Jun 30, 2018 08:15 UTC
  • Aya ya Hadithi (26)

Assalaam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza kipindi kingine katika mfululizo huu wa vipindi vya Aya na Hadithi ambapo leo tutanufaika na sehemu ya 26 ya mfululizo huu.

Katika kipindi cha leo tutajadili kwa ufupi Aya nne ambazo zinazungumzia suala la zuhdi (zuhudi) na kumwogopa Mwenyezi Mungu. Aya hizi ni za 21 hadi 24 za Surat al-Hadid ambazo tunazitegea sikio kwa makini ilitupate kunufaika na mafudisho yake. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya hizo: Kimbilieni maghufira ya Mola wenu, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyowekewa waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu. Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna akajifakhirisha. Ambao wanafanya ubakhili, na wanaamrisha watu wafanye ubakhili. Na anayegeuka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.

Ngugu katika imani, Aya ya kwanza inatufungulia mlango wa zuhudi (kuipa nyongo dunia) katika maisha yetu ya humu duniani na kujitenga nayo na kuelekea kwenye dunia ya mafanikio na kufuzu kukubwa, nayo ni mashindano kuelekea maghufira ya Mwenyezi Mungu, Pepo na fadhila zake ambazo amewaahidi waumini. Aya ya pili inaashiria kwamba maisha ya dunia yamejaa masaibu na mitihani ambayo ni ya dharura katika kuwalea wanadamu. Hivyo Basi katika maisha haya mwanadamu anatakiwa kufanya zuhudi kwa sababu dunia ni sehemu ya kupitia tu na wala sio ya kuishi milele. Aya ya tatu inabainisha natija na matokeo ya kufanya zuhudi humu duniani na kujitenga na mapambo yake. Matokeo hayo ni kwamba mja hapasi kuhuzunika kutokana na mambo yaliyompita wala kufuruahia na kujigamba na neema alizopewa kwa sababu neema hizo zina mwisho na wala si za kufuzu kukuu na fadhila za kudumu milele. Nayo Aya ya nne inaashiria alama ya zuhudi ya kweli humu duniani nayo ni kutofanya ubakhili duniani na pia kuwa na imani na ukarimu wa Mweye kujitosha (mkwasi), Msifiwa.

Surat al Hadid

 

Wapenzi wasikilizaji, baada ya kupitia kwa ufupi maana ya Aya hizi tukufu, ambazo zinatuongoza kujua maana halisi ya zuhudi, funguo na maana zake, tunachambua Hadithi kadhaa ambazo zinatufafanulia zaidi suala hili. Tunaanza kwa kauli ya Amir al-Mu'mineen Ali (as) ambaye anasema katika moja ya semi zake za hekima (usemi wa 433) kitabu cha Nahjul Balagha:  'Zuhudi (kujinyima starehe za dunia/kuipa nyongo dunia) kupo katika maneneo mawili ya Qur'ani. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Na asiyehuzunika na kilichompotea (kilichompita) wala kutofurahia kinachokuja baadaye, huwa amechukua zuhudi (zuhdi) kwa pande zake zote mbili.'

Imam (as) anabainisha maana hii hii katika Hadithi nyingine ambayo tunaisoma katika kitabu cha Raudhatul Waaidheen ambapo anasema: 'Zuhudi ni utajiri, ucha-Mungu ni ngao na zuhudi iliyo bora zaidi ni kuficha zuhudi. Zuhudi hubana matarajio na wala hakuna zuhudi iliyo bora kama kufanya zuhudi (kujizuia) kwenye haramu. Zuhudi (kujinyima starehe za dunia/kuipa nyongo dunia) kupo katika maneneo mawili ya Qur'ani. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Na asiyehuzunika na kilichompotea (kilichompita) wala kutofurahia kinachokuja baadaye, huwa amechukua zuhudi (zuhdi) kwa pande zake zote mbili. Enyi watu! Zuhudi ni kupunguza matarajio, kushukuru neema na kuepuka yaliyoharamishwa.'

Imepokelewa katika kitabu cha Mishkaatul Anwar, kauli ya Maulana al-Imam Swadiq (as) akisema: 'Zuhudi duniani sio kuacha mali wala kuepuka halali bali zuhudi duniani ni kutokuwa na yakini zaidi na kile kilichoko mkononi kwako kuliko kile kilichoko mkononi mwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.'

Na haya ndiyo madhumuni ya Aya ya nne kati ya Aya tulizosoma. Imam Swadiq pia amenukuliwa katika kitabu cha Bihar al-Anwar, baada ya kuulizwa mipaka ya zuhudi humu duniani naye akasema: 'Mwenyezi Mungu ameainisha mipaka hiyo kwenye kitabu chake aliposema: Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Hakika mtu anayemjua zaidi Mwenyezi Mungu ni yule anayemwogopa zaidi, anayemwogopa zaidi ni yule anayemjua zaidi na anayemjua zaidi ni yule aliye na zuhudi zaidi duniani.'

 

Ndugu wasikilizaji, Imam Sajjad (as) anatuelekeza kwenye mfungamano madhubuti uliopo kati ya zuhudi duniani na ikhlasi juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na taathira yake katika kumfikisha muumini katika daraja za juu za takwa, yakini na ridhaa. Imepokelewa katika kitabu cha ad-Da'waat kwamba: 'Imam Zeinul Abideen (as) aliulizwa kuhusu zuhudi naye akajibu kwa kusema: 'Zuhdi ina daraja kumi na daraja ya juu zaidi ya zuhdi ni daraja ya chini zaidi ya takwa (kuogopa/kumcha Mwenyezi Mungu), na daraja ya juu zaidi ya takwa ni daraja ya chini zaidi ya yakini, na daraja ya juu zaidi ya yakini ni daraja ya chini zaidi ya ridhaa. Tambueni ya kwamba zuhdi yote ipo kwenye Aya ya Mwenyezi Mungu Mtukufu inayosema: Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Mtu yule akasema: La Ilaha Ila Allah, naye Ali bin al-Hussein (as) akasema: Na mimi ninasema: La Ilaha Ila Allah Walhamdulillah Rabbil Aalaminee. (Mmoja wenu anaposema La Ilah Ila Allah, basi na aseme pia, Walhamdulillah Rabbil Aalamineen kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Basi muabuduni Yeye mkimsafishia Dini Yeye. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.)

Na katika Hadithi nyingine ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam huyohuyo Sayyid as-Sajideen (as), anasema kwamba zuhdi duniani ni msingi wa subira mbele ya masaibu na misiba. Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) amenukuliwa katika Tafsiri ya Thaqalain akisema: 'Ali bin Hussein (as) alipofika mbele ya Yazid, alimtazama na kumwambia: Ewe Ali! Misiba inayokusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Hapo Ali bin Hussein (as) akamjibu kwa kusema: La Hasha!....Aya hii haikuteremka kutuhusu sisi bali zilizoteremka kutuhusu ni hizi zinazosema: Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi. Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Na sisi huwa hatuhuzuniki kwa yaliyotupotea katika mambo ya dunia wala kujitapa kwa yale tuliyopewa.'

***********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki kwa juma hili. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassallam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags