Feb 09, 2018 02:41 UTC
  • Ijumaa tarehe 9 Februari, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 22 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na Februari 9, 2018.

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini. Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah. Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la mamluki hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangusha utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.

Wananchi wa Tehran wakipambana na gadi ya Shah

Miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi. Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq.

Operesheni ya Walfajiri 8

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, baada ya Chama cha Wokovu wa Kiislamu cha Algeria (FIS) kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Bunge, wanajeshi waliokuwa wakitawala nchini humo, walibatilisha matokeo ya uchaguzi huo na kukipiga marufuku chama hicho, hali iliyopelekea kuzuka machafuko makubwa. Machafuko hayo yalipelekea kuuawa watu wengi nchini Algeria.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani