Apr 30, 2018 03:47 UTC
  • Jumatatu, tarehe 30 Aprili, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Shaaban, 1439 Hijria sawa na Aprili 30, 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 241 iliyopita, alizaliwa Carl Friedrich Gauss mwanahisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani. Mama yake Gauss ndiye aliyemshawishi mno mwanawe ajikite zaidi katika somo la hisabati, na hatimaye mtoto huyo alitabahari kwenye fani hiyo. Msomi huyo wa hisabati na mnajimu mashuhuri wa Kijerumani alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 78.

Carl Friedrich Gauss

Tarehe 30 Aprili mwaka 1945 dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa mafichoni chini ya ardhi baada na kufeli ndoto yake ya kutawala dunia nzima. Hitler alizaliwa mwaka 1889 nchini Austria na alipigana Vita vya Kwanza vya Dunia katika safu za kwanza za askari wa Ujerumani. Adolf Hitler alianzisha chama cha National Socialist German Workers baada ya kuchanganya itikadi za kisoshalisti na mitazamo mikali ya utaifa. Na ulipotimia mwaka 1939 alianzisha Vita vya Pili vya Dunia.

Adolf Hitler

Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita alifariki dunia malenga, mwandishi na msanii wa uchoraji wa zama hizi wa Iran, Ustadh Ismail Ashtiyani. Baada ya masomo ya msingi na upili, Ustadh Ashtiyani alijifunza sanaa ya kuchora kwa msanii mashuhuri wa zama hizo Kamalul Mulk. Mwaka 1307 Hijria Shamsia alishika wadhifa wa mkuu wa Chuo cha Sanaa cha Darul Funun. Miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na diwani ya mashairi, Kumbukumbu ya Ulaya na Historia ya Kamalul Mulk.

Ustadh Ismail Ashtiyani

Tarehe 10 Ordibehesht miaka 39 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na Misri. Amri ya kukatwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri ilitolewa na hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Saadat kutia saini makubaliano ya aibu na fedheha ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusaliti malengo ya Wapalestina. Kutiwa saini makubaliano hayo ilikuwa hatua ya kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Palestina na kusaliti haki za Wapalestina waliokuwa wakipambana na utawala haramu wa Israel na vilevile kupuuza maslahi ya Umma wa Kiislamu. Baadaye kiongozi huyo wa Misri alitiwa adabu na shujaa, Khalid Islambuli aliyemmiminia risasi na kumuua kutokana na usaliti huo.

Anwar Saadat

 

Tags