Aug 04, 2017 02:27 UTC
  • Ijumaa tarehe 4 Agosti, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 11 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1438 Hijria, inayosadifiana na tarehe 4 Agosti mwaka 2017.

Siku kama ya leo miaka 1290 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake, Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijiria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati na zama zake. Historia inasema kuwa Imam Ridha kama walivyokuwa mababa na mababu zake watukufu (as) alianisika mno na Qur’ani na hakuacha kusoma kitabu hicho popote pale alipokuwa. Redio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa mnasaba huu.

Siku kama ya leo miaka 1102 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Dhul Qaad 336 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na faqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na akapata elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na lielimu za Sheikh Mufid ilikuwa kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh.

Sheikh Mufid

Miaka 225 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania.

Percy Bysshe Shelley

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye bahari ya China ya Kusini. Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini.

Bendera ya Vietnam

 

Tags