Alkhamisi 26 Oktoba, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Safar 1439 Hijria sawa na Oktoba 26, 2017.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita sawa na tarehe Nne mwezi Aban mwaka 1343 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 26 Oktoba mwaka 1964, Imam Khomeini (MA) ambaye ndio kwanza alikuwa ameachiwa huru kutoka jela ya utawala wa Shah, alitoa hotuba akilalamikia vikali hatua ya utawala huo ya kupasisha sheria ya capitulation au sheria ya kuwapatia kinga ya kutofikishwa mahakamani raia wa Marekani waliofanya uhalifu nchini Iran. Katika hotuba hiyo Imam Khomein alizilaani pia Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hotuba ya Imam dhidi ya sheria hiyo ya capitulation na utawala wa Shah iliwaamsha wananchi na hivyo kuuchukiza utawala wa Shah, ambao ulianzisha njama mpya dhidi ya Imam Khomeini, na siku zilizofuata Imam akatiwa tena mbaroni na kubaidishwa.
Katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Mfalme Hussein wa Jordan na Yitzhak Rabin, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel walitiliana saini mkataba uliojulikana kama makubaliano ya amani. Mkataba huo ulikuwa ni jitihada za Marekani za kuleta mapatano baina ya Waarabu na Wazayuni. Mwenendo wa mapatano na maridhiano hayo ulianza 1991 katika kongamano lililofanyika mjini Madrid Uhispania. Kwa mujibu wa mkataba huo, utawala wa Tel Aviv ulikubali kurejea nyuma kutoka katika baadhi ya ardhi za Jordan.
Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walimuua shahidi Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina Dakta Fathi Shiqaqi akiwa huko Malta. Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana. Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kuwekwa jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Ni kufuatia harakati zake hizo za kimapambano, ndipo Dakta Shiqaqi akachaguliwa kuwa katibu mkuu wa harakati hiyo ya Jiharul-Islami na kuendeleza mapambano yake dhidi ya Wazayuni maghasibu. Aidha Shiqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina.