Jumapili 18 Mach
Leo ni Jumapili tarehe 29 Jamadi th-Thani 1439 Hijiria, mwafaka na tarehe 18 Machi 2018, Miladia.
Siku kama ya lao miaka 205 iliyopita, alizaliwa Christian Friedrich Hebbel fasihi na mkosoaji mkubwa wa Ujerumani. Akiwa kijana mdogo na kutokana na kufariki dunia baba yake, alilazimika kufanya kazi katika kiwanda cha kuchapisha magazeti kwa lengo la kujidhaminia mahitaji yake. Hata hivyo baada ya kufanya tafiti kadhaa na kujiongezea maarifa, alianza kazi ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 20 Christian Hebbel alianza kusambaza Makala zake kwa ajili ya kuchapishwa katika magazeti ya fasihi ya mjini Hamburg, Ujerumani. Baada ya hapo alijiendeleza zaidi kielimu ambapo sambamba na kuendelea na masomo pia alikuwa akijihusisha na kazi za fasihi na kuandika michezo ya sinema mbalimbali ambapo pia katika uwanja huo ameacha athari katika uga wa fasihi na nadharia za ukosoaji. Hebbel alifariki dunia mwaka 1863 Miladia akiwa na umri wa miaka 50.
Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli. Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi. Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, hatimaye mapambano ya wananchi Waislamu wa Algeria yaliyoanzishwa kwa lengo la kuikomboa nchi hiyo na kukomesha uvamizi wa kikoloni wa Ufaransa yalipata ushindi baada ya miaka minane ya vita vikali. Watu milioni moja waliuawa katika vita hivyo. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pili wa Evian, Ufaransa ilitambua uhuru wa Algeria na kuwaondoa wanajeshi wake nchini humo. Hata hivyo jeshi la siri la Ufaransa liliendeleza operesheni za kigaidi kwa muda nchini Algeria. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Algeria wakati huo ilikuwa ikiongozwa na Yusuf bin Khada na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya utawala wa Ahmad bin Bella.
Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, Mahatma Gandhi, kiongozi mpigania uhuru wa India aliyekuwa akifanya jitihada za kuiondoa nchi hiyo katika ukoloni wa Uingereza kwa njia ya amani alikamatwa na baadaye kuhukumiwa kifungo cha miaka 6 jela. Kutiwa mbaroni Gandhi kulizidisha hasira na chuki za wananchi wa India dhidi ya Waingereza na kutia nguvu azma yao ya kupambana kwa ajili ya kuikomboa nchi yao. Katika mapambano yake Gandhi alitumia mbinu iliyoitwa 'Satyagraha' ambayo inamaanisha kutafuta hakika na kweli. Mbinu hiyo isiyotumia mabavu na ghasia, ilikusudiwa kudhihirisha makosa ya adui na kumlazimisha abadili mwenendo wake.
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita alifariki dunia Mfalme Farouk aliyeuzuliwa madarakani wa Misri. Farouk alizaliwa mwaka 1920 Miladia. Wakati alipozaliwa baba yake yaani Ahmad Fuad, alikuwa na cheo cha Pasha (waziri mkuu) ambapo alikuwa akiitwa, Fuad wa kwanza katika ufalme wa nchi hiyo, ambaye baadaye naye alikuja kuwa mfalme wa Misri pia. Katika kipindi hicho utawala wa nchi hiyo ulikuwa chini ya uungaji mkono wa Uingereza. Baada ya baba yake kufariki dunia mwaka 1936 na akiwa na umri wa miaka 16 pekee Farouk alichukua hatamu za uongozi na kwa kuwa alikuwa bado hajafikisha umri wa kisheria wa nafasi hiyo, hivyo ungozi ulikabidhiwa kwa Baraza la Niaba la Ufalme. Katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia na kutokana na kujiri mapigano kati ya nguvu zilizokuwa na tofauti huko kaskazini mwa Afrika, Misri pia iligeuka na kuwa mrengo na kambi muhimu ya waitifaki hususan Uingereza. Mwaka 1944 Farouk alitwaa mamkala kamili ya Misri na baada ya kuasisiwa utawala haramu wa Kizayuni na akishirikiana na nchi za Kiarabu aliingia vitani na utawala huo. Hata hivyo vita hivyo vilimalizika kwa kushindwa jeshi la Misri na utawala huo bandia ambapo kufuatia hali hiyo raia wa Misri walitokea kumchukia mtawala huyo. Hasira hizo za wananchi na pia ufisadi uliokuwa umekita mizizi ndani ya utawala wake, viliandaa mazingira ya kujiri mapinduzi yaliyoratibiwa kati ya Jenerali Najib na Gamal Abdel Nasser dhidi ya Farouk. Na hatimaye mfalme huyo akalazimika kujiuzulu tarehe 26 Julai mwaka 1952 Miladia.