Jun 30, 2018 08:32 UTC
  • Aya na Hadithi (28)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakukaribisheni tena muwe pamoja nasi ili tupate kusikiliza kwa pamoja sehemu hii ya 28 ya mfululizo wa vipindi hivi vya Aya na Hadithi.

Wapenzi wasikilizaji, maandiko matakatifu yanatwambia kwamba Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake mema na saada ya humu duniani na huko Akhera na si kama yanavyodai baadhi ya makundi yenye misimamo na itikadi za kupindukia mipaka kwamba Mwenyezi Mungu anataka waja wake wapiti mashaka na matatizo humu duniani ili wapate mafanikio huko Akhera. Kutokana na imani hiyo potovu, makundi hayo huwa yanajitesa na kujiharamishia mambo ambayo Mwenyezi Mungu mwenyewe ameyahalalisha, na hii ni bidaa hatari sana ambayo inakemewa na kupingwa na sheria tukufu za Mwenyezi Mungu. Tutaashiria hapa baadhi ya Aya na Hadithi tukufu ambazo zinaashiria ukweli huu ambapo tunaanza na Aya Tukufu za 31 hadi 33 za Surat A'raaf ambazo zinasema: Enyi wanaadamu! Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti, na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu (ubadhirifu). Kwa hakika Yeye hawapendi wanaofanya israfu. Sema: Ni nani aliyeharimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilowatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema: Hivyo ni kwa walioamini katika maisha ya dunia, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanaojua. Sema: Mola wangu ameharamisha mambo machafu ya dhahiri na ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asichokiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, Aya hizi tukufu zinawashauri waja kunufaika na riziki zilizo halali na nzuri ambazo wamejaaliwa na Mwenyezi Mungu katika hatua ya kwanza. Ni wazi kuwa kunufaika na neema hizi kwa nia hiyo ni ibada ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu Mtukufu moja kwa moja kwa sababu inaambatana na kutofanya israfu. Ni wazi kuwa kufanya israfu ni aina fulani ya kuwa mtumwa wa matamanio. Aya hizi pia zinatubainishia wazi kwamba kile kilichoharamishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, ni kila jambo lilalomdhuru mwanadamu na jamii nzima kwa ujumla, nayo ni maoavu na kila aina ya kuvuka mpaka katika matumizi ya kawaida anayoyahitajia mwanadamu pamoja na kukanyaga haki za watu wengine na vilevile kufuata ujahili na upotovu katika masuala ya kiitikadi, kama vile shirki na kusema mambo bila ya kuwa na elimu wala ufahamu wa kutosha kuhusiana nayo. Ama kuhusu vizuri katika riziki, ni wazi kuwa vizuri hivyo kwanza vinapasa kuwaendea waumini na waja wema humu duniani kabla ya kumuendela mtu mwingine yeyote navyo hivyo vitakuwa ni vyao tu katika maisha ya Akhera.

 

Ndugu wasikilizaji, ili kupata ufafanuzi zaidi wa suala hili, tunaashiria Hadithi ndefu ifuatayo ambayo imenukuliwa na Sheikh Tusi (MA) kutoka kwa Imam Ali (as). Imam (as) anasema: 'Fahamuni enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Ya kwamba wacha-Mungu wametambua vyema uzuri wa karibu (dunia) na mustakbali (Akhera). Wamekuwa washiriki (wamekuwa pamoja nao) wa wanadunia katika dunia yao lakini wanadunia hawajakuwa washiriki wao (hawajakuwa pamoja nao) katika Akhera yao. Mwenyezi Mungu amewajaalia kuwa mubaha (amewaruhusu) duniani kile kinachowatosheleza na kuwakinaisha. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Sema: Ni nani aliyeharimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilowatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema: Hivyo ni kwa walioamini katika maisha ya dunia, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanaojua. Wacha-Mungu wamekaa duniani kwa njia iliyo bora zaidi na kula chakula kilicho bora zaidi. Wameshirikiana na wanadunia (kuwa pamoja nao) kwenye dunia yao na kula pamoja nao chakula kilicho safi na kunywa nao vinywaji safi wanavyokunywa. Wamevaa nao nguo bora zaidi wanazovaa na kuishi kwenye maeneo bora zaidi wanayoishi. Wanaoa wanawake wazuri zaidi kama wanavyooa wao (wanadunia) na kupanda vipando bora zaidi kama wanavyopanda wao. Wamekuwa sawa na wanadunia katika kunufaika na ladha za duniani, ijapokuwa wao (wacha-Mungu) kesho watakuwa majirani wa Mwenyezi Mungu (watakuwa karibu Yake, kinyume na wanadunia). Atawapa kila kitu wanachokitamani na maombi yao yote kujibiwa. Hawatapungukiwa na ladha yoyote. Hivyo basi, enyi wacha-Mungu! Hili hulitamani (hulikimbilia) kila aliye na akili.'

 

Wapenzi wasikilizaji, Hadithi Tukufu zinatwambia kwamba kunufaika na riziki safi katika vyakula, mavazi na mambo mengine katika neema za Mwenyezi Mungu ni jambo linalompendeza na ni miongoni mwa kusimulia neema Zake, kama inavyosisitizwa mwishoni mwa Surat ad-Dhuhaa. Hivyo basi mtu yoyote anayenufaika na neema za Mwenyezi Mungu kwa nia hii safi bila shaka huwa amefanya ibada inayomridhisha Mwenyezi Mungu. Hebu tutazame Hadithi nyingine ambayo imenukuliwa katika Tafsiri ya Nur at-Thaqalain kutoka kwa Ibn al-Qaddaha ambaye anasema: 'Aba Abdillahi al-Swadiq (as) alikuwa ameniegemea- au alisema alikuwa amemuegemea baba yangu – ambapo Ubbad bin Kathir, aliyekuwa mmoja wa maulamaa wenye zuhudi kubwa wa Bani Abbas, alifika hapo na kumuona Imam akiwa amevalia vazi zuri la kupendeza…. Akasema: Eeh Aba Abdillah! Bila shaka wewe ni katika Ahlul Beit wa Mtume, na baba yako alikuwa vile. Hivyo ni vazi gani hili zuri (ghali) ambalo umelivaa? Kungelitokea nini kama ungelivaa vazi ambalo ni la kawaida? Hapo Imam Swadiq (as) akamjibu kwa kusema: Ole wako ewe Ubbad! Ni nani aliyeharimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilowatolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki? Mwenyezi Mungu anapomjalia mja wake neema, hupenda kuona athari za neema hiyo kwenye mja huyo. Ole wako ewe Ubbad! Mimi mwenyewe ni sehemu ya mwili wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), hivyo usiniudhi.'

Na mwishoni mwa kipindi hiki tunatazama Hadithi nyingine ya kuvutia inayohusiana na Imam Hassan (as) katika kufasiri Aya hizi tukufu. Hadithi hiyo iliyopokelewa na Khaithama imenukuliwa katika Tafsiri ya al-Ayyashi ambapo anasema: 'Kila wakati Imam al-Hassan bin Ali (as) alipokuwa akisimama kuswali, alikuwa akivalia mavazi yake mazuri zaidi na alipoulizwa: Ewe mwana wa Mtume! Ni kwa nini unavalia nguo zako zilizo bora zaidi? Alijibu: Hakika Mwenyezi Mungu ni Jamili na anapenda jamali. Hivyo ninajipamba kwa ajili ya Mola wangu ambaye anasema: Chukueni mapambo yenu katika kila msikiti. Hivyo ninapenda kuvalia nguo zangu zilizo bora zaidi.'

 

Na hivi ndivyo tunavyofikia mwisho wa kipindi cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho mmekuwa mkikitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi, huku tukikutakieni kila la kheri maishani. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags