Ijumaa, tarehe 4 Mei, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 17 Shaabani 1439 Hijria sawa na Mei 4, 2018.
Tarehe 4 Mei miaka 48 iliyopita wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha serikali cha Kent katika jimbo la Uhio nchini Marekani waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Gadi ya Taifa na wengine kadha wakajeruhiwa katika maandamano ya Wamarekani ya kupinga vita vya Vietnam. Kuanza mwaka 1969 Wamarekani hususan vijana walizidusha upinzani na maandamano ya kupinga vita na uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Vietnam. Maandamano hayo yalishadidi baada ya kufichuliwa habari ya mauaji ya mamia ya Wavietnam katika kijiji cha My Lai (My Lai massacre) na vilevile mwaka 1970 baada ya kuchapishwa habari ya kupanuka zaidi vita vya Vietnam na kuingia Cambodia.
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la chama cha Nazi, kilivunjwa rasmi nchini humo. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu cha chama hicho ambacho kiliingia madarakani tangu mwaka 1932 nchini Ujerumani, kilifikia ukingoni. Si vibaya kuashiria hapa kuwa, chama cha Nazi kiliundwa mwezi Oktoba mwaka 1920 baada ya kuongezeka harakati ya kisiasa za Munich. Hadi mwaka 1929 chama hicho kilikuwa na wanachama laki moja na 76 elfu tu lakini mwaka 1933 idadi hiyo iliongezeka na kufikia milioni mbili na kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni sita katika miaka iliyofuata. Inaelezwa kuwa, chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu ambalo lingeweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Nazi kilisambaratika na kutoweka.

Na siku kama ya leo miaka 1012 iliyopita alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari katika mji wa Herat nchini Afganistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nudhumu, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mahabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."