Mar 19, 2018 06:16 UTC
  • Ulimwengu wa Soka, Machi 19

Hujambo mpenzi msikilizaji wa RT na karibu tuangazie matukio muhimu yaliyojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.....

Mchuano wa kirafiki; Iran yaidhalilisha Sierra Leone

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeichabanga timu chovu ya Afrika ya Sierra Leone katika mchuano wa kirafiki uliopigwa Jumamosi katika Uwanja Taifa wa Azadi hapa mjini Tehran. Katika mchezo huo ambao vijana wa Iran waliutumia kujitutumua misuli kuelekea Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Russia, vijana wa Team Melli kama wanavyojulikana hapa nchini waliinyuka Sierra Leone mabao 4-0. Kiungo Mohammad Reza Khanzadeh ndiye alifungua mvua ya magoli dhidi ya vijana hao wa Kiafrika, kupitia goli alilolitia kimyani chini ya robo saa baada ya kuanza mchezo.

Mchezaji wa Sierra Leone akimkaba Muirani uwanjani Azadi

Dakika tatu baadaye, Ali Gholizadeh alicheka na nyavu, huku Kaveh Rezaei akiipa Iran la tatu, zikiwa zimesalia dakika 10 kipindi cha kwanza kimalizike.

Gholizadeh alifunga bao lake la pili likiwa ni la nne na la mwisho kwa Iran, katika dakika ya 47, na hivyo kupoteza matumaini ya Sierra Leone kujipapatua.

Iran itasafiri kaskazini mwa Afrika kwenda kuvaana na Tunisia Machi 23, na siku nne baadaye, watatoana udhia na Algeria nchini Austria. Team Melli itapepetana na Morocco katika mchuano wa kwanza wa Kundi B katika Kombe la Dunia nchini Russia Juni 15, kabla ya kukutana na Uhispania na Ureno katika mechi nyingine za makundi Juni 20 na 25 kwa usanjari huo.

Wanariadha wa Iran wazoa medali 23 mashindano ya Fazza UAE

Wanariadha wenye ulemavu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali kochokocho katika mashindano ya kimataifa ya Fazza mjini Dubai, huko Umoja wa Falme za Kiarabu. Wananariadha wa kike na kiume wa Iran wametwaa medali 23, zikiwemo dhahabu 6, katika duru ya 10 ya mashindano hayo yanayofahamika kama Fazza International Athletics Championships – Dubai 2018 World Para Athletics Grand Prix. Ijumaa ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya mashindano hayo, Muirani Abdolreza Jokar alirusha mkuki umbali wa mita 19.7 katika kitego cha F53/54 na kutwaa medali ya dhahabu. Muirani mwingine Ali Shamshiri, aliipa Iran dhahabu nyingine katika mchezo wa kurusha kitufe kategoria ya F12. Mashindano hayo ya mabingwa walemavu wa riadha yalianza Machi 13 na kumalizika tarehe 16.

Gor, Simba na Yanga zashindwa kutamba, zaondolewa CAF

Klabu ya Simba ya Tanzania imeondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF, baada ya kulazimishwa sare tasa na al-Masry ya Misri katika mchezo wa marudiano siku ya Jumamosi. Safari ya Wekundu wa Msimbazi  ya kuwania kufuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo ya CAF, ilihitimishwa katika uwanja wa Port Said nchini Misry baada ya kucheza mchezo wao wa marudiano dhidi ya Al Masry na kuambulia sare tasa. Simba katika mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiwa nyumbani ilifanya kosa la kuruhusu kufungwa magoli mawili katika mchezo uliyomalizika kwa sare ya kufungana magoli 2-2, hivyo Jumamosi walikuwa wanahitajika kupata japo ushindi wa goli 1-0 au sare ya kuanzia 3-3. Kwa sare hiyo ya mtungi kwa mtungi na kutokana na mchezo wa kwanza wa nyumbani waliotoka sare ya 2-2, Simba wanaondolewa katika michuano hiyo kwa goli la ugenini, licha ya makeke haya ya Masoud Djuma, naibu mkufunzi wa Simba kabla ya mchuano huo.

Klabu ya Yanga katika mchuano wa huko nyuma

Mwakilishi mwingine wa Tanzania katika mashindano hayo, Yanga, pia mambo yaliwaendea segemnege. Yanga walisafiri kwenda Gaborone mji mkuu wa Botswana wakiwa nyuma kwa magoli 2-1 baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani, hivyo waliingia Botswana wakihitaji ushindi wa kuanzia magoli 2-0 na kuendelea ili waweze kufuzu. Hata hivyo maji yalizidi unga na vijana hao wa Tanzania wakajikuta wanalazimishwa sare tasa na Township Rollers. Vijana wa Township Rollers waliweka ulinzi wa kutosha na kutoruhusu goli. Kwa msingi huo Township Rollers inakuwa klabu ya kwanza Botswana kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika historia. Nahodha ya Yanga hata hivyo amesisitiza kuwa kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa kusonga sima.

Katika matokeo mengine ya Ligi ya Mabingwa, mwakilishi wa Kenya klabu ya Gor Mahia maarufu kama Kogalo walitandikwa bao 1-0 na Esperence de Tunis ya Tunisia, na hivyo kuondolewa kwenye michuano hiyo kichwa chini mikono nyuma. KCCA ya Uganda iliishinda ST. Georges ya Ethiopia kwa bao 1-0 na kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya pili mfululizo, huku Mbabane Swallows ya Swaziland ikiishinda Zanaco ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-0. APR ya Rwanda nayo ilitolewa mashindanoni na Djoliba licha ya kushinda mabao 2-1, kwa kuwa ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza kwenye mchuano wa Shirikisho.

Hatua za kinidhamu dhidi ya Makamu wa Rais wa TFF

Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania TFF, imemuhukumu Makamu wa Rais wa shirikisho hilo Michael Wambura baada ya kupatikana na hatia katika makosa matatu yaliyokuwa yakimkabili. Makosa yaliyokuwa yakimkabili kiongozi huyo ni kupokea fedha za Shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013. Makosa mengine ni Kughushi barua ya kueleza alipwe malipo ya Kampuni ya JEKC SYSTEM LIMITED huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013 na Kufanya Vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na Ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (Kama ilivyorekebishwa 2015). Kamati ya maadili iliyotoa uamuzi huo ilikutana Machi 14 Jijini Dar es Salaam na kupitia shauri hilo kabla ya kutoa uamuzi wao Alkhamisi.

Rais wa TFF

Kamati ya maadili pia imependekeza Michael Wambura afikishwe kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi huku pia ikipendekeza viongozi wa zamani wa TFF, Jamal Malinzi aliyekuwa rais, Celestine Mwesigwa aliyekuwa katibu mkuu ambao walikuwepo wakati vitendo hivyo vikifanyika waunganishwe kwenye uchunguzi. Michael Wambura ametaja hukumu dhidi yake kama hujuma ya kimkakati na wala sio masuala ya maadili na sharia.

Droo ya Robo-fainali UEFA

Ijumaa ya Machi 16, Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA, ikiwa ni siku mbili baada ya kumalizika kwa hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya walichezesha droo ya robo fainali. Kwa mujibu wa orodha hiyo ya UEFA, Barcelona watavaana na Roma huku Juventus ikikabana koo na Real Madrid. Sevilla itahitajika kujituma zaidi ili kuishinda Bayern huku robo fainali inayoonekana fainali ikiwa kati ya Liverpool na ManCity. Chelsea imeshindwa kula meza moja na mibabe ya soka baada ya kuchabangwa magoli 3-0 na Bercelona uwanjani Camp Nou. Itakumbukwa kuwa, timu hizi zilitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa awali wa hatua ya makundi. Mabao ya Berca yalifungwa na Lionel Messi aliyepachika wavuni mawili na Osmane Dembele.

Lionel Messi akiwa uwanjani

Katika michuano ya kuelekea nusu fainali ya Kombe la FA wikendi, Wigan Athletic waliondoshwa na Southampton kwa kichapo cha bao 2-0, huku Chelsea wakijikatia tiketi ya kusonga mbele baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 walipovaana na Leceister City. Magoli ya The Blues yalifungwa Alvaro Morata na Pedro Eliezer Rodríguez.  Kwa matokeo hayo Southampton na Chelsea zinaungana na Manchester United na Tottenham katika hatua ya nusu fainal. Manchester U ilifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brighton, yaliyofungwa na Romelu Lukaku na Nemanja Matic huku Southampton wakisonga mbele kwa ushindgi wa magoli 3-0 dhidi ya Swansea.

……………………TAMATI……………….

 

Tags