Dec 09, 2017 02:31 UTC
  • Jumamosi, 9 Disemba, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria ambayo inalingana na tarehe 9 Disemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 989 iliyopita yaani tareher 20 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 450 Hijria, alifariki dunia Abu Tayyib Tabari, faqihi na mwandishi wa Kiislamu huko Baghdad. Abu Tayyib alizaliwa mwaka 348 Hijria huko Amol, moja kati ya miji ya kaskazini mwa Iran. Tabari alifanya safari katika nchi mbalimbali kwa lengo la kutafuta elimu. Abu Tayyib Tabari, aliishi na kufundisha huko Baghdad ambapo alikuwa miongoni mwa maulamaa wakubwa za zama zake. Faqihi Tabari alikuwa hodari katika taaluma ya fasihi na utunzi wa mashairi. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Jawab fi Sima'a" na "al Ghinaa wa Al Ta'aliqatil Kubra fil Furu'u".***

Abu Tayyib Tabari

Miaka 275 iliyopita katika sikuu kama ya leo, Carl Wilhelm Scheele mwanakemia mashuhuri wa Sweden na mmoja kati ya waasisi wa elimu ya kemia ya leo alizaliwa huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo. Mwanakemia huyo aliendelea na masomo yake kutokana na jitihada na hamu yake kubwa aliyokuwanayo licha ya familia yake kuwa duni. Carl Wilhelm ambae aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemikali, mwezi Oktoba mwaka 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya chlorine baada ya juhudi za miaka mitano. Gesi hiyo ni moja kati ya mada muhimu za kemikali na inatumika sana viwandani. Mbali na hayo mwanakemia huyo aligundua pia manganese na Glicerine.***

Carl Wilhelm Scheele

 Katika siku kama ya leo miaka 259 iliyopita, vita vya Madras vilianza na kudumu kwa miezi 13. Vita hivyo vinahesabiwa kuwa mojawapo ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa huko India. Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza. Ufaransa ilipigana ikiwa na wanajeshi elfu tatu dhidi ya Uingereza iliyokuwa na wapiganaji elfu 22. Mwezi Januari mwaka 1761, Ufaransa ilisalimu amri mbele ya Uingereza baada ya kikosi cha dhiba kushindwa kufika vitani. ***

Kuanza vita vya Madras baina ya Uingereza na Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, vikosi vya Uingereza viliwashinda wanajeshi wa utawala wa Othmania huko Palestina wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia na kisha vikaikalia kwa mabavu ardhi hiyo. Hadi kufikia Oktoba mwaka uliofuata, vikosi vya Uingereza vilikuwa vimefanikiwa kudhibiti ardhi nyingi za Mashariki ya Kati . Mwezi huo kulitiwa saini makubaliano ya kluacha vita na baadaye kukatiwa saini mkataba wa amani baina ya pande mbili. Kudhibitiwa Palestina na vikosi vya Uingereza kulihesabiwa kuwa na umuhimu kutokana na kuwa ilikuwa ni kupigwa hatua nyingine moja mbele kwa ajili ya kufikiwa vipengee vya Tangazo la Balfour (Balfour Declaration), Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza alililokuwa amelitoa mwezi mmoja kabla. Balfour aliahidi katika tangazo hilo juu ya kuanzishwa dola la Kiyahudi na Wazayuni huko Palestina na udhibiti wa Uingereza kwa ardhi hiyo ya Palestina, uliwaandalia mazingira Wazayuni ya kufikia lengo hilo. ***

Kuvamiwa Palestina na majeshi ya Uingereza

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 9 Disemba mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijikomboa na kupata uhuru. Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipojipatia uhuru wake wa kujitawala katika tarehe kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika. Mwaka 1964 Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ***

Image Caption

 

Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, yalianza mapambano yasiyo na kikomo ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. Mapambano hayo ya ukombozi ambayo ni mashuhuri kwa jina la "Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa baada ya kushadidi mauaji na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala huo ghasibu. Hayo yalijiri baada ya wananchi Waislamu wa Palestina kukatishwa tamaa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na nchi za Kiarabu na taasisi nyingi za Palestina kwa ajili ya kurejeshewa haki zao. ***

Intifadha ya Kwanza

Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti na kuutangaza utawala wa Baath wa Iraq kuwa ndio ulioanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Katika siku hiyo, Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika ripoti yake kuwa Iraq iliivamia Iran tarehe 22 Septemba mwaka 1980. Miji na vijiji vingi vya mpakani mwa Iran vilitekwa na kukaliwa kwa mabavu huku wanawake, watoto na wanaume wengi wakiwa wahanga wa vita hivyo vikubwa katika uvamizi huo ambao uliungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Magharibi. ***

Utawala wa Baath wa Iraq ulianzisha vita vya kichokkozi dhidi ya Iran

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali. ***

Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani

 

 

Tags