Apr 15, 2018 02:18 UTC
  • Jumapili, Aprili 15, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 28 Rajab 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 15 Aprili mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, ilianza safari ya msafara wa Imam Hussein (as) kutoka Madina kwenda mjini Makkah. Hatua hiyo ilijiri baada ya kufariki dunia Muawiyah Bin Abu Sufiyan tarehe 15 ya mwezi wa Rajab na kutwaa madaraka mwanaye, Yazid Bin Muawiyah. Baada ya Yazid kutwaa madaraka, haraka sana alimtaka mtawala wa mji wa Madina amlazimishe Imamu Hussein (as) kutoa baia (kiapo cha utiifu) kwake na kwamba iwapo angekataa kufanya hivyo basi amuuwe. Kwa kuzingatia kwamba Yazid alikuwa mtu muovu na mtenda madhambi, Imamu Hussein alikataa kutoa kiapo hicho na kwa ajili hiyo akaamua kuondoka Madina yeye na watu wa familia ya Mtume Muhammad (saw) kuelekea mjini Makkah. Kabla ya kuanza safari hiyo, Imamu Hussein (as) alimuusia kaka yake Muhammad Ibnil-Hanafiyyah akisema: "Ninatoka kwa ajili ya kurekebisha umma wa babu yangu Mtume wa Mwenyezi Mungu saw, ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu na kupita njia ya babu yangu Muhammad na baba yangu Ali Ibn Abi Twalib (as)…." Baada ya kufika mjini Makkah, baadaye na kufuatia kukithiri barua za watu wa mji wa Kufa Iraq, waliokuwa wamemtaka aelekee mji huo ili awaongoze, Imamu Hussein (as) aliamua kuelekea mji huo ambapo hata hivyo alizuiliwa na jeshi la Yazid eneo la Karbala na kuuawa shahidi yeye na watu wa familia ya Mtume (saw) katika eneo hilo.

Msafara wa Imamu Hussein (as).

Siku kama ya leo miaka 566 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mashuhuri wa kutengeneza vinyago wa Italia Leonardo da Vinci. Alionesha kipaji kikubwa cha kuchora akiwa bado mtoto mdogo na alikweya daraja za juu katika fani hiyo haraka mno. Mwaka 1506 Miladia da Vinci alichaguliwa kuwa mchoraji wa Mfalme Luis wa 12 kisha akawa mchoraji wa Mfalme Francis wa Kwanza. Mbali na uhodari wake katika kuchora na kutengeneza vinyago, Leonardo da Vinci pia alisomea fizikia na hisabati. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni michoro ya kanisa kuu la mji wa Milan, mchoro wa picha ya "Tabasamu la Jugund," picha ya Mona Lisa na ya Karamu ya Mwisho ya Issa Masih (as). Leonardo da Vinci alifariki dunia mwaka 1519 akiwa na umri wa miaka 67.

Leonardo da Vinci

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita meli kubwa ya abiria ya Titanic ambayo ilitambuliwa kuwa nembo ya mafanikio makubwa ya viwanda vya meli vya wakati huo iligonga mwamba wa theluji na kugharibi katika Bahari ya Atlantic, katika safari yake ya kwanza kutoka bandari ya Southampon nchini Uingereza kuelekea New York, Marekani. Zama hizo Titanic ilitambuliwa kuwa meli kubwa zaidi na ya kifahari kuliko meli nyingine zote duniani. Watengenezaji wa meli hiyo walikuwa wakisema kuwa haingeweza kughariki na kuzama. Ni wasafiri 705 tu kati ya abiria wake wote 2207 waliokuwemo kwenye meli hiyo ndio waliookoka katika ajali hiyo. Ajali hiyo inatambuliwa kuwa ajali mbaya zaidi ya baharini na iliyosababisha idadi kubwa ya vifo vya watu duniani.

Meli kubwa ya abiria ya Titanic

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita alifariki dunia Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammed Kazem Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa elimu ya fiqhi. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alijiunga na hauza ya kielimu ya mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Shirazi ambapo alifikia daraja ya ijtihadi. Baada ya hapo alijishughulisha na kazi ya ufundishaji huku akihusika pia na kuasisi vituo vya misaada, misikiti na shule za kidini. Ameacha taathira mbalimbali lakini maarufu ni kitabu cha 'Urwatul-Wuthqa' na 'Bustane Niyaz' ambacho kinahusiana na dua.

Ayatullahil-Udhma Sayyid Mohammed Kazem Yazdi

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, yaani sawa na tarehe 15 Aprili 1988, shirika la ujasusi la utawala bandia wa Israel MOSSAD lilimuua shahidi Khalil al Wazir maarufu kwa jina la Abu Jihad mwasisi na shakhsia nambari mbili wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO huko Tunis, Tunisia. Abu Jihad aliongozana na wenzake nchini Misri, na huko wakaamua kuanzisha harakati ya mapambano dhidi ya Wazayuni, na kuipatia jina la Harakati ya Ukombozi ya Palestina PLO.

Khalil al Wazir

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kuanzisha Shirika la Biashara Duniani (WTO) nchini Morocco. Utangulizi wa kuasisiwa shirika hilo ulifanywa na Marekani na Uingereza wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kwa msingi huo, mwaka 1947 nchi 23 zilizoendelea zilitia saini makubaliano ya kuanzisha GATT. Makubaliano hayo yalisisitiza juu ya kufanyika mazungumzo ya kupunguza ushuru wa forodha na vizuizi vya biashara huru. Baadaye jumuiya ya GATT ilibadilishwa jina na kuwa WTO na hati yake kuanza kutekelezwa Januari mwaka 1995. Hata hivyo Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeliteka shirika hilo la kibiashara duniani na kulitumia kwa faida na maslahi yao wenyewe.

Shirika la Biashara Duniani (WTO)