Nov 24, 2017 02:38 UTC
  • Ijumaa, Novemba 24, 2017

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na Novemba 24, 2017 Milaadia

Siku kama ya leo miaka 186 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara. Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.

Michael Faraday

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazerti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran. 

Gazeti la Majlis

Na siku kama ya leo miaka 4 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi 6 zinazounda kundi la 5+1 zilitia saini makubaliano ya muda ya nyuklia mjini Geneva huko Uswisi. Kutiwa saini makubaliano hayo kulitayarisha uwanja mzuri na kufungua njia ya mazungumzo zaidi kati ya Iran na nchi hizo sita ambazo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani kwa ajili ya kutia saini makubaliano kamili ya nyuklia na kuondoa hitilafu kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini, na mwishowe kufutwa vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

 

Tags