Oct 16, 2017 08:08 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu katika dakika hizi chache za kukupasha matukio mawili matatu yaliyotikisa uga wa michezo duniani, ndani ya siku saba zilizopita. Usibanduke kando ya radio yako hadi tamati ya kipindi, karibu……...

Soka U17: Iran yaibamiza Costa Rica 3-0

Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya mabarobaro wa Iran imeibamiza Costa Rica mabao 3-0 katika mchuano wa Kombe la Dunia kwa vijana wenye chini ya miaka 17. Katika ngoma hiyo ya Ijumaa uwanjani Jawaharlal Nehru mjini Goa, vijana wa Iran walionyesha mchezo mzuri na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira takriban muda wote. Bao la kwanza la Iran lilitiwa kimyani na Mohammad Ghobeishavi kunako dakika ya 25, huku kiungo Taha Shariati akifanya mambo kuwa mawioi kwa mtungi dakika nne baadaye. Mchezaji mahiri wa Iran Mohammad Sardari alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la vijana wa Costa Rica. Machipukiza hao wa Kiirani wamefunga jumla mabao 10 kufikia sasa; ambapo waliicharaza Guinea mabao 3-1 huku Ujerumani ikikokotezwa mabao 4-0. Team Melli ya Iran inatazamiwa kutoana udhia na Margao Oktoba 17.

Upigaji makasia: Timu ya wanawake ya Iran yaibuka ya 3

Timu ya taifa ya wanawake ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya mchezo wa kupiga makasia imeibuka katika nafasi ya tatu ya mashindano ya olimpiki yanayofahamika kwa Kimombo kama Asian Youth Olympic Games Qualification Regatta & Asian Rowing Junior Championships huko Sinigapore. Siku ya Jumamosi, akina dada hao wa Kiirani Asra Javanmardi, Kimia Zare’ei, Forough Aghabalazadeh na Fatemeh Safari, waliibuka katika nafasi ya tatu na kutunukiwa medali ya shaba. Kwa upande wa timu ya watu wawili ya mchezo huo kwa wanaume, vijana wa Iran Reza Ghahremani na Milad Allahverdian waliibuka kidedea na kutwaa medali ya dhahabu, wakifuatiwa na Japan na India.

Timu ya Iran ya wanawake

Mwanadada wa Iran Haniyeh Bidad aliibuka wa tatu na kuondoka na medali ya shaba katika kitengo cha mtu mmoja. Siku hiyo hiyo ya Jumamosi, vijana wa Iran Reza Ghahremani, Shirzad Ghaderi, Karou Hosseini na Milad Allahverdian, waliibuka katika nafasi ya tatu na kutunukiwa medali ya shaba. Uzbekistan iliibuka kidedea ikifuatiwa na China. Mashindano hayo ya kupiga makasia yaliyowawaleta pamoja wanamichezo kutoka nchi za bara Asia kama Iran, China, Japan, Thailand, Singapore na Uzbekistan yalianza Oktoba 11 na kumalizika Oktoba 14.

Voliboli: Kenya na Cameroon kuiwakilisha Afrika Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya Kenya ya mchezo wa voliboli kwa upande wa wanawake almaarufu Malkia Strikers pamoja na Cameroon zimefuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia la mchezo huo nchini Japan mwaka ujao 2018. Mashindano hayo huandaliwa na Shirikisho la Voliboli Duniani (FIVB). Malkia Strikers imejipatia tiketi hiyo licha ya kugaragazwa na mwenyeji Cameroon katika mchuano wa fainali ya Mabingwa Afrika mjini Yaounde. Kenya ilizabwa seti 3-0 za (25-22, 25-19, 29-27). Awali mabinti hao wa Kenya waliwasagasaga Waarabu wa Misri kwa seti 3-0 katika nusu fainali ya kipute hicho iliyoandaliwa Ijumaa jijini Yaounde, nchini Cameroon.  Warembo hao wanaotiwa makali na kocha Japheth Munala waliwaonyesha wenzao kivumbi licha ya kukabili ushindani wa kufa kwenye mchezo huo.

Voliboli

Vipusa wa Kenya chini ya nahodha, Mercy Moim walitumia mbinu zote kuhimili mtanange huo na kufaulu kuzoa ushindi wa alama 25-23, 25-23, 25-21.  Malkia Strikers walifuzu kwa nusu fainali baada ya kuibuka kidedea waliposhinda mechi zote nne Kundi 'B' na kutia kapuni alama 12. Misri ilifuzu kushiriki nusu fainali baada ya kumaliza ya pili Kundi 'A' kwa kunasa alama sita. Wenyeji Cameroon walitwaa tiketi ya kushiriki fainali kwa kuangusha Senegal kwa seti 3-0. Wenyeji walikuwa wameibuka kileleni mwa mechi za Kundi 'A' kwa alama tisa. Misri imewahi kutwaa ubingwa wa Afrika mara tatu sawa na Tunisia iliyolemewa kufana katika mashindano hayo baada ya kumaliza ya tatu kwenye dhoruba ya Kundi 'B' kwa kutia kapuni alama sita.

Ligi ya EPL

Kikosi cha Pep Guardiola kimeendeleza msururu wa ushindi baada ya kushusha kipigo kikali kwa kila timu wanayokutana nayo kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza. Man City ilitonesha kidonda cha Stoke City baada ya kuikandamiza mabao 7- 2 kwenye mechi ya ligi ya EPL Jumamosi katika Uwanja wa Etihad. Mabao ya City yalifungwa na Gabriel Jesus (2), Sterling, David Silva, Fernandinho, Sane na Bernardo Silva.

Timu hiyo imefikisha pointi 22 na kujiweka kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza, huku mahasimu wao wa jadi Man U wakifikisha pointi 2O wakiwa katika nafasi ya pili na wakifuatiwa na Tottenham katika nafasi ya tatu. Ushindi wa Jumamosi wa Watford dhidi ya Arsenal, umemuweka pabaya Kocha Arsene Wenger baada ya kushindwa kupanda kwenye nafasi nne bora za juu. Gunners walizabwa mabao 2-1.

Arsenal wakishangilia bao

Arsenal inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 13 nyuma ya Chelsea iliyopo nafasi ya tano yenye hizo hizo lakini wakiwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Matokeo hayo yamemchafulia Wenger ambaye huwa anakumbana na upinzani wa mashabiki wa timu hiyo mara anapofungwa na kuwakumbusha vidonda vilivyoanza kupoa. Wakati huo huo, Crystal Palace wamefanikiwa kupata alama tatu kwa mara ya kwanza na kufunga goli lao la kwanza kwenye msimu huu, baada ya kuibuka na ushindi dhidi Chelsea. Palace walichukua uongozi baada ya dakika ya 11 kufuatia krosi ya Andros Townsend kumkuta Yohan Cabaye ambaye aliupiga mpira na kumngonga Cesar Azpilicueta kabla ya kuingia kwenye wavu, na kusababisha furaha kutoka kwa timu hiyo ya nyumbani. Chelsea walisawazisha goli hilo ndani ya dakika saba, kona ya Cesc Fabregas kutoka upande wa kulia ambayo ilishindwa kuokolewa vyema na Watford na kuruhusu Tiemoue Bakayoko ambaye hakuwa amekabwa kufunga goli lake kwa la kwanza la Ligi Kuu. Sare ya Liverpool na Man United inaifanya Liverpool kuwa nafasi ya 7 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza kwa kufikisha point 13.

…………………………TAMATI……………………..