Jan 25, 2018 03:11 UTC
  • Alkhamisi, Januari 25, 2018

Leo ni Alkhamisi 7 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na Januari 25, 2018.

Siku kama ya leo miaka 1050 iliyopita, alifariki dunia Ibn Ghalabun al-Halabi, msomi wa Qur'ani na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya hadithi wa enzi hizo. Ibn Ghalabun alizaliwa mjini Aleppo, Syria mnamo mwaka 309 Hijiria na kuishi nchini Misri. Alipata kusoma elimu ya hadithi na qiraa ya Qur'ani Tukufu kwa wasomi wengi wa zama zake na kutokea kuwa mwalimu katika uwanja huo. Vilevile ametoa maoni na nadharia zake kuhusiana na qiraa ya Qur'ani ambazo zimeandika katika kitabu cha 'Al-Kashf kilichoandikwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abi Twalib.' Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni  'Al-Irshad' ambacho kinazungumzia qiraa saba za Qur'ani tukufu.

Katika siku kama ya leo miaka 562 iliyopita, kazi ya uchapishaji vitabu ilianza na kitabu cha kwanza kabisa kikachapishwa kwa kutumia mashine iliyogunduliwa na Mjerumani, Johannes Gutenberg. Mashine hiyo ya uchapishaji ilikuwa hatua muhimu katika njia ya uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.' Hii leo kurasa kadhaa zilizobakia za kitabu hicho zinahifadhiwa katika majumba ya makumbusho.

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita vijidudu maradhi vinavyosababisha maradhi ya ukoma viligunduliwa na tabibu na mhakiki wa Norway kwa jina la Gerhard Henrik Armauer Hansen. Ugonjwa huo huambatana na vidonda vikali vinavyovuruga na kuharibu maumbo ya muathirika. Vijidudu maradhi vya ugonjwa huo wa ukoma pia hukusanyika katika mishipa ya neva na kusababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya mishipa hiyo. Maradhi hayo hujitokeza zaidi katika maeneo yenye joto. Licha ya maendeleo makubwa ya kisayansi yaliyopatikana katika kudhibiti ugonjwa wa ukoma, lakini njia ya kutibu maradhi hayo sugu bado haijapatikana na idadi kubwa ya waathirika wake wanaendelea kuteseka katika nchi mbalimbali duniani.

Gerhard Henrik Armauer Hansen

Miaka 53 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo Sayyid Qutb msomi na mwanamapambano wa Misri alinyongwa pamoja na wenzake wawili huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Msomi huyo alihifadhi Qur'ani tukufu katika ujana wake. Sayyid Qutb alifahamiana na Hassan al Bana na kujiunga na harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchi hiyo wakati alipokuwa akiendesha harakati za kisiasa. Sayyid Qutb alitiwa nguvuni na baadaye kunyongwa baada ya kuzuka hitilafu kati ya Gamal Abdel Nasser Rais wa wakati huo wa Misri na Ikhwanul Muslimin. Msomi huyo alikuwa akiiamini kwamba "kambi za Mashariki na Magharibi zinapigana na Waislamu na kwamba kambi mbili hizo zimeungana ili kupora maliasili za nchi za Kiislamu". Miongoni mwa vitabu vya msomi na mwanamapambano huyo wa Kiislamu ni kile alichokipa jina la" Uislamu na Amani ya Kimataifa".

Sayyid Qutb

Na siku  kama ya leo miaka 12 iliyopita Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge ikiwa ni mara ya kwanza kwa harakati hiyo kushiriki kwenye zoezi hilo. Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na waangalizi wa kigeni, Hamas ilifanikiwa kupata viti 76 kati ya jumla viti 132 vya Bunge la Palestina licha ya propaganda chafu zilizokuwa zikifanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Kwa utaratibu huo Hamas ilimuarifisha Ismail Hania kama Waziri Mkuu na kutangaza kwamba itaunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na muitifaki wake Israel, zilikataa kutambua rasmi serikali hiyo iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Palestina.

 

Tags