Jun 02, 2018 22:08 UTC
  • Jumapili, Juni 3, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 18 Ramadhan mwaka 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 3 Juni 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 516 iliyopita Vasco da Gama mwanabaharia wa Ureno alitekeleza mauaji ya umati na ya kinyama huko Calicut India. Calicut ambayo hii leo inajulikana kwa jina la Kozhikode au Kolkata ni bandari iliyoko Madras kusini mwa India. Hii ndiyo iliyokuwa sehemu ya kwanza kwa Vasco da Gama kutua na kuiteka katika safari yake ya kuelekea India mwaka 1498. Kama walivyokuwa wakoloni wenzake, alijichukulia kuwa mmiliki halisi wa India. Wakati wafanyabiashara 800 wa Kiarabu walipofika katika eneo hilo kwa lengo la kufanya biashara ya mchele, Vasco da Gama alitoa amri ya wafanyabiashara hao kukatwa mikono, masikio na mapua na kisha kuwaua kwa umati baada ya kuteketeza meli zao.

Bandari ya Calicut India

Siku kama ya leo miaka 351 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya tiba na upasuaji, kitendo cha kuongezwa damu katika mwili wa binadamu kilifanyika. Damu hiyo iliwekwa kwenye mwili wa mwanadamu na tabibu wa Kifaransa aliyeitwa Jean Baptiste Denis. Utiaji damu huo kwa wagonjwa, ulihesabiwa kuwa tukio na mafanikio makubwa katika sayansi ya tiba. Hii ni kwa sababu zama hizo wagonjwa wengi walipoteza maisha yao kutokana na kuvuja damu nyingi na ukosefu wa damu. Katika jaribio lake la kwanza, tabibu huyo wa Kifaransa alichukua damu ya kondoo na kuitia katika mwili wa mwanadamu, na baadaye akawa anawaongeza wagonjwa damu ya wanadamu.

Jean Baptiste Denis

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita alizaliwa, Jacques de Morgan, mtaalamu wa historia ya maumbile na mwanasayansi wa masuala ya ardhi wa nchini Ufaransa. Awali alisafiri nchi tofauti kwa ajili ya kuvumbua madini mbalimbali ambapo kwa muda fulani alijishughulisha pia na uvumbuzi wa masuala ya historia nchini Misri. Tangu mwaka 1889 Miladia na kwa muda wa miaka mitatu Morgan alifanya utafiti kuhusiana na masuala ya kale nchini Iran huku akiandika vitabu katika uwanja huo. Kuanzia mwaka 1889 na kuendelea kwa miaka 15 baadaye alikuwa msimamizi wa kamisheni ya masuala ya kihistoria nchini Ufaransa ambapo aliendeleza utafiti wake katika maeneo mbalimbali ya dunia. Jacques de Morgan alifariki dunia mwaka 1924. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'Mwanadamu Kabla ya Historia' 'Operesheni ya Kielimu Mjini Paris' na 'Utangulizi wa Historia ya Mashariki.'

Jacques de Morgan

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, alizaliwa Mirza Abdul-Adhim Khan Qarib, mtaalamu wa fasihi na mtafiti mkubwa wa Iran huko mjini Gorgan moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya masomo yake ya awali, alianza kufanya utafiti katika elimu ya swarfu, nahw, mantiki, hisabati na fasihi na kufikia daraja ya ualimu katika elimu hizo. Khan Qarib ameandika vitabu vingi kuhusiana na lugha ya Kifarsi moja ya vitabu hivyo kikiwa ni kitabu cha ‘Kanuni za Kifarsi’ na ‘Mwanzo wa Fasihi na Faida za Fasihi.’

Mirza Abdul-Adhim Khan Qarib

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, alifariki dunia Nazim Hikmet malenga mashuhuri wa Kituruki. Alizaliwa mwaka 1902 na kuanza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 12. Malenga huyo wa Kituruki alijiunga na jeshi la nchi hiyo baada ya kuhitimu masomo yake ya shule ya upili. Lakini mwaka 1920, Nazim Hikmet alijiondoa jeshini kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Kisha alielekea Moscow mji mkuu wa Urusi ya zamani kwa ajili ya kuendelea na masomo yake na baadaye akarejea Uturuki baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu katika taaluma ya uchumi wa kisiasa. Baada ya hapo, Nazim Hikmet alianza kutunga mashairi ya kimapinduzi dhidi ya ufashisti, yaliyokuwa yakiukosoa utawala wa kidikteta wa Ataturk, rais wa kwanza wa Uturuki.

Nazim Hikmet

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita Imam Khomeini (M.A), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba kali ya kihistoria dhidi ya utawala wa kitwaguti wa Iran, kwa mnasaba wa Ashura ya Imam Husseini (A.S). Imam Khomeini alitoa hotuba hiyo mbele ya hadhara kubwa ya wananchi na wanazuoni katika Madrasa ya Faidhiya katika mji mtakatifu wa Qum hapa nchini, licha ya vizuizi na vitisho vya utawala wa Shah. Imam alikosoa vikali usaliti wa utawala wa Shah na vibaraka wake dhidi ya wananchi Waislamu wa Iran. Sehemu ya hotuba ya Imam Khomeini ilisema hivi kama ninavyomnukuu: "Watu hao wanapinga Uislamu na wanazuoni na wana nia ya kuutokomeza. Enyi wananchi, dini yetu ya Kiislamu na nchi yetu viko hatarini na tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Iran." Mwisho wa kunukuu.

Imam Khomeini (M.A)

Na siku kama ya leo miaka miwili iliyopita alifariki dunia Muhammad Ali Clay, bondia wa kihistoria wa uzani mzito wa nchini Marekani. Muhammad Ali ambaye zamani alikuwa akiitwa Cassius Marcellus Clay Jr. alizaliwa tarehe 17 Januari 1942 Miladia na kutokea kupata umashuhuri mkubwa katika ndondi za uzani mzito. Baada ya kubadili dini na kujiunga na Uislamu, alijihusisha na harakati za kisiasa na ni kwa ajili hiyo ndio maana alitokea kuwa mashuhuri kuliko wanamichezo wengine duniani. Aidha katika karne ya 20 alikuwa mmoja wa mabingwa wakubwa wa michezo duniani. Muhammad Ali Clay alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74 katika siku kama ya leo baada ya kusumbuliwa na maradhi ya Parkinson kwa miaka 32 ambao mwishoni ulimsababishia matatizo ya kupumua.