Jun 19, 2018 22:04 UTC
  • Jumatano, tarehe 20 Juni, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 6 Shawwal 1439 Hijria sawa na 20 Juni 2018

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita magaidi wa kundi la Munafiqin walitenda jinai kubwa ya kutisha katika haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) katika mji mtakatifu wa Mash'had. Bomu liliripuka ndani ya haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) alasiri ya siku ya Ashura mwaka huo wakati watu walipokuwa wakifanya ziara na marasimu ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya kuuawa shahidi Imam Hussein (a.s). Makumi ya waumini na wapenzi wa Ahlul Bait (a.s) waliuliwa shahidi au kujeruhiwa katika haram hiyo. Mlipuko huo ulisababisha hasara na maafa mengi katika haram hiyo tukufu.

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo msomi wa Poland kwa jina la Casimir Funk kwa mara ya kwanza kabisa alifanikiwa kugundua vitamin au virutubisho. Baada ya uhakiki mwingi Dakta Casimir Funk aligundua kwamba vyakula vinavyotumiwa na mwanadamu vina baadhi ya virutubisho (vitamins) ambavyo japokuwa ni vichache sana lakini vina udharura mkubwa katika ukuaji na usalama wa mwili na akaamua kuvipa jina la Vitamini.Kuna aina mbalimbali za vitamin kama A, B, C, D na E, na kila moja ina sifa za kipekee na matumizi ya aina yake katika mwili.

Casimir Funk

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita inayosadifiana na hii ya leo yaani tarehe 20 mwezi Juni mwaka 1875, Kisiwa cha Okinawa kinachopatikana katika bahari ya Pacific huko Japan kilidhibitiwa na jeshi la nchi hiyo. Hata hivyo mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia kisiwa hicho cha kistratijia chenye ukubwa wa kilomita mraba 1250 kilikaliwa kwa mabavu na majeshi ya Marekani licha ya mapambano makali ya jeshi la Japan. Jeshi la Marekani liliondoka Japan mwaka 1958 lakini kisiwa cha Okinawa kiliendelea kudhibitiwa na Wamarekani. Mwaka 1972 vikosi vya Marekani vilisitisha ukaliaji wa mabavu wa kisiwa hicho kufuatia mazungumzo marefu kati ya Washington na Tokyo.

Kisiwa cha Okinawa

Na siku kama ya leo miaka 653 iliyopita, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokeaji wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Bardes alizaliwa huko Ba'labak moja kati ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus baada ya kukamilisha masomo yake ya awali, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na akaanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhuri baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al Iilamu fii Wafayatil Aalam.