, mashambulizi hayo ya askari na Mabudha wa Myanmar, ni aina ya maangamizi ya kizazi kama ambavyo pia ni jinai dhidi ya binaadamu.

John McKissick, mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)

Aidha John McKissick, mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ametangaza kuwa, serikali ya Myanmar inatekeleza maangamizi ya umati dhidi ya watu wa jamii ya Rohingya wasio na ulinzi.

************************************

Hata kama katika vyombo vya habari kumekuwa kukitangazwa kuwa, Waislamu hao ni wahanga wa ukatili wa kidini wa Mabudha wa Myanmar na kuwafanya kuwa wakimbizi, lakini ukweli ni kwamba vyombo hivyo havijaweza kuandika uhalisia na ukubwa wa jinai na ukatili wote wanaofanyiwa watu wa jamii hiyo na katika hilo huishia tu kuzungumzia juu juu matukio hayo machungu.

Saskia Sassen, mtaalamu wa elimu ya kijamii

Hivi karibuni Saskia Sassen, mtaalamu wa elimu ya kijamii na muhadhiri wa Kimarekani katika Chuo Kikuu cha Colombia na mkazi wa jijini New York Marekani, alifanya utafiti wa kielimu juu ya chanzo cha Waislamu wa Rohingya kuwa wakimbizi. Aliandika matokeo ya uchunguzi wake katika vitabu na makala zake kadhaa, ambapo alibainisha kiini na ukubwa wa jinai za Mabudha kuwalenga watu wa jamii hiyo ya Rohingya. Kwa mujibu wa Saskia Sassen, watu wa jamii ya Rohingya ambao ni jamii ya wachache kuwepo kwa karne kadhaa katika eneo la Rakhine, wamekuwa wakikumbwa na mashambulizi ya kutisha ya askari na viongozi wa Mabudha wenye misimamo mikali nchini humo. Utafiti wa msomi huyo unaonyesha kwamba dini na kabila la Waislamu hao, ndio sababu kuu ya kukumbwa na mashambulizi na ukatili wa kila aina kutoka kwa maafisa hao wa usalama wa serikali na Mabudha. Tangu muongo wa 1990 hadi sasa, jeshi la Burma limepora ardhi na mashamba makubwa ya Waislamu hao bila kuwalipa fidia yoyote ile. Suala hilo limeendelea kwa kipindi chote huku likishika kasi zaidi katika miaka ya hivi karibuni hususan kuanzia mwaka 2012 baada ya kubadilishwa sheria ya umiliki wa ardhi kwa maslahi ya serikali na mashirika makubwa ya nchi hiyo.

****************************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilicho hewani ni makala yanayoangazia ukatili na jinai kubwa za serikali na Mabudha wa Myanmar kuwalenga Waislamu wa kabila la Rohingya hii ikiwa ni sehemu ya 10 ya makala hizo.

Moja ya jinai mbaya za askari na Mabudha wa Myanmar kwa kuwachoma moto Waislamu

Saskia Sassen anaendelea kufafanua kadhia hiyo kwa kusema: ‘Ikiwa tutaangalia upande wa kiuchumi, tutafahamu kwamba, serikali ya Myanmar inawaondoa watu wa kabila la Rohingya kutoka katika ardhi zao za jadi, kwa madai ya kutaka kuinua kiwango cha uchumi wake kupitia sekta ya kilimo. Hii ni kusema kuwa katika hilo serikali ya nchi hiyo imeweza kufikia malengo yake ambapo hivi karibuni tu ilitenga ekari milioni moja, laki mbili na elfu 68, katika maeneo walipokuwa wakiishi Waislamu wa Rohingya kwa ajili ya sekta ya kilimo, kupitia mashirika makubwa maalumu. Hii ni katika hali ambayo kiwango cha ardhi kilichotengwa kwa ajili ya kazi hiyo mwaka 2012 kilikuwa ni ekari elfu saba pekee, hii ikiwa na maana kwamba katika kipindi cha miaka minne iliyopita, kiwango hicho kimeongezeka mara 160 zaidi.’ Pamoja na hayo, wakati kunapotangazwa habari za jinai na ukatili wanaofanyiwa Waislamu wa Rohingya kutoka kwa serikali na Mabudha wa Burma, hakuwekwi wazi uhalisia wa mambo wa kile kinachojiri hususan suala zima la kuporwa mamilioni ya mashamba ya Waislamu hao. Ni kwa ajili hiyo ndio maana ikasemekana kuwa, licha ya vyombo vya habari hivi karibuni kuanza kutangaza habari za machungu ya Waislamu hao, lakini bado havijaweza kuakisi uhalisi wa jinai na kile kinachojiri nchini Burma.

Viongozi wa serikali wakijaribu kuwahadaa walimwengu kupitia vikao na baadhi ya makabila

Ukweli ni kwamba, ikiwa tutaendelea kuchunguza ukubwa wa taathira hasi kwa jamii ya wanavijiji wa Myanmar kutokana na ukatili na ukandamizaji wa serikali dhidi yao, tutapata kufahamu masuala mawili. Moja ni kwamba, mpango wa timuatimua wa miaka ya hivi karibuni wa serikali ya Naypyidaw dhidi ya wanavijiji, umegeuka na kuwa mradi kabambe ambao umekuwa ukitekelezwa na Mabudha katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni Nchini Myanmar. Serikali ya nchi hiyo inaamini kuwa ni kupitia mwenendo huo ndipo itaweza kutekeleza miradi mikubwa kama vile biashara ya mbao, kilimo na uvunaji maji kutoka ardhi hizo za Waislamu. Pamoja na hayo, vyombo vya habari vinaishia tu kuakisi ukatili na jinai za kidini na kikabila. Hata Bi Aung San Suu Kyi, mshindi wa  zawadi ya amani ya Nobel na ambaye mwaka 2015 chama chake kilishinda uchaguzi, kinyume na ilivyotarajiwa naye amenyamanzia kimya jinai na unyanyasaji unaofanywa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Chuki ya mwanamama huyo dhidi ya Waislamu wa Rohingya imekuwa kubwa kiasi cha kuitaka jamii ya kimataifa kutotaja jina la Rohingya kwa madai kwamba, jina hilo linaweza kukwamisha mwenendo wa maridhiano ya kitaifa nchini Myanmar.

Mabudha wakatili wanaohusika na jinai

Aidha hivi karibuni Waziri huyo wa Mambo ya Nje na Kiongozi wa mrengo wa demokrasia nchini Burma (Aung San Suu Kyi) katika mahojiano aliyofanyiwa na Shirika la Habari la BBC alikadhibisha aina yoyote ya jinai na mauaji kuwalenga Waislamu wa nchi hiyo. Kadhalika Bi Suu Kyi akizungumzia maangamizi ya kizazi na mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu hao alisema: “Mimi ni mwanasiasa tu. Kiujumla mimi sishabihiani na mtu kama vile Bi Margaret Hilda Thatcher. Lakini kwa upande mwingine sifanani pia na Mama Teresa.” Mwisho wa kunukuu.

************************************************

Hata hivyo suala linalofaa kuashiriwa ni kwamba, katika mahojiano hayo, Aung San Suu Kyi alitoa madai akisema: “Ninadhani ukatili unaofanyika Rakhine unaripotiwa visivyo. Watu wanaowaua Waislamu wanadhaniwa kwamba wanashirikiana na viongozi wa ngazi ya juu wa taifa.” Mwisho wa kunukuu. Kupitia matamshi hayo Bi Aung San Suu Kyi alikusudia kusema kwamba, watu wanaotekeleza jinai na uvunjwaji wa haki za binaadamu dhidi ya Waislamu, hawana mahusiano yoyote na serikali. Hii ni katika hali ambayo Umoja wa Mataifa na mashirika mbalimbali yamekiri kwamba, vitendo hivyo vinavyowalenga Waislamu wa Rohingya, vimetekelezwa na maafisa usalama wa serikali kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali ya kigaidi.

Askari wa serikali wakielekea vijiji vya Waislamu kufanya jinai

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mashambulizi yaliyoibuka yapata miezi tisa iliyopita mkoani Rakhine, mbali na kusababisha mauaji ya maelfu ya watu, yalisababisha pia kwa akali watu elfu 70 ambao ni Waislamu kulazimika kuwa wakimbizi nje ya nchi yao kutokana na wasi wasi mwingi waliokuwa nao wa kuuawa kwa halaiki na maafisa usalama wa serikali. Pamoja na hayo, Suu Kyi mbali na kukanusha kuwepo mauaji ya kimbari mkoani Rakhine anadai kuwa hata wanaotekeleza vitendo hivyo vya ukatili hawahusiani na serikali na kwamba hata ripoti za ukandamizaji huo zinaripotiwa visivyo. Licha ya radiamali mbalimbali kutoka kwa baadhi ya asasi, mashirika na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu kulaani hujuma hizo, lakini bado serikali ya Burma inaendelea na mwenendo wake wa unyang’anyi wa ardhi za Waislamu wa Rohingya bila kuwa na wasi wasi wowote.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 10 ya makala haya yanayozungumzia jinai na ukatili wa kutisha unaofanywa na Mabudha wenye kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

Tags