Jun 30, 2018 08:12 UTC
  • Aya na Hadithi (25)

Assalam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kipindi cha leo kitaendelea kujadili Aya ya an-Nur na aya nyingine tatu zinazofungamana nayo. Aya hizi ni miongoni mwa aya tukufu mno za kitabu kitakatifu cha Qur'ani ambazo huangaza nyoyo za waumini kwa mwongozo wa mbinguni na pia kwa mahaba na mapenzi ya minara maasumu ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlu Beit wake watoharifu (as).

Hivyo umewadia wakati wa kusikiliza kwa makini Aya hizi Tukufu za 35 hadi 38 za Surat an-Nur ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa yenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humuongoza kwenye Nuru Yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka. Ili Mwenyezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyatenda, na awazidishie katika fadhila Zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

Wapenzi wasikiliza, tulipata kujua baada ya kuzingatia kwa kifupi Aya hizi katika kipidi kilichopita kwamba zinatuongoza kufikia mjumuiko wa nuru maalum ya Mwenyezi Mungu, ambayo imetukuka na kujitenga na kila kasoro za kiitikadi za dunia ziwe ni za Mashariki au Magharibi. Bila shaka nuru hiyo inapatikana kwenye nyumba ambazo Mwenyezi Mungu amezijaza mwanga wake na hivyo kufanya wakazi wake kuwa Hoja yake kwa walimwengu ambapo watu na wakazi wa nyumba hizo huwa wamejaa na kunufaika na mwanga huo wa mbinguni katika harakati na maisha yao yote. Na vitabu vya kuaminika vya Hadithi vinasema wazi kwamba makudsudio ya nyumba hizo ni nyumba za Manabii (as) na tukufu zaidi kati ya nyumba hizo ni nyumba ya Bwana wa Mitume hao wote ambaye si mwingine bali ni Mtume wetu Mtukufu (saw). Tafsiri ya Majmaul Bayaan inafafanua kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake kwa kusema: 'Imepokelewa kwamba Mtume (saw) aliulizwa maana ya nyumba hizo aliposoma Aya hii naye akajibu: Ni nyumba za Manabii. Hapo Abu Bakr akasimama na kuuliza, huku akiwa anaashiria nyumba ya Ali na Fatimah, je, nyumba hii ni miongoni mwa nyumba hizo? Mtume akajibu: Nam, bali ni katika nyumba bora zaidi.'

 

Hapa tunazingatia kwa pamoja wapeni wasikilizaji Hadithi Tukufu ifuatayo ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi na vitabu viginevyo vya kuaminika vya Hadithi ambayo inaashiria nukta muhimu na ya kuvutia kwamba makusudio ya nyumba katika hadithi hiyo ni watu wanaoishi kwenye nyumba hizo na ambao wamejaa mwanaga wa hidaya na rehema ya Mwenyezi Mungu. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hamza ath-Thumali kwamba alisema: 'Abu Ja'ffar al-Baqir (as) alimuuliza Qatada, je, wewe ni nani? Naye akajibu: Mimi ni Qatada mwana wa Da'amat al-Baswari. Akamuuliza tena, je, wewe ni faqih wa watu wa Basra? Akajibu: Nam. Hapo Abu Ja'ffar akamwambia: Ole wako ewe Qatada! Hakika Mwenyezi Mungu ameumba kundi la watu miongoni mwa viumbe wake na kulijaalia kuwa Hoja (makhalifa) juu ya viumbe wake. Watu hao kwa hakika ni msingi na nguzo ya ardhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu nao ni wateule wa elimu Yake. Mwenyezi Mungu aliwateua kabla ya kuumba watu, nao walikuwa kivuli katika upande wa kulia wa Arshi Yake. Akasema: Hapo Qatada alinyamaza kimya kwa muda mrefu na kisha kusema: Mwenyezi Mungu akupe heri (akubariki)! Wallahi nimeketi mbele ya mafuqaha wengi na pia mbele ya Ibn Abbas lakini moyo wangu ulikuwa haujawahi kupiga (kwa kasi) kama unavyopiga hivi sasa mbele yako. Imam Baqir (as) akamwambia: Ole wako! Je, unajua uko wapi? Wewe uko sehemu ambayo 'Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala, na kutoa Zaka. Wewe uko katika sehemu kama hii ni sisi ndio hao watu waliokusudiwa…. Hapo Qatada akasema: Wallahi unasema kweli. Mwenyezi Mungu atufanye sisi kuwa fidia kwenu! Hakika nyumba hii si ya mawe wala udungo…'

***********

Hadithi Tukufu wapenzi wasikilizaji, zinatufahamisha kwamba kunufaika na mwanga wa wema hawa watukufu na maasumu wa Nyumba ya Bwana wa Mitume na Manabii (saw) kuna maana ya kuchukua mwanga na nuru safi na halisi ya hidaya ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuwawezesha waumini kunufaika vilivyo na nuru hiyo ya Mwenyezi Mungu katika miamala na harakati zao zote maishani. Imepokelewa katika Tafsiri ya Ali bin Ibrahim kutoka kwa Imam Ridha (as) kwamba alisema katika Hadithi moja ndefu kuhusiana na tafsiri ya Aya tukufu ya Nur: 'Sisi tumeshikamana na mkanda wa Mtume wetu (saw) ambapo na yeye Mtume ameshikamana na mkanda wa Mola wetu, na mkanda hapa ni nuru, na Mashia wetu wameshikamana na mkanda wetu. Mtu anayetuacha huangamia na anayetufuata huokoka….. Mtu anayeaga dunia hali ya kuwa anatupenda ni haki kwa Mwenyezi Mungu kumfufua pamoja na sisi. Sisi ni nuru kwa mtu anayetufuata na uokovu kwa anayefuata mwongozo wetu……. Na ni haki kwa Mwenyezi Mungu kumfufua walii wetu hali ya kuwa uso wake unang'ara na hoja zake kuwa wazi….'

 

Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa watu wanaoshikamana na nuru ya wilaya na mapenzi ya Ahlul Beit (as) huwa hawashughulishwi na jambo jingine linaloweza kuwaweka mbali na kusifu pamoja na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kama zinavyoashiria Aya tulizotangulia kuzisoma mwanzoni. Tunasoma pia katika kitabu cha al-Kafi kwamba Amir al-Mu'mineen (as) alipokuwa akishiriki vita alikuwa akishauri na kuwanasihi Waislamu kwa kusema: 'Chukueni ahadi juu ya jambo la Swala na kuihifadhi (kuiswali daima), na muikithirishe na kwayo jikurubisheni, kwani Swala ni wajibu uliowekewa wakati maalumu kwa waumini. Je, hamulisikii jibu la watu wa Motoni pindi watakapoulizwa: Ni kitu gani kilichowaingizeni Motoni? Watasema: Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali (Qur'ani; 74:42-43)……'Na wameitambua haki yake watu miongoni mwa waumini ambao hawashughulishwi na mapambo ya vitu (vya dunia kiasi cha kuwafanya waache swala), wala na kitulizo cha jicho miongoni mwa watoto na mali. Mwenyezi Mungu anasema: Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi (hakuwasahaulishi) kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusimamisha Swala na kutoa Zaka.'

Na tunasoma katika Tafsiri ya Nuru ath-Thaqalain kutoka kwa Asbaat bin Salim ambaye anasema: 'Nilifika mbele ya Abi Abdallah (Imam Swadiq) (as) na akauliza juu ya hali ya Umeir bin Salim. Nilisema: Ni mtu mzuri lakini ameacha kufanya biashara. Imam (as) akasema mara tatu: 'Hii ni kazi ya shetani.' Je, hajui kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alinunua bidhaa kutoka kwa msafara uliokuwa umetoka Sham na kisha kuiuza bidhaa hiyo kwa faida ambapo alipata kulipa deni lake na kuigawa faida iliyobaki miongoni mwa jamaa zake? Mwenyezi Mungu anasema: Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru (kumkumbuka) Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala, na kutoa Zaka. Imam Swadiq (as) aliendelea kusema: Wasimulizi wa visa wanasema Aya hii iliteremka kuwasifu watu wasiofanya biashara, lakini wanasema uongo. Hii ni kwa sababu Aya hii iliteremka kuzungumzia watu waliokuwa wakifanya biashara lakini bishara yao hiyo haikuwazuia kusimamisha Swala kwa wakati wake. Kisha Imam (as) alisema: Bila shaka watu hawa ni bora kuliko wale wanaoswali lakini hawafanyi biashara.'

 

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi kwa juma hili. Kipindi ambacho kumekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags