Sep 06, 2017 03:35 UTC
  • Jumatano tarehe 6 Septemba, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 15 Dhilhija 1438 Hijria sawa na 6 Septemba 2017.

Siku kama ya leo miaka 1224 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Ali Naqi (AS) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW, katika mji mtakatifu wa Madina. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad AS, Imam Hadi alichukua jukumu zito la Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha utawala wa ukoo wa Bani Abbas, na Mutawakkil ndiye aliyekuwa ameshika hatamu za uongozi wakati huo. Baada ya mtawala huyo kuhisi kuwa Imam Hadi (as) na wafuasi wake walikuwa hatari kwa utawala wake, aliamrisha Imam atolewe Madina na kuhamishiwa Samarra, Iraq ili amuweke chini ya uangalizi. Licha ya hayo yote, lakini Imam Naqi aliendelea kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 251 iliyopita, alizaliwa John Dalton, msomi na mtaalamu wa fizikia wa Kingereza katika familia ya watu wa kijijini. Kutokana na Dalton kupendelea sana elimu na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, alifanikiwa kwenda shuleni na kujifunza mambo mbalimbali. Ni wakati huo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na utafiti katika masuala mbalimbali ya kielimu. Dalton alibuni na kuvumbua mambo mengi katika uwanja wa fizikia, kemia na sayansi asilia baada ya utafiti mkubwa. Msomi huyo hakuchoka na badala yake aliendeleza utafiti mkubwa katika uga atomu. John Dalton alifariki dunia mwaka 1944.

John Dalton

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo. Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Vita hivyo vilidumu kwa takribani wiki tatu. Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkent mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani. Japokuwa azimio la Tashkent lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kukaribishwa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.

Vita vya pili vya Kashmir

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, baada ya kupamba moto harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah, kulifanyika maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini. Kwa sababu hiyo utawala wa Shah uliokuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na harakati hizo za mapinduzi, uliamua kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile. Wakati huo huo huo Imam Ruhullah Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni huko Najaf nchini Iraq alitoa taarifa akiwataka wananchi wa Iran kudumisha harakati za mapambano. Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa wananchi, Imam Khomeini aliyataja maandamano yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo ya Kiislamu kuwa ni ibada.

Maandamano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya Shah

Na siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Swaziland ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama ya leo husherekewa nchini humo kwa anwani ya siku ya taifa. Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Swaziland kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Ulaya. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru. Swaziland ina ukubwa wa kilomita mraba 17364 na kijiografia iko kusini mwa bara la Afrika ikiwa inapakana na nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

Nchi ya Swaziland

 

Tags