May 28, 2018 04:13 UTC
  • Jumatatu, Mei 28, 2018

Leo ni Jumatatu mwezi 12 Ramadhani 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 28 Mei 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa Kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhamia Madina akitokea Makka, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha na kuwanusuru Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu wa Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.

Kuunganisha udugu

 

Siku kama ya leo yaani mwezi 12 Ramadhani kwa mujibu wa wapokezi wengi wa kalenda ya Hijria Qamaria, ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.

Injili ya Kale

 

Tarehe 12 Ramadhani miaka 842 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.

Ibn Jawzi

 

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliafikiana na fikra ya kubuniwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ambapo mwanzoni ilizijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 likaanza shughuli zake za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974 PLO ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa ambapo kufikia mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia. Taratibu PLO ilianza kupoteza muelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo kufikia mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, ilikubali kuutambua rasmi utawala huo kwa kutia saini mapatano ya Oslo hapo mwaka 1993.

Chama cha Ukombozi wa Palestina PLO

 

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi. Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 Milaadia wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa. Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili, shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1930 hadi 1974 na kisha akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.

Mengistu Haile Mariam

 

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, kwa mara ya kwanza Pakistan ilifanya majaribio matano ya nyuklia. Majaribio hayo yalifanyika wiki mbili baada ya India, jirani yake hasimu, kufanya majaribio ya nyuklia. Kwa msingi huo mashindano ya majaribio ya mabomu ya nyuklia yakaibuka kati ya maadui hao wawili wa muda mrefu. Majaribio ya nyuklia ya Pakistan yaliibua hasira ya nchi za Magharibi ambazo ziliamua kuiwekea vikwazo vya kiuchumi. Pamoja na hayo, lakini hadi sasa Pakistan haijakubali mashinikizo ya nchi hizo ya kuitaka itie saini mkataba wa kuzuia uzalishaji na usambazaji wa silaha za nyuklia NPT.

Bomu la nyuklia

 

Na siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alifariki dunia Eugène Burnouf, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufaransa. Burnouf alizaliwa mjini Paris mwaka 1801 Miladia na kuhitimu somo la sheria. Hata hivyo kupendelea sana kusomea lugha na fasihi sambamba na kuvutiwa na masuala ya Mashariki ya Kati, kulimfanya ajifunze lugha za Sanskrit na Iran ya kale. Kadhalika Eugène Burnouf alijifunza utamaduni wa nchi za Iran na India. Moja ya kazi zilizozifanya msomi huyo ni pamoja na kufasiri sehemu za kitabu cha Avesta. Vitabu vya ‘Dondoo za Yasna’ ‘Historia ya dini ya Mabudha’ na ‘Babr Bayan’ ni miongoni mwa athari za Eugène Burnouf.

Eugène Burnouf

 

 

Tags