Aya na Hadithi (8)
Assalaam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya nane ya kipindi hiki ambapo kwa leo tutazungumzia suala la tiba ya Qur'ani dhidi ya magonjwa sugu ya mwili, karibuni.
Katika kipindi kilichopita tulipata kufahamu kwamba katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani kuna ponyo la magonywa yote yawe ni ya kimaanawi au ya kimaada, kutokana na Aya za kitabu hicho cha mbinguni kutoshurutisha ponyo hilo na jambo jingine lolote. Kuna Hadithi nyingi mno ambazo zinawasihi Waislamu kutafuta ponyo la Qur'ani katika kutibu maradhi ya kimaanawi kama vile kufuru na unafiki na magonywa mengine ya kimaadili kama wifu, kiburi, majivuno, ubakhili na mengineyo mengi. Mbali na hayo, kuna Hadithi nyingi pia ambazo zinazungumzia sifa za tiba ya magonjwa tofauti ya kimaada ambayo yamewashinda madaktari wa kawaida kuyatibu. Sifa hizo za tiba zinajumuisha usomaji wa Aya maalumu za Qur'ani Tukufu kulingana na ugonjwa uliomsibu mtu. Mifano ya Hadithi hizo imenukuliwa katika vitabu vingi vya kuaminika kutoka madhehebu zote za Kiislamu. Pamoja na hayo, je, kuna masharti gani yanayopasa kuzingatiwa ili kunufaika na tiba hiyo ya Qur'ani kwa ajili ya kutibu magonjwa ya kimaada na kimaanawi au kwa ibara nyingine kiroho?

Ndugu wasikilizaji, hebu kwanza tusikilize kwa makini kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya ya 82 ya Surat al-Israa inayosema: Na tunateremsha katika Qur'ani ambayo ni ponyo na rehema kwa waumini. Wala hayawazidishii madhalimu ila hasara.
Tunaona hapa kwamba imani ni kiungo na sharti muhimu katika kunufaika na ponyo la Qur'ani Tukufu. Hivyo dhalimu ambaye anamshirikisha Mwenyezi Mungu, kuzichezea shere Aya Zake au kuidhulumu Qur'ani kwa njia yoyote ile huwa hazidishiwi ila hasara na hivyo kutonufaika kwa njia yoyote na Aya hizo. Ama muumini hunufaika na tiba hiyo ya Qur'ani na kujitosheleza kikamilifu na kitabu hicho kitakatifu katika kutibu maradhi yake tofauti ya kiroho na kimaada. Kuhusu suala hilo Mtume Mtukufu (saw) anasema kama ilivyopokelewa katika vitabu tofauti vya kutegemewa kutoka madhehebu zote mbili za Kiislamu, vikiwemo vya Bihar al-Anwar na Kanz al-Umaal: 'Qur'ani ni utajiri usiokuwa na mbadala na wala hakuna umasikini unaobaki baada yake.'
Na Wasii wake al-Imam Ali al-Murtadha (as) anasema kama ilivyokuja katika hotuba yake ya 176 ya Nahjul Balagha: 'Na tambueni kwamba hakuna yeyote atakayekuwa na mahitajio kinyume na Qur'ani, wala yeyote hatajitosheleza pasi na Qur'ani.' Basi jitibuni kwayo maradhi yenu, na jisaidieni kwayo kwa shida zenu - yaani matatizo na masaibu yanayokupateni maishani – kwa sababu ndani yake muna tiba ya ugonjwa mkubwa nao ni kufuru, unafiki, maasi na upotovu.'
**********
Ndugu wasikilizaji, na Hadithi Tukufu zinatwambia kuwa sharti muhimu la kupata ponyo na tiba ya Qur'ani Tukufu ni kuwa na ikhlasi katika kutafuta ponyo hilo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia kitabu chake na kuamini jambo hilo kwa dhati.
Al-Hafidh az-Ziyaat (MA) anasema hivi katika kitabu chake cha Tibb al-Aimat Aleihim as-Salaam: 'Aba Abdillahil Imam as-Swadiq (as) amesema: Hakuna muumini yeyote anayelalamikia maradhi na kutamka mameno yafuatayo kwa ikhlasi hali ya kuwa amegusa kwa mkono wake sehemu anayoumwa: Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara, ila huponywa maradhi hayo na thibitisho la jambo hilo linapatikana kwenye Aya hiyohiyo ambapo Mwenye Mungu anasema: Yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini.'

Ama sharti la tatu la ponyo na tiba ya Qur'ani Tukufu ni kupata tiba hiyo kutoka kwa Ahlul Beit wa Mtume (as) kwa kuwa wao ndio milango ya elimu ya Mtume (sw), na wajuzi wa siri za Qur'ani Tukufu. Wao ni Kizito cha pili tulichoachiwa na Mtume (saw) ambapo kushikamana nao hakutimii ila kwa kufuata na kuwatii kikamilifu kama inavyobainisha wazi suala hilo Hadithi mashuhuri ya Thaqalain. Kitabu cha Tibb al-Aimat pia kinazungumzia jibu lililotolewa na Imam Swadiq (as) kuhusiana na swali aliloulizwa kuhusiana na hirizi ambapo alisema: 'Hakuna tatizo kama hirizi itakuwa inatoka kwenye Qur'ani kwa sababu mtu asiyetibiwa na Qur'ani hapati tiba kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Je, kuna kitu kingine kilicho bora katika vitu hivi kuliko Qur'ani? Je, si Mwenyezi Mungu anasema: Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini? Na je, si Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Lau tungeliiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeliuona ukinyenyekea, ukipasuka kwa hofu ya Mwenyezi Mungu? Tuulizeni ili tupate kukuelimisheni na kukujuzeni kimbizo (tiba) la Qur'ani (Aya zinazosomwa wakati wa kuhofu jini na wanadamu kama vile Aya ya Kursiy) kwa ajili ya kila gonjwa.'
Na Imam (as) anasema katika Hadithi nyingine iliyopokelewa na Muhammad bin Mas'oud al-Ayyashi katika Tafsiri yake: 'Hakika ponyo linapatikana katika elimu ya Qur'ani tu kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: Na tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Ni ponyo na rehema kwa wastahiki, na halina shaka wala wasi wasi ndani yake (kwa wajuzi wa Qur'ani). Na wastahiki (na wajuzi) hao ni Maimamu Waongofu ambao Mwenyezi Mungu anasema kuhusiana nao: Kisha tumewarithisha Kitabu wale ambao tumewateuwa miongoni mwa waja wetu.

Kwa msingi huo, masharti matatu ya kunufaika na ponyo la Qur'ani Tukufu katika kutibu magonjwa yote yawe ni ya kimaanawi au ya kimaada ni imani na itikadi ya kiroho kuhusiana na ponyo la Qur'ani, ikhlasi juu ya mwenyezi Mungu katika kutafuta ponyo kutoka kwake na la tatu ni kupata ponyo hilo kutoka kwa watu wanaoelewa na kuwa na utambuzi wa kutosha kuhusu siri za Qur'ani Tukufu na ambao ndio warithi wastahiki wa kitabu hicho cha mbinguni, ambao si wengine bali ni Mtume Muhammad na kizazi chake kitakatifu (as).
Na kwa natija hii ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kutoka kwetu hatuna la ziada isipokuwa kukutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia huku tukikutakieni kila la heri maishani, kwaherini.