Sep 08, 2017 02:45 UTC
  • Ijumaa, Septemba 8, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 17 Mfunguo Tatu Dhulhaji, 1438 Hijria, sawa na tarehe 8 Septemba, 2017 Milaadia.

Tarehe 8 Septemba ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ujinga. Kujua kusoma na kuandika ni miongoni mwa vielelezo vya ustawi katika jamii ya mwanadamu na ujinga husababisha umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mkakati wa kupambana na kutojua kusoma na kuandika haukuwa wa kuridhisha katika baadhi ya nchi na hadi sasa idadi kubwa ya watu hawajapata neema hiyo.

Nchini Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kulifanyika jitihada kubwa za kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa kadiri kwamba Disemba mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuasisiwa Harakati ya Kupambana na Ujinga. Taasisi hiyo imepiga hatua kubwa hapa nchini.  

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu bila ya kuzingatia hali hiyo, wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao.

Harakati ya tarehe 17 Shahrivar

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita kulitiwa mkataba wa ulinzi wa mataifa ya Asia ya kusini mashariki (SEATO) katika mji mkuu wa Uphilipino, Manila. Mkataba huo ulitiwa saini na nchi za Marekani, Uingereza, Australia, Pakistan, Tailandi, Ufaransa, New Zealand na Uphilipino. Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi mwanachama inapokabiliwa na mashambulio ya kijeshi, shambulio la uasi na kukabiliwa na vitisho kutoka nchi isiyomwanachama, basi nchi wanachama zinapaswa kuisaidia nchi hiyo kijeshi au kwa kutumia wenzo wa vikwazo.

Miaka 76 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi waliuzingira mji wa Leningrad, Saint Petersburg ya sasa. Hata hivyo mji huo haukutekwa na jeshi la Kinazi licha ya matarajio ya Adolf Hitler na makamanda wake. Wakazi wa Leningrad waliendeleza mapambano ya ukombozi hadi Januari mwaka 1944 wakati walipofanikiwa kujiondoa katika mzingiro wa wanajeshi wa Ujerumani.

Kushindwa mzingiro wa Leningrad

Na siku kama ya leo miaka 254 iliyopita, baada ya mapigano ya muda mrefu na kwa mujibu wa makubaliano ya Paris, Canada iliondoka chini ya udhibiti wa Ufaransa na kudhibitiwa rasmi na Uingereza. Hata hivyo mivutano baina ya Wacanada wenye asili ya Ufaransa na Waingereza waliokuwa wakiishi Canada iliendelea kwa muda mrefu. Licha ya Canada kujitangazia uhuru na mamlaka ya kujitawala mwaka 1867 lakini nchi hiyo inafuata Uingereza katika mfumo wake wa kisiasa.

Canada