Sura ya As-Sabaa, aya ya 1-5 (Darsa ya 761)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 1-5 (Darsa ya 761)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 33 ya Ahzab, katika darsa hii ya 761 tutaanza kuizungumzia sura ya 34 ya Sabaa. Sura hii imeteremshwa Makka; na kwa sababu ya kuzungumziwa ndani yake habari za watu wa kaumu ya Sabaa imepewa jina hilo la Sabaa. Tunaianza tarjumi na maelezo ya sura yetu hii kwa aya yake ya kwanza na ya pili ambazo zinasema:
الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَلَهُ الْحَمْدُ فِي الْآخِرَةِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye ni vyake (vyote) vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na sifa ni zake Yeye katika Akhera. Naye ni Mwenye hikima, Mwenye khabari.
يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۚ وَهُوَ الرَّحِيمُ الْغَفُورُ
Anayajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda huko. Na Yeye ni Mwenye kurehemu, Mwingi wa maghufira.
Kwa kawaida, sisi sote tunapoona picha za michoro ya kupendeza ya mandhari za maumbile za milima, misitu, bahari na anuai za wanyama huwa tunatekwa na kuvutiwa na michoro hiyo na kujikuta tunamsifu na kumpongeza msanifu wa athari hizo za sanaa. Lakini hebu na tujiulize, je yule Muumbaji halisi wa mbingu na ardhi na mandhari zote hizo nzuri na za kuvutia za maumbile ambazo picha zake tu sisi zimetuvutia na kutufanya tumsifu mchoraji wake, si mwenye kulaiki na kustahiki zaidi kuhimidiwa na kusifiwa? Ndani ya Qur'ani tukufu kuna sura tano zinazoanza kwa kumsifu na kumhimidi Mwenyezi Mungu SW. Sura fupi zaidi kati ya hizo tano ni Suratul-Fatihah tunayoisoma katika Sala. Suratus-Sabaa ni sura nyengine kati ya sura hizo tano ambayo imeanza kwa kumhimidi Allah SW kwa kuumba ulimwengu huu wa kuvutia na wenye adhama. Yeye Mola ni Muumba wa ulimwengu wote wa maumbile na vilevile ni Mjuzi wa kila kilichomo ndani yake na kila kinachohusiana na kitu kimoja kimoja. Hakuna chochote kifichikacho katika elimu yake; na anauendesha ulimwengu kwa elimu na hekima yake. Huko akhera pia watu wa peponi watamhimidi na kumsifu Allah kwa sababu ataamiliana na waja wake kwa uadilifu na kwa fadhila zake; na atawapa waja wake waliotenda mema malipo makubwa kabisa. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wa kusifiwa, kushukuriwa na kuhimidiwa kiuhakika na kiuhalisia ni Allah SW; na kila kinaposifiwa chochote chenye sifa za ukamilifu huwa kwa hakika anasifiwa na kuhimidiwa Muumba wa hicho kinachosifiwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa elimu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ulimwengu na mwanadamu si ya ujuzi na utambuzi wa kijumla tu. Hakika Yeye Mola ni mjuzi na mwenye elimu ya kina ya vitu vyote vilivyoko katika ulimwengu na mjuzi wa kila kubwa na dogo kabisa lifanywalo na viumbe wa ulimwengu huu.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tatu ambayo inasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَأْتِينَا السَّاعَةُ ۖ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتَأْتِيَنَّكُمْ عَالِمِ الْغَيْبِ ۖ لَا يَعْزُبُ عَنْهُ مِثْقَالُ ذَرَّةٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ وَلَا أَصْغَرُ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرُ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ
Na walisema walio kufuru: Haitatufikia Saa (ya Kiyama). Sema: Ndio! Naapa kwa haki ya Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya ghaibu, hapana shaka itakufikieni! Hapana kinacho fichikana kwake hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko hivyo, wala kikubwa zaidi; ila (vyote hivyo) vimo katika Kitabu chake chenye kubainisha.
Watu wanaokana kuwepo kwa Mwenyezi Mungu Mola Muumba na Mlezi wa viumbe na ambao hawako tayari kukubali kuwepo kwa mwanzishaji mwenye tadbiri na mwendeshaji wa ulimwengu ni wazi kwamba hawatokubali pia kuwepo kwa Kiyama na hawatoamini kuwepo kwa maisha ya baada ya kufa na kuhudhurishwa viumbe kwenye mahakama ya Siku ya Kiyama. Lakini Bwana Mtume SAW anatangaza na kueleza kinagaubaga kuwa: Hii ni dhana, takwa na matamanio ya makafiri kwamba kisiwepo Kiyama baada ya kufa ili wao waweze kufanya lolote wapendalo hapa duniani bila ya mipaka wala vizuizi vyovyote. Lakini kwa mujibu wa wahyi utokao kwa Allah ambao Nabii Muhammad SAW alikuwa akiupokea moja kwa moja, wanadamu wote waumini na makafiri watahudhurishwa katika mahakama ya Siku ya Kiyama na watapaswa kuwajibika na kujieleza kwa yote waliyoyafanya hapa duniani. Mahakama hiyo itashughulikia kwa uadilifu madaftari ya amali za watu kulingana na ushahidi wa maandishi uliosajiliwa kwenye madaftari hayo na malaika wa Allah hapa duniani; na hakuna hata moja, liwe kubwa au dogo ambalo watakuwa wameacha kuliorodhesha kwenye daftari hilo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wakanushaji wa Maadi, yaani kufufuliwa viumbe hawana hoja madhubuti ya kukanushia jambo hilo; wanafanya hivyo kwa dhana tu na kwa kutegemea elimu yenye mpaka maalumu waliyonayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mwanadamu anaamiliana na Mungu ambaye ni mjuzi kamili na mwenye elimu mutlaki ya yote yafanywayo na kiumbe huyo kwa siri na kwa dhahiri, kwa kujionyesha na kujificha; na hakuna chochote kinachoweza kufichika katika elimu yake Mola. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba katika mfumo wa kimaada wingi wa kitu una taathira kubwa sana, lakini katika ulimwengu wa akhera ubora ndio wenye nafasi ya kwanza pamoja na nia aliyofanyia mtu amali yake.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya nne na ya tano ambazo zinasema:
لِّيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ
Ili awalipe walio amini na wakatenda mema. Hao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مِّن رِّجْزٍ أَلِيمٌ
Na wale walio hangaika kuzipinga Ishara zetu wakaona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.
Aya hizi zinaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kuhusu Mahakama ya Siku ya Kiyama kwa kuashiria hatima za watu zitakavyokuwa na kueleza kwamba: Watu Siku ya Kiyama watakuwa makundi mawili. Kundi moja ni la watu wa peponi ambao kutokana na amali njema na za kheri walizofanya duniani watastahiki kupata riziki njema za Mola huko akhera. Na kundi jengine ni la watu wa motoni ambao hapa duniani walikuwa na hima kubwa ya kukadhibisha na kuzikufuru aya za Qur'ani tukufu na mafundisho yake. Watu hao walikuwa wakidhani kuwa wataweza kumshinda Mola na kutoka nje ya mamlaka yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, imani sahihi na amali njema ndiyo njia pekee ya kupatia malipo mema ya Allah Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa anayeweza kumpa mwanadamu malipo kamili na halisi ya amali zake ni Yule mwenye elimu na ujuzi kamili wa matendo na amali zake zote pamoja na nia aliyofanyia matendo na amali zake hizo. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba tusije tukaghafilika na njama za maadui za kuidhoofisha Qur'ani na dini tukufu ya Uislamu ambao nia yao ni kuwaweka watu mbali na Kitabu hicho kitukufu cha mbinguni. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 761 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani, na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya Moto. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/