Nov 20, 2017 02:46 UTC
  • Jumatatu, Novemba 20, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Mfunguo 6 Rabiul Awwal 1439 Hijria, sawa na tarehe 20 Novemba, 2017 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita, Mtume Muhammad (saw) alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka. Hijra ya Mtume (saw) na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba vilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1374 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa huko Iraq walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati ya mapambano dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala huyo katili na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi.

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kirusi Leo Tolstoy. Mwandishi huyo alizaliwa mwaka 1828 na aliondokewa na baba na mama yake akiwa bado mdogo. Alifanya safari za kitalii na uchunguzi katika jamii nyingi za Ulaya na mambo aliyoyashuhudia katika safari hizo yalimfanya achukie ustaarabu wa kimaada wa nchi za Magharibi. Tolstoy alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwapa elimu na malezi watoto wadogo na alikuwa akijitahidi mno kusaidia matabaka ya watu maskini na wasiojiweza.Leo Tolstoy ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Kiyama", "Kipindi cha Utotoni" na riwaya ya "Vita na Amani".

Leo Tolstoy

Tarehe 20 Novemba miaka 97 iliyopita mapambano makubwa ya wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni wa Kiingereza yalishindwa. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kusambaratika utawala wa Kiothmania, serikali za Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi za utawala huo katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo Uingereza ilichukua Iraq na kukabiliwa na mapambano makali ya wananchi tangu hapo mwanzoni. Mapambano hayo yaliongozwa na wanazuoni wa Kiislamu waliotoa wito wa kufukuzwa wakoloni wa Kiingereza na kuundwa serikali huru itakayozingatia sheria za Kiislamu.

Askari wa Uingereza wakiingia Baghdad mwaka 1917

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza, aliuawa shahidi. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar nchini Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Muingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Sheikh Izzuddin Qassam

Na siku kama ya leo miaka 67 iliyopita majeshi ya Marekani na China yalipambana uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabisa katika vita vya Korea. Mapigano hayo yalitokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini.Vita vya Korea vilisababisha hasara kubwa mno kwa pande zote mbili. Vita hivyo vilisimama kutokana na upatanishaji wa Umoja wa Mataifa na hadi sasa Korea Kaskazini na Kusini zimebakia nchi mbili zilizojitenga.

 

Tags