Apr 17, 2018 09:11 UTC
  • Aya na Hadithi (15)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi kingine cha Aya na Hadithi. Hakuna shaka kwamba kila mmoja wetu anapenda usomaji wake wa Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu uwe ni usomoji bora zaidi na unaostahiki kwa sababu tumemsikia Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenyewe akiwasifu na kuwataja kwa wema wale wanaosoma vyema kama inavyostahiki kusomwa na kukipa haki Kitabu chake hicho.

Lakini je, tutafikia vipi daraja na hatua hiyo ya watu wanaosoma kitabu hicho kwa njia bora zaidi na kukipa haki kinayostahiki? Kwa maneno mengine, ni vipi tutaweza kuwa miongoni mwa watu waliosifiwa na Mwenyezi Mungu kutokana na kusoma kwa njia bora na kama inavyostahiki kusomwa Kitabu chake kitakatifu? Hili ni swali muhimu ambalo tutajaribu kulijibu kupitia maandiko matakatifu ambayo tutayapitia katika kipindi hiki, hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

********

Wapenzi wasikilizaji, hebu kwanza tusikilize kwa makini Aya ya 121 ya Surat al-Baqarah ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Wale tuliowapa Kitabu, wakakisoma kama inavyostahiki kusomwa, hao ndio kweli wanakiamini. Na wanaokikataa basi hao ndio wenye hasara.

Ni wazi kuwa uzingatiaji wa Aya hii unatupa jibu jumla la swali tulilouliza mwanzoni mwa kipindi kuhusiana na usomaji sahihi, bora na unaostahiki wa Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu, nao ni usomaji unaotokana na imani kuwa Kitabu hiki ni cha Mwenyezi Mungu ambacho ndani yake mna mwongozo. Kwa maana kuwa usomaji wa Aya zake zenye mwongozo mtakatifu unaambatana na neema tukufu ambayo tunapaswa kunufaika nayo kwa ajili ya kuepuka hasara. Lakini je, jambo hilo linathibiti vipi? Swali hili linajibiwa na Hadithi ambazo zimenukuliwa na Allama Tabatabai (MA) katika Tafsiri yake ya al-Mizaan ambapo Imam Swadiq (as) amenukuliwa akisema kuhusiana na Aya hii ya Wale tuliowapa Kitabu, wakakisoma kama inavyostahiki kusomwa, kwamba: 'Husoma Aya zake taratibu na kutafakari maana yazo. Hutekeleza kimatendo mafundisho yake, kutumainia ahadi zake, kuogopa onyo zake na kupata ibra kutokana na visa vyake. Hutekeleza amri za aya hizo na kuepuka makatazo yake. Wallahi maana halisi ya haki ya kusoma (Kitabu/Qur'ani) ni hii, na sio kuhifadhi tu Aya zake, kufundisha herufi zake, kusoma Sura zake wala kuzijua Sura hizo kwa mafungu ya Sura kumi kumi au tano tano. Watu wamehifadhi na husoma na kutamka vizuri herufi za Aya hizo lakini wamekiuka mipaka (maana/mafundisho) yake. Bali maana ya kusoma Kitabu kama inavysostahiki ni kutafakari na kuzingatia Aya zake pamoja na kutekeleza mafundisho yake, kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Aya ya 29 ya Surat Swaad: Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili.'

Hadithi hii tukufu iko wazi na kamilifu zaidi katika kubainisha mfano wa usomaji sahihi na unaostahiki wa Kitabu Kitakatifu. Imam Swadiq (as) anabainisha kwamba haki ya usomaji bora na unaofaa wa Qur'ni Tukufu unampasa msomaji kusoma kwa makini huku akizingatia maana ya Aya za kitabu hicho cha mbinguni kama utangulizi wa kufanyia kazi mafundisho yake, kwa upande mmoja na kujiepisha na kila aina ya upotovu wa kimaanawi kwa upande wa pili. Na hili ndilo jambo analolizungumzia Imam Hassan al-Mujtaba (as) katika hotuba yake muhimu ambayo imenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi ambapo tutakusomeeni hivi punde sehemu ya hotuba hiyo, endeleeni kuwa nasi.

Imam Hassan al-Mujtaba (as) anasema:

'Tambueni kwamba hamtajua maana ya uongofu (haki) hadi mjue ni nani aliyeuwacha, hamtatekeleza agano la Kitabu hadi mjue ni nani aliyelivunja, hamtashikamana nalo hadi mjue aliyelikiuka, hamtasoma Kitabu kama inavyostahiki kusomwa hadi mjue ni nani aliyepotosha usomaji wake, hamtajua upotovu hadi mjue uongofu na hamtajua takwa hadi mjue aliyevuka mpaka. Ni baada ya kuyajua hayo ndipo mtakapojua bidaa (uzushi) na changamoto zilizopo na kuweza kuona vyema tuhuma (uongo) zinazotolewa dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake pamoja na upotoshaji wa Kitabu chake. Hapo ndipo mtakapoweza kuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyowaongoza aliowaongoza. Hivyo basi wasikupotezeni wale wasiojua kwa sababu hawaijui elimu ya Qur'ani isipokuwa wale waliokwishaonja utamu wake na wakaitafuta kutoka kwa wale wanaoijua vyema (Ahlul Beit as) kwa sababu ni wao tu ndio waliopewa nuru ambayo hutumika kuangazia njia (kuelekea kwenye haki). Ni Maimamu wanaofuatwa, wanaohuisha elimu na kutokomeza ujahili.'

Wao ndio wale ambao hekima yao hukufahamisheni elimu yao, kimya chao hukujulisheni mantiki yao na dhahiri yao batini yao. Huwa hawakhalifu dini wala kuhitilafiana kwayo. Hivyo Qur'ani kwao ni shahidi mkweli na mkimya anayezungumza. Huwa hawakhalifu haki wala kuhitilafiana kwayo. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka sunna miongoni mwao na kutekeleza sheria kupitia kwao. Katika hilo kuna zingatio kwa wanaozingatia. Hivyo basi kila mnaposikia maneno ya Maimamu Maasumu (as) yazingatieni kwa makini na sio kuyasikiliza kijuu juu tu. Hii ni kwa sababu wapokezi wa kitabu ni wengi lakini wanaokilinda ni wachache, na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kutegemewa.'

 

Wapenzi wasikilizaji, na kwa hotuba hii ya kuvutia ya Imam Hassan (as) inabainika wazi kwamba usomaji bora na unaostahiki wa Qur'ani Tukufu unathibiti kwa kunufaika na milango ya elimu ya kizazi cha Mtume Mtukufu (saw), ambao ndio wajuzi wa maana halisi ya mafundisho ya Qur'ani na kujiepusha na maoni ya watu wanaotafsiri kitabu hicho cha mbinguni bila ya kuwa na elimu ya kutosha na safi kama ile waliyonayo watukufu wa Nyumba ya Mtume (saw).

Na kwa natija hii ndio tunafikia mwisho wa sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.