Jumanne, 15 Mei, 2018
Leo ni Jumanne tarehe 28 Shaaban 1439 Hijria mwafaka na tarehe 15 Mei 2018 Miladia.
Siku ya leo inayosadifiana na tarehe 25 Ordibehesht Hijria Qamaria, alifariki dunia Abul Qassim Ferdowsi, mwanafalsafa na malenga mashuhuri wa Iran. Inasemekana kuwa, Ferdowsi alizaliwa mwaka 319 au 320 Hijria Shamsia katika mji wa Tus, kaskazini mashariki mwa Iran. Miongoni mwa athari muhimu za malenga huyo wa Kiirani ni kitabu alichokipa jina la "Shahnameh Ferdowsi". Kitabu hicho kilichosheheni historia ya jadi na utamaduni wa Iran kabla ya ujio wa Uislamu, kimefasiriwa kwa lugha mbali mbali. ***

Tarehe 15 Mei miaka 242 iliyopita katika siku kama hii ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke. Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin. Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini. ***
Miaka 160 iliyopita alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa. Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho kilianza kuonekana tokea ujana wake, na hatimaye kuibuka kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre. Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906. ***
Katika siku kama ya leo sawa na tarehe 15 Mei 1919 mji wa Izmir moja ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi. Mji wa Izmir uko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianziwa katika mji huo wa kihistoria. ***
Na miaka 78 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 15 Mei mwaka 1940, jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru wake mwaka 1945.