Jun 30, 2018 04:01 UTC
  • Jumamosi, Juni 30, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Mosi Shawwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe 30 Juni 2018 Miladia.

 

Siku kama ya leo miaka 929 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Ibn Azraq Faruqi, mtaalamu maarufu wa hadithi, fiqhi na historia. Katika kipindi cha ujana wake, Ibn Azraq alijifunza elimu ya fiqhi, hadithi lugha na tafsiri ya Qur'an Tukufu, na kutokana na kuwa alivutiwa mno na historia, ndipo akasomea pia elimu hiyo. Kwa upande mwingine ni Faruqi alifahamu tamaduni na historia mbalimbali za watu, kutokana na safari alizozifanya katika maeneo kadhaa ya dunia. Aliyaandika matukio aliyoyashuhudia katika safari zake hizo katika kitabu cha 'Taarikh al-Faruqi.' ***

Ibn Azraq Faruqi,

 

Miaka 58 iliyopita mwafaka na tarehe 30 mwezi Juni 1960, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yaani Zaire ya zamani ilitangaza uhuru wake. Kasavubu alichaguliwa kuwa Rais na Patrice Lumumba Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Kabla ya uhuru, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilikuwa ikikoloniwa na Wabelgiji. Mapambano ya wapigania ukombozi wa Kongo chini ya uongozi wa mpigania uhuru mashuhuri wa Kiafrika Patrice Lumumba yalifikia kilele miaka kadhaa baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea kukombolewa Zaire ya zamani. Hata hivyo baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake, serikali ya Ubelgiji ilihusika pakubwa katika kuzusha uasi mkubwa nchini humo. Aidha ulijiri mzozo kati ya Lumumba na Moise Tshombe kibaraka aliyekuwa na uhusiano wa wakoloni wa Kibelgiji na hivyo kuzidisha hali ya machafuko huko Zaire ya zamani. Nchi hiyo ilizidi kuwategemea wageni baada ya kuuawa Lumumba na vibaraka wa ndani. Hatimaye Mobutu Seseseko alichukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1965 kwa uungaji mkono wa Marekani na kuanza kuwakandamiza wananchi wa nchi hiyo. ***

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, sawa na tarehe 9 Tir 1365 Hijria Shamsia, ilianza operesheni ya kijeshi ya Karbala -1 kwa ajili ya kukomboa mji wa Mehran huko magharibi mwa Iran uliokuwa umetwaliwa na jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq. Mji huo ulikaliwa kwa mabavu muda mfupi baada ya jeshi la Baath la Iraq kuvamia ardhi ya Iran Septemba 1981 na ulikombolewa na wapiganaji shupavu wa Iran katika operesheni makini ya Karbala-1. ***

Operesheni ya Karbala-1

 

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo Jenerali Omar Hassan Ahmad al-Bashir aliipindua serikali ya Sadiq al-Mahdi iliyokuwa ikikabiliwa na migogoro ya ndani, katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu. Omar al-Bashir na Dakta Hassan Turabi waliunda chama cha Congres ya Taifa ya Sudan kabla ya mapinduzi hayo na wao ndio waliokuwa wakiongoza chama hicho na kushikilia madaraka ya nchi. ***

Omar Hassan al-Bashir

 

Na katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, mfumo wa ubaguzi wa rangi ulihitimishwa rasmi huko Afrika Kusini. Makaburu walio wachache wa Afrika Kusini waliwatwisha raia weusi wa nchi hiyo utawala wa ubaguzi wa rangi "Apartheid" tangu mwaka 1948 Miladia na kwa mujibu wa mfumo huo wa kibaguzi, asilimia 20 ya wazungu wachache wa Afrika Kusini walitambulika kama watu wa tabaka la juu na wenye madaraka ya kuainisha mustakbali na kuongoza nchi. Vilevile ndoa kati ya raia weusi na wazungu zilipigwa marufuku huko Afrika Kusini na wazalendo walizuiwa kuendesha shughuli za kisiasa. 

Nelson Mandela, shujaa wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini

 

Tags