Mar 12, 2018 23:10 UTC
  • Jumanne tarehe 13 Machi, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 24 Jamadithani 1439 Hijria sawa na 13 Machi, 2018.

Siku kama ya leo miaka 895 iliyopita alifariki dunia Ahmad Bin Ali Baihaqi Sabzavari, mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya Qur’ani mjini Neishabur. Ali Baihaqi Sabzavari alitabahari katika elimu ya fasihi lugha ya Kiarabu kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake na vilevile katika tafsiri ya Qur’an Tukufu. Msomi huyo wa Kiislamu pia alikuwa mahiri katika qiraa ya Qur’an Tukufu. Ali Baihaqi Sabzavari ameandika vitabu mbalimbali vikiwemo vile vya ‘Taajul-Maswadir’ ‘Al-Muhit bi Ilmilil Qur’an.’

Siku kama ya leo miaka 285 iliyopita, yaani 13 Machi, 1733 alizaliwa Joseph Priestley, mkemia na mwanafizikia wa Uingereza. Msomi huyo aliishi katika kipindi kilichokuwa maarufu kama zama za dhahabu za kemia na elimu hiyo ilikuwa imepiga hatua. Katika uchunguzi na utafiti wake, Priestley alivumbua uvutaji pumzi katika mimea na gesi za oksijeni na haidrojeni. Joseph Priestley alifariki dunia mwaka 1804.

Joseph Priestley

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita sawa na tarahe 13 Machi 1948, Wazayuni waliokuwa na mfungamano na kundi la kigaidi la Haganah walishambulia kitongoji cha Wapalestina cha Husseiniyah katika eneo la kaskazini mwa Jalilah. Wazayuni hao licha ya kuwaua shahidi zaidi ya Wapalestina 60, waliharibu nyumba zao kadhaa. Hali kadhalika katika siku hiyo hiyo, wanajeshi wa Israel walizilipua kwa mabomu nyumba za Wapalestina katika eneo la 'Qatmuun' lililoko Baitul Muqaddas. Mauaji ya Waislamu wa Palestina yaliyofanywa na makundi ya kigaidi ya Israel yalitekelezwa kwa lengo la kutaka kutangaza uwepo wa utawala huo bandia kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina baada ya kuondoka vikosi vya majeshi ya Uingereza katika eneo hilo.

Miaka 38 iliyopita inayosadifiana na tarahe 22 Esfand 1357 Hijria Shamsia, Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa taasisi ya kushughulikia masuala ya familia za mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini. Taasisi hiyo hadi sasa bado inaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa familia za mashahidi wa harakati za mapinduzi na familia za mashahidi wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, katika kuwapatia huduma za kiutamaduni, kijamii na kiuchumi.

Taasisi ya Mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali.

Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani