Jul 29, 2017 02:20 UTC
  • Jumamosi, Julai 29, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 5 Mfunguo Pili, Dhulqaadah 1438 Hijria mwafaka na tarehe 29 Julai mwaka 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 774 iliyopita, aliaga dunia Radhi ud-Deen Ali ibn Musa mashuhuri kwa jina la Sayyid Ibn Tawus, fakihi, mpokezi wa hadithi, mwanahistoria na mwanafasihi wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Hillah nchini Iraq. Awali Ibn Taus alisoma kwa baba yake na kwa babu yake na kisha baadaye akahudhuria masomo ya wanazuoni mashuhuri katika zama hizo mjini Hillah. Sayyid Ibn Tawus mbali na kulikana kuwa kama msomi na alimu mkubwa, aliondokea pia kuwa mashuhuri kwa sifa ya uchaji Mungu na kuipa mgongo dunia. Aidha alimu huyo ameandika vitabu kuhusiana na maudhui mbalimbali. Moja ya vitabu vyake mashuhuri ni kile kinachojulikana kwa jina la Lohoof  kinachozungumzia tukio la Ashura. ***

Sayyid Ibn Tawus

Katika siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, alizaliwa Benito Mussolini mwanasiasa, dikteta na mwasisi wa chama cha Kifashisti nchini Italia. Ufashisti ni utawala wa kidikteta uliojikita katika kuleta aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani na kupotosha itikadi na fikra za wananchi. Mwaka 1922 Mussolini alinyakua wadhifa wa uwaziri mkuu wa Italia, na hivyo udikteta kuendelea kutawala nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler na kuandaa mazingira ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. ***

Benito Mussolini

Miaka 76 iliyopita, vikosi vya Japan iliyokuwa muitifaki wa Ujerumani wakati wa kujiri Vita Vikuu vya Pili vya Dunia viliwasili katika maeneo ya pwani ya kusini ya India na China kwa ajili ya kuyakalia kwa mabavu maeneo hayo. Kabla ya hapo Japan ilikuwa imelidhibiti na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi za mashariki na kusini mwa China. Katika kipindi cha miaka ya 1941 hadi 1942, Japan ilifanikiwa kuzikalia kwa mabavu ardhi za Thailand, Malaysia, Singapore, Ufilipino, Indonesia na Myanmar ambazo kabla zilikuwa chini ya himaya ya Uingereza, Ufaransa na Uholanzi. ***

Japan na Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, uliasisiwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Lengo la kuasisiwa kwa wakala huo lilikuwa kusimamia shughuli za vituo vya nyuklia kwa lengo la kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia na uzalishaji wa silaha za maangamizi ya umati. Ofisi ya wakala huo iko mjini Vienna, Austria na maabara moja ya utafiti ipo katika mji huo, ambapo hutoa natija ya uchunguzi mbalimbali kuhusiana na matumizi ya nishati ya nyuklia kwa nchi wanachama. Hata hivyo kutokana na kwamba wakala huo umeathiriwa na madola makubwa, umekengeuka malengo yake na kufuata mielekeo ya kisiasa.***

Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA)

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia mwanafikra wa Kijerumani Herbert Marcuse. Marcuse alizaliwa mwaka 1898 na baada ya Wanazi kutwaa madaraka ya nchi hiyo, yeye alielekea Marekani. Herbert Marcuse alikuwa akijitambua kuwa mfuasi wa fikra za Umaxi, ingawa alikuwa akikosolewa na Wamaxi. Reason and Revolution na An Essay on Liberation ni baadhi tu ya vitabu mashuhuri vya Herbert Marcuse. ***

Herbert Marcuse

Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo, Abul Hassan Bani Sadr, Rais aliyeuzuliwa wa Iran aliikimbia nchi akiwa pamoja na kiongozi wa kundi la Munafiqin la MKO, Massoud Rajavi. Siku 37 kabla yake Bani Sadr alikuwa ameuzuliwa cheo cha Urais kutokana na kukosa ustahiki, kuzusha machafuko nchini na kushindwa kulinda nchi mbele ya hujuma za utawala wa dikteta Saddam Hussein. Bani Sadr alikuwa na matumaini kwamba, mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na kundi la MKO yangeweza kumrejesha tena madarakani. Hata hivyo kuchaguliwa Muhammad Rajai kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu kulimvunja moyo Bani Sadr ambaye aliamua kukimbilia Ufaransa akiwa amevaa nguo za kike.***

 

Bani Sadr na Massoud Rajavi