Jul 01, 2018 01:47 UTC
  • Jumapili, Julai Mosi, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 17 Shawwal 1439 Hijiria, inayosadifiana na Julai Mosi mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 230 iliyopita alizaliwa Jean Victor Poncelet mwasisi wa uchambuzi wa maumbo. Victor Poncelet aliyekuwa mtaalamu wa hisabati maarufu wa nchini Ufaransa, alitambulika kuwa mwasisi wa uchambuzi wa maumbo na ambaye alizaliwa tarehe Mosi Julai 1788 Miladia. Aidha Poncelet alikuwa mmoja wa maafisa wa jeshi la Napolione na katika kipindi cha kurejea nyuma jeshi la Ufaransa kutoka Urusi ya zamani, alitekwa na Warusi. Hata hivyo katika kipindi cha kutekwa alijiendeleza kielimu na kufanikiwa kuhitimu elimu yake ya uhandisi. Jean Victor Poncelet alifariki dunia tarehe 22 Disemba 1867 Miladia.

Jean Victor Poncelet

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita alifariki dunia mjini Karbala, Iraq Sayyid Ibrahim Karbalai, mmoja wa maulama wa Kiislamu wa karne 13 Hijiria. Alizaliwa mwaka 1214 Hijiria nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea mjini Karbala kwa ajili ya kujiendeleza na masomo ya juu ya kidini ambapo hadi mwisho wa maisha yake aliendelea kusoma na kufundisha ndani ya mji huo. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyo mkubwa wa kidini ni pamoja na kitabu cha 'Dalaailul-Ahkaam' 'Nataaijul-Afkaar' na 'Risaalat fii Abwaabil-Hajj.'

Sayyid Ibrahim Karbalai

Siku kama ya leo miaka 151 iliyopita, nchi ya Canada ilijitangazia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Canada iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na kuanzia wakati huo kwa zaidi ya karne mbili, Uingereza na Ufaransa zilikuwa zikishindana katika ardhi ya nchi hiyo kwa lengo la kupanua udhibiti wao. Ushindani huo ulipelekea kujiri vita kati ya mataifa hayo ya kikoloni ambapo mwaka 1689 Miladia vita hivyo vilimalizika kwa kushindwa Ufaransa, katika vita hivyo ambavyo vilidumu karibu miaka 75. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 19 taratibu zilianza harakati za kupigania uhuru wa Canada ambapo zilizaa matunda mwaka 1867 Miladia katika siku kama ya leo.

Bendera ya Canada

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, sehemu mbili za Somalia ya Uingereza na ya Italia ziliungana na kuunda nchi moja ya Somalia yenye kujitawala. Karne kadhaa nyuma, Somalia iliwahi kujitawala kwa kipindi kifupi. Mwaka 1884 Uingereza iliiweka katika himaya yake sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Miaka mitano baadaye Italia nayo ikakoloni baadhi ya sehemu za Somalia. Harakati za mapambano za Muhammad Abdullah Hassan dhidi ya Waingereza kuanzia mwaka 1901 hadi 1920 hazikusaidia kitu. Mwaka 1950 Umoja wa Mataifa uliitaka Italia iandae mazingira ya kujitawala na kuwa huru Somalia.

Ramani ya Somalia

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, nchi ya Burundi ya barani Afrika ilijitangazia uhuru wake. Kwa miaka mingi, yaani kuanzia mwaka 1899 hadi 1917 Miladia nchi hiyo pamoja na Rwanda, zilikuwa ni makoloni ya Ujerumani eneo la Afrika Mashariki. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kufuatia kushindwa Ujerumani katika vita hivyo, jamii ya kimataifa iliiweka Burundi chini ya usimamizi wa Ubelgiji na mwaka 1946 usimamizi huo ukatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa. Mwaka 1962 Burundi ilijitenga na mfumo wa kiufalme lakini miaka minne baadaye wapiganiaji wa mfumo wa jamhuri nchini humo walimuuzulu mfalme na kutangaza serikali ya jamhuri. Burundi ina ukubwa wa karibu kilomitamraba elfu 28 eneo la mashariki mwa bara la Afrika huku ikiwa imepakana na nchi za Rwanda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hivi sasa nchi hiyo ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bendera ya Burundi

Na siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Rwanda ilipata uhuru. Rwanda ina historia inayofanana na jirani yake wa kusini yaani Burundi ambapo kabla ya nchi hizo kujitangazia uhuru zilikuwa zikikoloniwa na Ubelgiji. Mwaka 1973, Meja-Generali Juvenal Habyarimana alichukua madarakani baada ya kufanya mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu. Baada ya mapambano mtawalia ya wapigania uhuru wa Rwanda, hatimaye mnamo mwaka 1962, nchi hiyo ilipata uhuru na kabila kubwa la Wahutu likashika hatamu za uongozi wa nchi. Hata hivyo mwaka 1994 kulitokea mauaji ya kimbari ambapo zaidi ya watu laki 8 waliuawa wengi wao wakiwa ni wa kabila la Kitutsi.

Bendera ya Rwanda