May 14, 2018 06:13 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Mei 14

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita..

Wanawake wa Iran watwaa ubingwa wa Futsal Asia

Timu ya taifa ya wanawake ya futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya mchezo huo barani Asia mwaka huu 2018, baada ya kuichabanga Japan mabao 5-2 katika mchuano wa fainali siku ya Jumamosi. Akina dada hao wa Kiirani walitawala mchezo huo uliopigwa katika Ukumbi wa Huamark katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok. Sara Shirbeigi ndiye aliyefungua mvua ya mabao ya Iran kunako dakika ya 28, na dakika mbili baadaye, Fereshteh Karimi akaipa Iran la pili. Shirbeigi aliongeza la pili na la tatu, na kwa msingi huo akawa amefunga hatrick.

Wachezaji wa kike wa Iran wakishangilia bao

 

Bao la 5 na la ushindi la mabinti hao wa Iran lilifungwa na Fahimeh Zarei. Baada ya ushindi huo wa kishindo na wa aina yake, wachezaji hao wa kike wa Iran wa mchezo wa futsal walitunukiwa Kombe la Asian Football Confederation (AFC) Women's Futsal Championship.

Mwenyeji Thailand iliibuka ya tatu baada ya kuichachafya Vietnam mabao 3-2 katika upigaji penati, baada ya dakika za ada kuishia kwa sare tasa. Rais Hassan Rouhani, Rais wa Shirikisho la Soka Iran, Mehdi Taj, mkufunzi wa timu ya taifa ya soka ya Iran, Carlos Queirroz na Spika wa Bunge la Iran, Ali Larijani ni miongoni mwa shakshia waliotuma salamu za pongeza kwa timu hiyo ya taifa ya futsal ya wanawake kwa ushindi huo, ambao kwa mara nyingine umelipa fahari taifa la Iran. Mashindano hayo ya kieneo yalianza Mei 2 na kumalizika Mei 12.

Wanamieleka wa Iran waibuka kidedea Uzbekistan

Timu ya taifa ya mieleka mtindo wa Free Style ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka kidedea katika Mashindano ya Asian Cadet Championships nchini Uzbekistan. Hii ni baada ya wanamieleka wa Iran kuzoa medali lukuki katika mashindano hayo ya kikanda, ambayo yalifunga pazia lake siku ya Jumapili.

Iman Sadeqi, moja wa wanamieleka bingwa wa freestyle wa Iran

 

Iran ilizoa jumla ya medali 8, zikiwemo 6 za dhahabu. Timu hiyo ya taifa ya mieleka mtindo wa Free Style ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa taji hilo la kieneo kwa kuzoa jumla ya alama 196, mbele ya wenyeji Wakazaki walioambulia pointi 171, huku Uzbekistan ikifunga orodha ya tatu bora kwa kuchota alama 146, katika mashindano hayo yaliyoanza Mei 10 na kufikia tamati Mei 13 nchini Uzbekistan.

Klabu ya Simba yanguruma, yatwaa Ligi ya Soka Tanzania Bara

Klabu ya Simba imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu huu wa 2017/2018, lakini nje wa uwanja. Hii ni baada ya mahasimu wao wa jadi klabu ya Yanga kufungwa mabao 2-0 na wanagereza, klabu ya Prisons katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya siku ya Alkhamisi. Hata hivyo siku ya Jumamosi Simba ikiwa ugenini katika Uwanja wa Namfua ilivaana na Singida United na kufanikiwa kupata ushindi mwembamba wa goli 1-0. Bao hilo la kipekee na la ushindi la Simba lilifungwa na beki wa kupanda na kushuka, Shomari Kapombe kunako dakika ya 23, baada ya kutumia makosa ya mabeki wa United baada ya kugongana wenyewe na kuacha mpira ukizagaa eneo la hatari.

Wachezaji wa Simba wakiwa uwanjani

 

Kwa matokeo hayo Simba imeendelea kuweka rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote msimu huu na kujikita kileleni ikiwa na pointi 68 ikifuatiwa na Azam FC wenye 52. Yanga ambao walicharazwa mabao 2-0 na Prisons wanasalia na alama 48. Kwa kutwaa ubingwa huo, Simba itaiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2019. Afisa Habari wa Wekundu wa Msimbazi, Haji Manara anasema Jumanne ijayo itakuwa siku ya kutoa madukuduku yake yote ya moyoni.

AFCON U20: Ngorongoro ya Tanzania yanyolewa na Mali

Timu ya taifa ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 20 ya Tanzania, Ngorongoro Heroes, siku ya Jumapili walishindwa kutamba mbele ya Mali licha ya kukipiga nyumbani katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam. Ngorongoro ilikubali kichapo cha mabao 2-1, katika mechi hiyo ya raundi ya pili ya kuwania kufuzu Michuano ya Afrika kwa vijana wa umri huo ambapo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Niger. Ousmane Diakite aliwapa wageni bao la kwanza katika dakika ya 33, na dakika 7 baadaye wakapiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Ngorongoro kupitia bao lililotokana na mkwaju wa adhabu. Bao la kufutia machozi la vijana wa Tanzania lilifungwa na mshambuliaji wa klabu ya Azam, Paul Peter katika dakika ya 44, baada ya kipa wa Mali kutema mpira wa iqabu.

Mashabiki wa Ngorongoro wamembebesha lawama zote mkufunzi huyo kwa kutomchezesha kipa mahiri Ramadhani Kabwili ambaye alitofautiana naye kabla ya mchezo. Ngorongoro imefika hatua hiyo baada ya kuizaba Congo DR mabao 6-5 katika mikwaju ya penalti.

Klabu za Afrika zavaana na miamba ya soka Ulaya

Mabingwa wa Ligi ya Kandanda nchini Kenya klabu ya Gor Mahia waliilazimisha klabu ya Uingereza ya Hull City sare tasa katika mchuano wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa Jumapili katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi, na hivyo timu hizo zikalazimika kuingia kwenye upigaji penati. Gor Mahia walilambishwa mabao 4-3 katika penati, lakini mashabiki wengi wameipongeza klabu hiyo inayofahamika pia kama Kogalo kwa kuitoa jasho timu ya Uingereza na kuilazimisha sare tasa katika dakika za ada. Hull City ambayo ipo katika Ligi ya daraja la Pili EFL nchini Uingereza, imevaana na Gor takriban mwaka mmoja baada ya Kogalo kuchachawizwa mabao 2-1 waliposhuka dimbani kucheza na klabu ya Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza Everton, katika mechi nyingine ya kimataifa ya kirafiki.

Mchuano wa Gor na Hull uwanjani Kasarani, Nairobi

 

Huku hayo yakiarifiwa, klabu ya Mamelody Sundowns ya Afrika Kusini imethibitisha kuwepo kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa Uhispania, Barcelona. Mchezo huo utachezwa Mei 16 katika Uwanja wa FNB ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kusherekea miaka 100 tangu kuzaliwa kwa baba wa taifa hilo, mwendazake Nelson Mandela. Hii itakuwa mara ya pili kwa klabu hizo kucheza nchini Afrika Kusini, mara ya kwanza ilikuwa 2007 ambapo Barcelona ilishinda mabao 2-1. Shirikisho la Soka Afrika Kusini, SAFA tayari limethibitisha kuwepo wa mchezo huo wa kukata na shoka utakaopigwa siku ya Jumatano

……………………..TAMATI…………………

 

 

Tags