Jun 19, 2018 02:20 UTC
  • Jumanne, Juni 19, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 5 Mfunguo Mosi Shawwal 1439 Hijria sawa na 19 Juni, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, chombo cha kwanza cha kupaa angani, kilifanyiwa majaribio ya kutua au kubakia angani bila ya kuhitajia uwanja wa kutua. Chombo hicho ambacho kilipewa jina la helikopta, kilifanyiwa majaribio na Enrico Forlanini, mhandisi wa Kitaliano katika bandari ya Alexandria nchini Misri.

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita inayosadifiana na 29 Khordad 1330 Hijria Shamsia, baada ya kupitishwa sheria ya kutaifisha mafuta nchini Iran tarehe 29 Esfand 1329 Hijria Shamsia, jopo lililoundwa la wataalamu wa Kiirani, lilipewa jukumu la kuliongoza Shirika la Taifa la Mafuta la Iran. Jopo hilo liliundwa kutokana na mapendekezo yaliyotolewa na Ayatullah Kashani na Dokta Muswaddiq, na kupitishwa na Bunge na hatimaye Baraza la Seneti hapa nchini.

Shirika la Mafuta la Uingereza lilipokonywa sekta ya mafuta Iran

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.

Bendera ya Kuwait

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita inayosadifiana na 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati, mwandishi na msomi wa Kiirani wa zama hizi mjini London, Uingereza. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Dakta Ali Shariati aliingia kwenye uwanja wa siasa na kupambana dhidi ya utawala wa kifalme hapa nchini. Msomi huyo ameacha athari za vitabu kadhaa, miongoni mwa hivyo, ni Historia ya Ustaarabu', Uislamu na Mwanadamu' na Fatima ni Fatima.'

Dakta Ali Shariati

Na siku kama ya leo miaka 151 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo.

 

Tags