Jun 06, 2018 02:26 UTC
  • Jumatano, Julai 6, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 21 Ramadhani, mwaka 1439 Hijria, inayosadifiana na tarehe 6 Juni, 2018 Miladia.

Miaka 1399 iliyopita, katika siku kama ya leo, yaani tarehe 21 Ramadhani mwaka 40 Hijria, alikufa shahidi Imam Ali bin Abi Talib AS, ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume Mtukufu SAW. Imam Ali AS alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiswali Sala ya alfajiri katika Msikiti wa Kufa nchini Iraq, siku mbili kabla ya yeye kufa shahidi kutokana na jeraha hilo. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili mkubwa baada ya Mtume Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa alikuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na mwadilifu. Alipata elimu na mafunzo kwa Mtume Mtukufu SAW na alikuwa mwanamume wa kwanza kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na alihatarisha hata maisha yake kwa ajili ya kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji shupavu, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo. Alipenda haki na uadilifu na kupambana ipasavyo na dhulma katika kila njanya.

 

@@@@@@@@@@

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, yaani tarehe 16 Khordad mwaka 1368 Hijria Shamsia, mwili mtoharifu wa Imam Khomeini (MA) ulizikwa hapa mjini Tehran katika maziko yaliyohudhuriwa na wimbi la mamilioni ya watu waliokuwa na majonzi makubwa. Zaidi ya waombolezaji milioni kumi kutoka miji mbalimbali ya Iran na nje ya Iran walishiriki katika maziko hayo ambayo hayajawahi kutokea mfano wake. Moja ya sifa za kipekee za maziko hayo ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambaye alitumia umri wake wote kwa ajili ya ukombozi na kuwaletea heshima wanadamu, ni wimbi kubwa mno la mamilioni ya watu walioshiriki kwenye maziko hayo. Maziko hayo yalikuwa ni medani adhimu ya kuonesha imani na mapenzi ya wananchi wa Iran na wa maeneo mengine mengi duniani kwa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu awe radhi naye) na kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran. Hivi sasa haram ya mwanachuoni huyo mkubwa iko pembeni mwa maziara matoharifu ya maelfu ya mashahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kusini mwa Tehran. Wapenzi wa mwanachuoni huyo kutoka kona zote za dunia hufanya ziara kwenye haram yake na kumuombea dua za kupandishwa daraja kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Haram ya Imam Khomeini MA

@@@@@@@@@@

Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 6 Juni 1901 Milaadia, alizaliwa Ahmad Sukarno, baba wa ukombozi wa Indonesia na rais wa kwanza wa nchi hiyo kubwa ya Kiislamu ya kusini mashariki mwa Asia. Baada ya kumaliza masomo yake ya upili aliendelea na masomo yake katika masuala ya uhandisi hasa fani ya usanifu majengo hadi alipofikia daraja ya uzamivu katika fani hiyo. Ahmad Sukarno alijihusisha na masuala ya siasa tangu akiwa mwanafuzi. Mwaka 1926, aliviandaa vyama vya wenyeji wa Indonesia kuanzisha vita na wakoloni wa Uholanzi. Wakoloni ambao hawakupenda kabisa kusikia neno uhuru, walimtia mbaroni mara kadhaa Ahmad Sukarno na mwaka 1940 wakamfukuza katika kisiwa cha Java na kumbaidishia kisiwani Sumatra. AAhmad Sukarno alitoa mchango mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya Wajapani katika Vita vya Pili vya Dunia. Wakati Indonesia ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uholanzi mwaka 1945, Ahmad Sukarno alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Ahmad Sukarno, Rais Tito wa Yugoslavia na Rais Abdel Nassir wa Misri ndio waasisi wakuu wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote, NAM.

Ahmad Sukarno

@@@@@@@@@@

Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 6 Juni 1966 Milaadia, merikebu ya kwanza isiyo na rubani ilitua juu ya mwezi. Baada ya kupamba moto ushindani wa teknolojia ya anga za mbali baina ya Marekani na Umoja wa Kisovieti hasa katika suala la kuizunguka dunia, mwaka 1966 Milaadia, kilianza kipindi kipya cha ushindani baina ya nchi hizo mbili. Awali, tarehe 4 Aprili 1966, merikebu ya Umoja wa Kisovieti iliuzunguka mwezi kwa mara ya kwanza na kutuma picha zake ardhini kutoka masafa hayo ya mbali. Jambo hilo liliongeza ushindani baina ya madola mawili makubwa wakati huo, na tarehe 6 Juni mwaka huo huo, merikebu ya kwanza ya Marekani isiyo na rubani ilitua juu ya mwezi na kutuma taarifa ardhini kutoka juu ya mwezi. Kasi ya teknolojia hiyo iliongezeka sana baada ya hapo na ilipofika tarehe 21 Julai 1969, raia mmoja wa Marekani akaweka mguu wake kwa mara ya kwanza juu ya mwezi.

Mtu wa kwanza kuweka mguu wake juu ya mwezi

@@@@@@@@@@

 

 

Tags