Jumatatu tarehe 11 Juni 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 26 Ramadhani 1439 Hijria sawa na 11 Juni 2018
Miaka 446 iliyopita na katika siku kama ya leo Ben Jonson, mwandishi wa michezo ya kuigiza na muigizaji mashuhuri wa Uingereza alizaliwa katika familia masikini. Alilazimika kufanya kazi za mikono katika sekta ya ujenzi akiwa na baba yake wa kambo ili kujidhaminia karo ya shule. Baada ya kuhitimu masomo ya juu alijiunga na jeshi la nchi hiyo akiwa na umri wa miaka 29 lakini bado jambo hilo halikumpa utulivu wa moyo, na hivyo akalazimika kuondoka jeshini. Aliingia kwenye uwanja wa michezo ya kuigiza kama muigizaji na kisha kuanza kuandika michezo hiyo mwenyewe. Aliishi katika zama za Shakespeare, mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza na kushirikiana naye kwa karibu. Katika michezo yake, Ben Jonson alikuwa akiwakejeli mabwanyenye na viongozi wa makanisa jambo lililowakasirisha sana. Hata hivyo umasikini na matatizo mengine yalimwandama Jonson hadi mwishoni mwa maisha yake hapo mwaka 1637.
Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen. Si vibaya kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio ka kuvutia ambalo linasababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Haitham na Qutbuddin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

Na miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari Muhammad Khazaaili, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na Kuwasaidia Vipofu ya Iran. Dakta Khazaaili alipokuwa mtoto alipoteza uwezo wa kuona kutokana na ugonjwa wa ndui. Alipata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, msomi huyo alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kuhitimu shahada ya uzamilifu ya sheria katika chuo kikuu cha Tehran. Dakta Khazaaili alifahamu vyema lugha za Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali. Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo Dakta Khazaaili ni kupigania huduma muhimu za vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la Kitaifa la kuwahudumia vipofu na katika Jumuiya ya Kimataifa ya Vipofu.