Oct 23, 2017 08:09 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 23

Hujambo mpenzi msikilizaji wa RT na karibu tutupie jicho matukio kadhaa muhimu yaliyotawala uga wa spoti kitaifa na kimataifa, ndani ya siku saba zilizopita. Usibanduke kando ya radio yako hadi tamati ya kipindi...

Soka U17: Iran yazabwa na Uhispania robo fainali

Timu ya taifa soka ya vijana wa Iran imekubali kichapo cha mabao 3-1, iliposhuka dimbani kuvaana na Uhispania katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia kwa vijana wenye chini ya umri wa miaka 17. Mchuano huo wa aina yake ulipigwa mjini Kochi nchini India Jumapili. Mabao ya timu hiyo ya Ulaya yalifungwa na Abel Ruiz na Ferran Torres, huku Saeid Karimi akiipa Iran bao la kufutia machozi.

Iran ilitinga robo fainali baada ya kuibamiza Mexico mabao 2-1 katika hatua ya makundi wiki jana, siku chache baada ya kuichachafya Costa Rica mabao 3-0. Kabla ya hapo, mabarobaro hao wa Kiirani waliicharaza Guinea mabao 3-1 huku Ujerumani ikikokotezwa mabao 4-0.

Mieleka: Wairani watwaa mataji Uturuki, Bulgaria

Wanamieleka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameendelea kutamalaki mashindano ya kimataifa ya mieleka na kuudhihirishi uliwengu kuwa wao ni moto wa kuotea mbali. Nchini Uturuki, timu ya wanamieleka wa Iran mtindo wa Sumo waliibuka kidedea katika Michezo ya Mabingwa wa Dunia 2017, baada ya kuzoa medali kochokocho. Milad Rahimi Aliabadi aliipa Iran medali ya dhahabu baada ya kuonyesha mchezo wa kufana katika fainali ya wanamieleka wenye kilo 100, huku Mostafa Mahmoudi akiibuka wa pili na kutuzwa medali ya fedha katika kategoria ya kilo 85. Wanamieleka nyota wa Iran wa safu ya wenye uzani mwepesi Alireza Tanha, Majid Rezaei Omran na Moslem Faramarzi walituzwa kila mmoja dhahabu. Iran ilitia kibindoni medali za fedha na shaba katika kitengo cha kilo 75 kupitia wamanimieleka Shoja’ Maghsoudi naAbolfazl Cheravi. Mashindano hayo ya kimataifa yanayofahamika kwa Kimombo kama World Elite Games 2017 yamfanyika katika pwani ya Kemer, yapata kilomita 40 magharibi mwa mji wa Antalya, kuanzia Oktoba 19 na kufunga pazia lake Oktoba 22.

Wanamieleka wa Iran waliozoa medali chungu nzima Uturuki

Kwengineko, timu ya wanamieleka waliobobea ya mtondo wa Freestyle ya Iran imetwaa taji Mabingwa wa Dunia 2017 nchini Bulgaria. Hii ni baada ya kuzoa medali 14 za dhahabu, fedha nne na shaba nne, huku ikijikusanyia jumla ya pointi 299.

Marekani imeibuka ya pili kwa alama 156 huku Russia ikifunga orodha ya tatu bora kwa alama 150. Mashindano hayo yanayofahamika kama Veteran World Championships yalianza Oktoba 10 na kumalizika siku baadaye, katika mji wa Plovdiv nchini Bulgaria.

Mazembe yatinga fainali CAF

Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetinga fainali ya Kombe la Shirikisho CAF, baada ya kumlazimisha mwenyeji wake FUS Rabat sare tasa katika mechi ya nusu fainali ya marudiano iliyopigwa Morocco Jumamosi usiku. Matokeo hayo katika Stade de FUS mjini Rabat yaliipatia Mazembe ushindi wa jumla ya 1-0 na wametinga fainali na kujipa fursa kutetea ubingwa wao. Mechi ya kwanza, timu hizi mbili zilitoka sare ya bao 1-1. Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, itachezwa mwishoni mwa mwezi huu huku ile ya mwisho ikipigwa mapema mwezi Novemba.

Riadha: Mkenya avunja rekodi Uhispania

Mwanariadha mahiri wa Kenya Joyciline Jepkosgei amedhihirisha yeye ni malkia wa mbio za kilomita 21 baada ya kuvunja rekodi yake ya dunia akitwaa ubingwa wa Valencia Half Marathon nchini Uhispania, Jumapili. Akiwekewa kasi na mfalme wa zamani wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Ezekiel Kemboi, Jepkosgei alifuta rekodi ya dunia ya saa 1:04:52 aliyoweka aliposhinda Prague Half Marathon katika Jamhuri ya Czech kwa kukamilisha Valencia Half Marathon kwa saa 1:04:51. Mwanariadha huyo wa Kenya alikamilisha kilomita 10 kwa dakika 30:09 kabla ya kasi yake kupungua kilomita tano zilizofuata akimaliza kilomita 15 za kwanza kwa dakika 45:59.

Mwanariadha aliyevunja rekodi wa Kenya, Joyciline Jepkosgei

Alipovunja rekodi mwezi Aprili mwaka huu 2017, alikamilisha kilomita 15 kwa kutumia dakika 45:37. Kuvunja rekodi yake mwenyewe ni ndoto aliyokuwa nayo tangu Aprili mwaka huu.

Viongozi wa kisiasa na Wakenya wa mataba yote wamezika tofauti zao za kisiasa na kuungana kumpongeza mwanariadha huyo nyota aliyeiweka Kenya kwenye ramani ya dunia.

Ligi ya Premier

Na tunafunga kipindi kwa kutupia jicho matokeo ya michuano kadhaa muhimu iliyopigwa katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Mchuano wa Jumapili kati ya Arsenal na Everton umeendelea kuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa soka hususan kwenye mitandao ya kijamii, haswa kwa kutilia maanani kuwa, ushindi mnene wa Gunners umezidisha mashinikizo ya kumtaka kocha wa Everton, Ronald Koeman ajiuzulu. Ni mchuano ulioshuhudia mbwembwe za aina yake haswa baada ya Idrissa Gueye kupigwa nyekundu na Everton kusalia na wachezaji 10 uwanjani. Everton iligeuzwa kichwa cha mwendawazimu na Wabeba Bunduki na kutandikwa mabao 5-2 katika uga wa Goodison Park. Mabao ya Arsenali yalifungwa na viungo Nacho Monreal, Mesut Ozil, Alexandre Lacazette, Aaron Ramsey na Alexis Sanchez.

Wachezaji wa Arsenali wakishangilia bao

Mwanasoka nyota wa kimataifa Wayne Rooney aliwafungia Everton bao lao la kwanza huku Oumar Niasse akifunga la pili.

Mbali na hayo, Michy Batshuayi aliyefanikiwa kucheka na nyavu mara mbili aliiwezesha Chelsea iliyokuwa imeshapokea kipigo cha mabao 2-1 kupindua matokeo na kupata ushindi wa aina yake wa mabao 4-2 nyumbani Stamford Bridge walipochuana na Watford.

Kwengineko, Manchester United wamepoteza mechi yao ya kwanza msimu huu baada ya kukubali kipigo cha mabao mawili kwa moja dhidi ya Huddersfield. Huddersfield ndiyo walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia kiungo Aaron Mooy, akimalizia mpira uliotemwa na De Gea kufuatia shuti kali la Tom Ince kunako dakika ya 28, huku Laurent Depoitre akipiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Man U,  kufuatia uzembe wa mabeki wa Mashetani Wekundu.

Marcus Rashford ambaye alitokea benchi ndiye aliyefunga goli la kufuta machozi la Man U katika dakika ya 78 akimalizia krosi safi ya Lukaku.

Katika matokeo mengine, West Ham ilipokea kichapo cha mbwa cha mabao 3-0 kutoka Brighton wakati ambapo New Castle na Southampton walikuwa wanaicharaza Crystal Palace na West Brom bao 1-0 kwa usanjari huo. Leicester iliitandika Swansea mabao 2-1 namna ambavyo Bornemouth iliizaba Stoke.

Kwa matokeo hayo, Manchester City iliyowanyoa bila maji Burnley mabao 3-0 wanasalia kileleni mwa jedwali la EPL ikiwa na alama 25 ikifuatiwa na mtani wake wa jadi, Man U yenye alama 20 licha ya kula kichapo kutoka Huddersfield, alama sawa na Tottenham yenye kufunga orodha ya tatu bora, baada ya kuigaragaza Liverpool mabao 4-1. The Blues na Gunners kwa sasa zitasalia kubabana sako kwa bako katika nafasi ya nne na tano kwa usanjari huo, zote zikiwa na alama 16.

..........................................TAMATI.............................

 

Tags