Jun 30, 2018 08:20 UTC
  • Aya na Hadithi (27)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza sehemu ya 27 ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambapo Aya zinazojadiliwa humu na kufafanuliwa kwa kina na Hadithi Tukufu huangaza na kuchangamsha nyoyo zetu.

Aya tutakayoijadili katika kipindi hiki cha leo ni Aya ya 125 ya Surat al-An'am, ambayo tunasoma na kuisikiliza hapa kwa makini, lakini kabla ya hapo tutangulia kusoma Aya tatu za kabla ya Aya hiyo. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya hizo: Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama yule aliye gizani akawa hata hawezi kutoka humo? Namna hiyo makafiri wamepambiwa waliyokuwa wakiyafanya. Kadhalika katika kila mji tumewajaalia wakubwa wa wakosefu wao wafanye vitimbi humo. Na wala hawafanyii vitimbi isipo kuwa nafsi zao, nao hawatambui. Na inapowajia Ishara, wao husema: Hatutoamini mpaka tupewe mfano wa waliyopewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi kuliko wote kujua wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia hao waliokosa udhalili na adhabu kali kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya. Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumwongoza humfungulia kifua chake Uislamu. Na anayetaka apotee hukifanya kifua chake kina dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia uchafu juu ya wasioamini.

 

Ndugu wasikilizaji, katika Aya ya kwanza kati ya aya hizi tulizosoma kuna mlinganisho wa hekima na busara kubwa kati ya mtu anayehuishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kupitia nuru inayomwongoza katika harakati zake na yule ambaye ameamua kubakia kwenye giza la maasi na kuabudu nafsi na matamanio. Hadithi Tukufu zimefasiri maisha na uhai hapa kwa maana ya uhai wa imani ambayo humfanikisha muumini kwa baraka za kufuata nuru ya khalifa maasumu wa Mwenyezi Mungu katika hali ambayo yule anayeamua kuifunga nafsi yake kwenye giza la maasi na madhambi ndiye huamua mwenyewe kutofuata nuru ya hidaya ambayo hupatikana kwa walii maasumu wa Mwenyezi Mungu. Aya ya nne inabainisha matunda ya uhai huu unaotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kumfungulia kifua yule anayemwongoza kupitia nuru ya mbinguni ambapo aya mbili za 122 na 123 zinabainisha hali ya wale watu waliozifunga nyoyo zao kwenye giza la dhambi na matokeo yao mabaya. Wao huzizamisha nafsi zao kwenye giza hilo na matokeo yake ni Mwenyezi Mungu kuwaajalia uchafu na adhabu kali na kufanya vifua vyao kuwa na dhiki na kubana. Hali hiyo huwafanya hata wasifikirie juu ya kujitoa kwenye giza hilo na hivyo kutopata fursa ya Mwenyezi Mungu kuwafungulia vifua vyao kwa nuru yake.

Allama Tabarsi anasema katika Tafsiri yake ya Majmaul Bayaan: 'Kuna Riwaya sahihi ambayo inasema kwamba Ayah ii ilipoteremka, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliulizwa maana ya kufunguliwa kifua naye akasema: Ni nuru ambayo Mwenyezi Mungu huirusha (huiweka) kwenye moyo wa muumini ambapo kifua chake hupata kufunguka na kupanuka. Wakamuuliza, je, kuna alama yoyote inayojulisha jambo hilo? Mtume (saw) akasema: Nam, kurejea kwenye nyumba (makao) ya kudumu milele, kuepuka nyumba ya ghururi na kujitayarisha kwa mauti kabla ya kuteremka mauti.'

Kuna Riwaya inayosema kwamba Maulana Imam Zeinul Abideen (as) katika usiku wa tarehe 27 katika mwezi mtukufu wa Ramadhani alikuwa akikariri sana dua ifuatayo: 'Allahuma! Niruzuku (nijaalie) kuepuka Nyumba (makao) ya ghururi na kurejea kwenye nyumba (makao) ya milele na kujitayarisha kwa ajili ya mauti kabla hayajafika.'

Imam Sajjad Zaynul Abidin AS

 

Hadithi tukufu zinatwambia kwamba miongoni mwa baraka za kufanikiwa kupata msaada huu muhimu wa Mwenyezi Mungu, yaani kufunguliwa kifua, ni mu'mini kuneemeka kutazama kupitia nuru ya Mwenyezi Mungu, jambo ambalo humuwezesha kutambua vyema haki katika mazingira ya kutokea fitina na kuchangayika haki na batili. Amir al-Mu'mineen Ali (as) amenukuliwa katika kitabu cha Ihtijaaj akisema kupitia Hadithi ndefu kwamba: 'Kutokana na kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ana rehema na huruma kubwa kwa viumbe wake na kutokana na kutambua kwake kuwa ungefika wakati ambapo waovu wangejaribu kupotosha maneno Yake, aligawa maneno yake katika sehemu tatu: Alijaalia sehemu ya kwanza ya maarifa ya Qur'ani kufahamika na wote wasomi na majahili (wasiokuwa wasomi), sehemu ya pili haifahamiki ila na wale walio na akili safi, hisia nyororo na shakhsia salama miongoni mwa watu waliofunguliwa vifua vyao Uislamu…….'

Na tunasoma katika kitabu cha al-Kafi Hadithi kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) ambapo anatunasihi tumuombe Mwenyezi Mungu atufungulie vifua vyetu kwa sababu miongoni mwa baraka zake ni malezi ya ulimi ambapo huwa hautamki ila haki na kuimarishwa matendo mema kwenye moyo. Anasema (as): 'Tambueni kwamba Mwenyezi Mungu anapomtakia mja kheri, humfungulia moyo wake kwa ajili ya kuukubali Uislamu. Hivyo anapompa hilo, ulimi wake hutamka haki na moyo wake kufungamana na haki ambapo hufanya kila jambo kwa mujibu wa haki hiyo. Mwenyezi Mungu anapomkusanyia mawili hayo, Uislamu wake huwa umekamilika. Anapoaga dunia katika hali hiyo huwa ameaga dunia hali ya kuwa ni Mwislamu wa kweli mbele ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu asipomtakia heri mja, humuacha peke yake na hivyo moyo wake kupata dhiki na kubana. Hivyo anapotamka haki moyo wake huwa haufungamani nayo. Hivyo inapokuwa kwamba moyo wake haufungamani na haki aliyotamka, Mwenyezi Mungu humnyima taufiki ya kuitekeleza haki hiyo. Mambo hayo yanapokusanyika kwake na kuaga dunia katika hali hiyo, huwa miongoni mwa wanafiki mbele ya Mwenyezi Mungu; na haki ile aliyoitamka lakini hakupewa na Mwenyezi Mungu taufiki ya kufungamana na moyo wake wala kuitekeleza, hugeuka na kuwa hoja dhidi yake. Hivyo mcheni (mwogopeni) Mwenyezi Mungu na mumuombe akufungulieni nyoyo zenu kwa ajili ya Uislamu na kuzifanya ndimi zenu ziseme haki hadi akufisheni mkiwa katika hali hiyohiyo.'

 

Kama ambavyo miongoni mwa baraka za kufunguliwa kifua na Mwenyezi Mungu ni kufanikiwa mumini kupata msaada Wake, ambao humkinga kutumbukia kwenye fitina na upotovu. Imam as-Swadiq (as) amenukuliwa akisema katika kitabu cha al-Kafi: 'Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anapomtakia heri mja, huweka moyoni mwake athari ya nuru, kufungua masikio ya moyo wake na kumpa Malaika anayemsaidia. Na anapomtakia mja mabaya, huweka moyoni mwake athari ya weusi, kufunga masikio ya moyo wake na kumuwekea shetani anayempotosha.'

Na Imam Ridha (as) anatubainishia kwamba kufunguliwa kifua hutimia katika kusalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumwamini na hii ni daraja ya juu zaidi ya imani. Kwa maana kwamba miongoni mwa baraka za kufunguliwa kifua ni kufanikiwa kupata nafsi iliyotua na kutulia pamoja na kuungana na waja wema wa Mwenyezi Mungu. Imam (as) anasema katika Hadithi iliyonukuliwa kutoka kwake katika kitabu cha at-Tauhid: 'Mwenyezi Mungu anapotaka kumuongoza mja kupitia imani yake humu duniani kufikia Pepo na nyumba ya utukufu wake huko Akhera, hufungua kifua chake kwa ajili ya kusalimu amri mbele Yake, kumwamini, kutulia na kuwa na yakini na ahadi za thawabu Zake. Na Mwenyezi Mungu anapotaka kupotosha na kumuweka mtu mbali na Pepo pamoja na nyumba ya utukufu Wake huko Akhera, kutokana na kumkufuru na kumuasi humu duniani, hufanya kifua chake kuwa na dhiki na kubana hadi kushuku katika kufri yake, moyo wake kuchanganyikiwa na kushuku (kuwa na wasiwasi) itikadi yake hadi kufikia mithili ya mtu anayepanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia uchafu juu ya wasioamini.'

************

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi kwa juma hili, ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags