Ijumaa 11 Agosti, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Dhulqaada 1438 Hijria, sawa na 11 Agosti 2017.
Tarehe 11 Oktoba miaka 488 iliyopita Martin Luther alitangaza rasmi madhehebu ya Protestant. Uprotestanti ulianzishwa na Martin Luther kama harakati ya kidini katika karne ya 16 kwenye ulimwengu wa Kikristo kwa lengo la kufanya mageuzi ya kidini. Harakati hiyo ilianza dhidi ya kanisa Katoliki na udikteta wa viongozi wa madhehebu hiyo kuhusu suala la msamaha wa dhambi unaotolewa makasisi na Papa. Martin Luther aliyekuwa Mjerumani alianza harakati hiyo ya uasi ndani ya kanisa Katoliki baada ya kufasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani tofauti kabisa na amri ya Papa kwa lengo la kuvunjilia mbali taasubu za kimadhehebu za Kikatoliki.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa. Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wacha-Mungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado kijana mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq. Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita Haile Selassie, mfalme wa Ethiopia alitia saini azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuiunganisha Eritrea na Ethiopia. Ardhi ya Waislamu ya Eritrea ambayo hapo kabla ilikuwa ikikoloniwa na Italia, katika Vita vya Pili vya Dunia ilikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Mwezi Desemba 1950 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Eritrea kuongozwa kwa mfumo wa shirikisho sambamba na kuunganishwa na Ethiopia. Hata hivyo kutokana na kwamba wananchi wengi wa Eritrea hawakuridhishwa na hatua hiyo pamoja na kupuuzwa haki zao na utawala wa Ethiopia, walizidisha upinzani wao dhidi ya utawala wa Addis Ababa na hatimaye kuanzisha harakati ya kupigania uhuru wa nchi yao mnamo mwaka 1960. Mwaka 1993 mapambano ya wananchi wa Eritrea yalizaa matunda ambapo walishiriki katika kura ya maoni na kupiga kura ya kujitenga na Ethiopia.
Na siku kama ya leo miaka 57 iliyopita nchi ya Chad ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakoloni wa Ufaransa waliishambulia Chad na katika kipindi cha miaka mitatu wakaidhiiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mwaka 1958 Ufaransa uliipa Chad hiari ya kujiongoza na miaka miwili baadaye na katika siku kama ya leo nchi hiyo ikapata uhuru kamili na kuchagua mfumo wa uongozi wa jamhuri. Nchi ya Chad inapakana na nchi za Libya, Cameroon, Sudan, Afrika ya Kati, Nigeria na Niger.