Oct 09, 2017 09:25 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Okt 9

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, ndani na nje ya nchi....

Soka: Iran yaizaba Togo 2-0

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeinyuka Togo mabao 2-0 katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki, ambao umetumiwa na vijana wa Team Melli kama wanavyojulikana hapa nchini, kupasha misulu moto kwa ajili ya Kombe la Dunia mwakani. Katika mechi hiyo iliyopigwa Alkhamisi jioni katika Uwanja wa Azadi, magharibi mwa Tehran, vijana wa Iran waliutandaza mpira na kuwaacha hoi mahasimu wao The Sparrow Hawks kutoka Togo. Licha ya mchezo huo kuwa wa kasi na majaribio ya hapa na pale ya magoli bila mafanikio, lakini timu hizo zilienda mapumzikoni kabla ya kuona nyavu za mwenzake.  Katika kipindi cha pili, labda baada ya mkufunzi wao kuwadokeza kunako mapungufu, Iran ilipata bao la kwanza kupitia mshambuliaji wake mahiri, Karim Ansarifard katika dakika ya 51, bao lililowanyanyua mashabiki kwa hoi na vifijo kutoka kwenye viti vyao. Hata kabla ya mate kukauka, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 wa Iran na ambaye anakipiga katika klabu ya Olympiacos ya Ugiriki alifanikiwa kucheka na nyavu tena na kufanya mambo kuwa 2-0. Timu hiyo ya mpira wa miguu ya Iran inatazamiwa kuvaana na Russia mjini Kazan katika mchuano mwingine wa kupasha misuli moto kuelekea Kombe la Dunia mwaka ujao 2018.

Soka: Iran yaibamiza Guinea 3-1 Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya mabarobaro wa Iran imeibamiza Guinea mabao 3-1 katika mchuano wa ufunguzi wa Kombe la Dunia kwa vijana wenye chini ya miaka 17. Katika mchuano huo uliopigwa Jumamosi katika Uwanja wa Fatorda, mjini Margao nchini India, mabaromabaro hao wa Iran waliwapeleka mbio vijana wa timu hiyo ya Afrika Magharibi katika kampeni yao ya kwanza ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo, yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA.

Wachezaji wa Iran wakishangilia bao

Bao la kwanza la Iran lilifungwa na Allahyar Sayyad kabla ya Mohammad Sharifi kufanya mambo kuwa 2-0 kupitia mkwaju wa penati. Saied Karimi aliipa Iran bao la tatu katika dakika za lala salama. Bao la kufutia machozi la Guinea lilifungwa na Fandje Toure.

Timu hiyo ya Iran ambayo ipo katika Kundi C, inatazamiwa kupepetana na Ujerumani katika mechi yake ya pili hatua ya makundi siku ya Jumanne. Niger ambayo ni mara ya kwanza kushiriki mashindano hayo imeanza vyema, baada ya kuilambisha sakafu Korea Kusini, kwa kuifunga bao 1 moja la uchungu kwa mtungi.

Soka: Mechi za Kirafiki

Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars imechabangwa bao 1-0 na Thailand katika mchuano wa kimataifa ya kirafiki. Bao la Teerasil Dangda wa timu mwenyeji lilitosha kuikata ngebe Harambee Stars katika mechi hiyo ya Jumapili uwanjani SGC mjini Bangkok. Kenya ilitazamiwa ing'are katika mchuano huo licha ya kuwa ugenini kwa kutilia maanani kuwa, Thailand ipo nafasi ya 50 nyuma ya Harambee Stars katika orodha ya mwisho ya FIFA. Thailand imevuna ushindi huo dhidi ya Kenya siku tatu baada ya kuicharaza Myanmar mabao 3-1 katika mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa.

Huku hayo yakiarifiwa, Jumamosi ya Oktoba 7 timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars ilicheza mchezo wa kimataifa ya kirafiki pia dhidi ya ya Malawi katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam na kuambulia sare ya 1-1. Mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Malawi unakuwa ni mchuano wa 13 chini ya mkufunzi Salum Mayanga, wakiwa wamefungwa mchezo mmoja pekee dhidi ya Zambia katika michuano ya Baraza la Vyama vya Soka kanda ya Afrika Kusini (COSAFA) na wametoka sare mechi sita na kushinda sita. Mchezaji Ngambi Robert ndio aliifungia Malawi goli la uongozi dakika ya 35 lakini Simon Msuva akaisawazishia Taifa Stars kunako dakika 57. Hata hivyo baadhi wa mashabiki wanaipongeza Taifa Stars kwa kuwa walilazimika kumaliza mechi wakiwa wachezaji tisa uwanjani kutokana wachezaji 2 Erasto Nyoni na Mzamiru Yassin kupigwa kadi nyekundu.

 

Mbio za Kombe la Dunia 2018

Bao la pekee la kiungo wa Gunners Alex Iwobi liliipaisha Nigeria ilipochuana na Zambia na ushindi huo hafifu wa bao 1-0 ukaifanya Super Eagle kuwa timu ya kwanza barani Afrika kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mwaka ujao 2018 nchini Russia. Ushindi huo umeiwezesha Nigeria kujikusanyia jumla ya pointi 13 kwenye Kundi B. Mchezaji Shuhu Abdullahi alimpa Iwobi pasi safi na kijana huyo ambaye ananolewa na Arsene Wenger adhihirisha umahiri wake kwa kujaza bao wavuni katika dakika ya 73.

Huku hayo yakiarifiwa, Mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2018 kati ya Uganda na Ghana iliyomalizika kwa sare ya 0-0 Jumamosi katika uwanja wa Nelson Mandela mjini Nambole, huenda ikarudiwa ikiwa Shirikisho la Soka la Ghana (GFA) litafanikiwa kulishawishi Shirikisho la Soka duniani (FIFA) kuwa Black Stars ilinyimwa bao halali.  Refa Daniel Bennett kutoka Afrika Kusini na wasaidizi wake Eldrick Adelaide na Steve Marie kutoka Ushelisheli wanamulikwa kutokana na uamuzi wao wa kutatanisha wa kunyima Ghana bao. Ripoti nchini Ghana zinadai kuwa GFA imeandikia FIFA barua rasmi kuitisha mechi hiyo irudiwe. Itakumbukwa kuwa, mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2018 kati ya Afrika Kusini na Senegal itarudiwa Novemba 10. Afrika Kusini ilikuwa imeshinda Senegal mabao 2-1 Novemba 12 mwaka jana 2016 mjini Polokwane, lakini refa akapatikana na hatia ya kupendelea Afrika Kusini katika maamuzi yake. Aliipa Afrika Kusini penalti ya utata iliyoiwezesha kushinda 2-1. The Cranes ya Uganda itamenyana na Madagascar Jumatano katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki kabla ya kutoana udhia na Ghana katika mchuano muhimu wa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia. Hayo yakirifiwa, Misri imevuna ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Kongo DR na hivyo kuweka tiketi mfukoni ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Mshambuliaji mahiri wa Liverpool Mohamed Salah alionekana kuwa nyota wa Misri katika mchuano huo.

Kombe la Dunia 2018 nchini Russia

Mafarao wa Misri ambao wanaizidi Uganda kwa pointi nne, watakabiliana na Ghana katika mechi yao ya mwisho Novemba 6. Kwengineko, mabingwa wa Kombe la Dunia 2010, Uhispania imefuzu kwa mara 11 mfululizo kwa fainali za mwakani Russia. Hispania imepata tiketi hiyo baada ya kuifunga Albania mabao 3-0. Wakati huo huo, Afrika Kusini imeweka katika mazingira mazuri katika kampeni yake ya kufuzu katika Kombe la Dunia baada ya kuifunga Burkina Faso 3-1 mjini Johannesburg. Mbali na hayo, bao la kusawazisha mambo la kiungo Omar al-Somah limewapa matumaini vijana wa Syria kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018 kwa waliposhuka dimbani kuvaana na Australia.Timu nyingine za hivi punde kutinga Kombe la Dunia nchini Russia mwaka ujao 2018 ni Uholanzi baada ya kuitandika Belarus mabao 3-1 wakati ambapo Uingereza ilikuwa inajipatia tiketi kwa kuichachafya Slovenia bao 1-0.

Imarati yaitaka Qatar isiandae Kombe la Dunia 2022

Afisa wa ngazi za juu wa usalama katika Umoja wa Falme za Kiarabu amesema mgogoro uliopo kati ya Doha na nchi kadhaa za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia utapatiwa ufumbuzi iwapo Qatar itaachana na azma yake ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022.

Qatar, mwenyeji wa Kombe la Dunia 2022

Dhahi Khalfan, Mkuu wa Usalama mjini Dubai ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Iwapo Kombe la Dunia 2022 halitaandaliwa na Qatar, mgogoro wa Qatar utaisha. Hadi tunaenda mitamboni, serikali ya Qatar ilikuwa haijatoa maelezo kuhusu pendekezo hilo la afisa wa ngazi za juu wa Imarati. Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe Tano Juni mwaka huu zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi hiyo. 

Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar mzingiro wa kiuchumi na kuipa masharti chungu nzima. Qatar inakadhibisha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Saudia.

……………………………… TAMATI………………….