Mar 12, 2018 11:24 UTC
  • Usimwambie uongo  mtu ambaye anakuamini; na usimuamini mtu ambaye anakwambia uongo\
    Usimwambie uongo mtu ambaye anakuamini; na usimuamini mtu ambaye anakwambia uongo\".

Ni wakati mwingine wapenzi wasikilizaji mnapojiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Sehemu iliyopita ya mfululizo huu ilijadili maudhi ya kuwakera watu wengine na jinsi suala hili lilivyokemewa na kukatazwa katika Uislamu. Tulisema kuwa, heshima na kumuenzi ndugu muumini ni jambo ambalo limekokotezwa na kutiliwa mkazo mno katika mafundisho ya Kiislamu, kiasi kwamba, hakuna mtu mwenye haki ya kumuudhi muumini. Tulieleza pia kwamba, kuwaudhi watu wengine ni katika madhambi makubwa na mambo machafu ya kimaadili ambayo huyakwaza maisha ya mtu binafsi na ya kijamii haopa duniani na kesho Akhera. Tulinukuu hadithi ya Mtume Muhammad SAW ambaye alinukuliwa akisema: Yeyote atakayemuudhi Muumini, kwa hakika ameniudhi mimi na mwenye kuniudhi mimi kwa hakika amemuudhi mwenyezi Mungu na yeyote mwenye kumuudhi Mwenyezi Mungu kama ilivyokuja katika Torati, Injili na Qur’ani yuko mbali na rehma ya Mwenyezi Mungu. 

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 110 itazungumzia tabia mbaya ya kusema uongo. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kusema uongo ni katika aibu na mapungufu mabaya kabisa na ni katika madhambi makubwa kabisa. Uongo kwa hakika ni chimbuko la mambo mengi machafu na mabaya. Katika mafundisho ya Kiislamu uongo au kusema uongo kunatajwa kuwa chimbuko la machafu mengi. Aidha katika baadhi ya hadithi uongo unaelezwa kuwa ni ufunguo wa mambo yote machafu na mabaya.

Ole wako na uongo..."

 

Imam Hassan Askary AS anasema: Uongo ni ufunguo wa kila shari. Aidha amesema: Machafu yote yamewekwa ndani ya nyumba na ufunguo wa nyumba hiyo ni uongo.

Moja ya mahusiano ya uongo na dhambi nyingine ni kwamba, mtu mwongo na mdanganyifu daima hujitenga na kusema ukweli, kwani kusema ukweli kutamuumbua na kumfedhehesha. Na ndio maana daima husema uongo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana uongo ukawa ni chimbuko la nifaki pia. Kusema ukweli maana yake ni hali ya kuweko uwiano baina ya ulimi na moyo. Hii ni katika hali ambayo, uongo ni hali ya kutokuweko uwiano na uratibu baina ya viungo viwili hivyo. Kwa maana kwamba, ulimi unasema kitu ambacho hakiko moyoni. Aidha nifaki ni kitu cha dhahiri na kisicho cha batini. Kwa maana kwamba, mtu anasema kitu kingine ambacho hakiko ndani ya moyo wake. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Mtume SAW alipoulizwa, je mtu muumini anaweza kuwa mwoga? Akasema, ndio! Kisha akaulizwa: Je inawezekana muumini akawa bakhili na mwenye mkono wa birika? Akajibu kwa kusema: Ndio! Kisha akaulizwa je yumkini muumini akawa mwongo? Akajibu kwa kusema, hapana, katu muumini hawezi kuwa mtu mwongo.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, sababu ya mtu kusema uongo ni hofu ya umasikini na wakati mwingine hofu ya kupoteza nafasi na cheo alichonacho na wakati mwingine ni kutokana na anayesema uongo kupenda mno mali, jaha na uongozi. Wajuzi wengine wa mambo wanaamini kwamba, mtu anayesema uongo huwa na nakisi na mapungufu na hutaka kufidia mapungufu hayo kwa kusema uongo. Hata hivyo kuna watu wengine ambao ni wagonjwa na wanaugua maradhi ya kusema uongo ambapo katu ni muhali kusikia akisema kweli.

Usimuulize mwongo kwa nini amesema uongo, kwani bila shaka atakujibu kwa majibu ya uongo.

 

Muumini wa kweli ni yule ambaye ameupokea ukweli kwa ujudi na uwepo wake wote kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mtatuzi wa matatizo yake yote. Lakini mtu mwongo akiwa na nia ya kufikia lengo lake, huutumia uongo kama wenzo wake athirifu kwa ajili ya kufikia mradi wake na kwa hakika hii ndio ile shirki ndogo, hafifu na isiyoonekana iliyoelezwa katika baadhi ya hadithi. Huu kwa hakika ni udhaifu na nakisi ya mtu mwongo kuhusiana na taathira ya Mwenyezi Mungu katika mambo.

Imam Muhammad Baqir AS anasema: Uongo hubomoa nyumba ya imani.

Baadhi ya hadithi zinaonyesha kuwa, mtu mwongo katu hawezi kuonja ladha ya imani. Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa kuhusiana na hilo akisema kuwa: Madhali mtu angali anasema uongo na hajaacha tabia hiyo, iwe ni kwa utani au kwa jaddi, hataonja ladha ya imani.

Kwa hakika moja ya rasilimali muhimu kabisa za jamii, ni kuweko hali ya kuaminiana baina ya wanajamii na kitu kikubwa kinachoangamiza rasilimali hii ni uongo.

 Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Bwana Mtume SAW na Maimamu watoharifu AS wakiwa na lengo la kulinda na kuhifadhi rasilimali hii, walikuwa wakiwakataza waumini kufanya urafiki na makundi kadhaa wakiwemo watu waongo. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Jizuie kuingiliana na mwongo; na ikibidi kuingiliana naye, basi usimsadiki wala usimfanye ajue kwamba wajua asema uongo, kwa sababu ataacha urafiki nawe, lakini hatoacha tabia yake ya kusema uongo.

Miongoni mwa madhara ya kijamii ya mtu kusema uongo ni kutoaminiwa na watu. Hali hiyo huwa mbaya kiasi kwamba, hata ikitokea msema uongo amesema neno la kweli, watu hawamuani kwani ameshakuwa mashuhuri baina ya watu kwa uongo.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anaashiria nukta hiyo kwa kusema: Ajulikanaye kwa kusema uwongo, hupungua kuaminiwa kwake. Aidha anasema katika sehemu nyingine kwamba: Mwislamu anapaswa kujiweka mbali na kutofanya udugu na urafiki na mtu mwongo, kwani kutokana na mtu huyo kusema uongo, hata akisema ukweli si mwenye kuaminiwa.

Mwongo hafichi ukweli, bali anachokifanya ni kuchelewesha kufahamika kwake

 

Wapenzi wasikilizaji kula yamini au kiapo ni katika mbinu zinazotumiwa kwa ajili ya kuwafanya wanajamii wengine wamuamini mtu. Hata hivyo baadhi ya watu hasa waongo hutumia suala la halafa na kiapo kama ilivyo kwa jambo jingine tukufu, kama wenzo wa kuwahadaa watu wengine. Hii ni katika hali ambayo, Mwenyezi Mungu amewaonya na kuwatahadharisha waumini na jamii za mwanadamu kwamba, wasiyafanye matukufu kama Allah na kiapo, kama kitu cha kufikia malengo yao ya kidunia. Aidha wamewataka wasiyatumie matukufu hayo kwa ajili ya kula viapo batili na vya uongo, na hivyo kutokuwa sababu ya kudhoofishwa matukufu na itikadi katika jamii. Hii ni kutokana na kuwa, kufanya hivyo, hakuna kheri hapa duniani wala Akhera na kitendo hicho hakina kingine ghairi ya kuporomoka wao na jamii. Aya ya 95 ya Surat an-Nahl inasema:

Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajua. Aidha ya 14 na 15 za Surat al-Mujaadah zinasema:

 Huwaoni wale waliofanya urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uongo, na hali ya kuwa wanajua. Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyokuwa wakiyatenda ni maovu kabisa.

Mtume SAW anakitaja kiapo cha uongo kuwa ni katika dhambi chafu na mbaya kabisa na ni katika mapungufu mabaya mno. Anasema: Mwene kuapa kwa kumtaja Mwenyezi Mungu na kiapo chake kikawa na uwongo wa kiwango cha bawa la mbu, hujitokeza doa jeusi katika moyo wake na litabakia mpaka Siku ya Kiyama.

Aidha Mtume SAW amesema kuwa: Makundi matatu ya watu ambayo Mwenyezi Mungu hatazungumza nayo Siku ya Kiyama, ayatapuuza na kutoyatakasia dhambi zake ni kundi la watu ambao wanapotoa hutoa kwa masimbulizi na masimango. Pili watu ambao wanauza bidhaa zao kwa kiapo cha uongo na kundi la tatu ni la watu wenye kiburi.

Katika baadhi ya hadithi, kusema uwongo kunatajwa kuwa ni kubaya zaidi kuliko hata riba. Mbora huyo wa viumbe anasema: Riba mbaya kabisa na ya juu zaidi ni uongo.

Kwa leo wapenzi wasikilizaji tunakomea hapa, msisite kujiunga nami wiki ijayo, katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…